Wednesday, November 7, 2018

TANZANIA KUSHIRIKI MAONESHO YA CIIE YATAKAYOFANYIKA SHANGHAI NCHINI CHINA

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii

KATIKA  kuendeleza mkakati wa kutangaza utalii wa Tanzania nchini China, Bodi ya Utalii Nchini (TTB) kwa kushirikiana na wadau wa Utalii wa Tanzania pamoja na Sekta ya Madini inashiriki onesho kubwa la biashara yaliyoandaliwa na Serikali ya China.

Maonesho hayo makubwa  yajulikanayo kama China International Impact Expo (CIIE) yatafanyika katika jiji la Shanghai kuanzia  5-10 Novemba, 2018 na  Kupitia maonesho haya, sekta ya madini itaudhihirishia ulimwengu kuwa Madini ya Tanzanite yanapatikana Tanzania tu. 

Akielezea safari hiyo ya nchini China, Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii  Jaji Mstaafu Thomas Mihayo amesema kuwa safari hiyo ya nchini China imeandaliwa na bodi ya utalii kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini China na Shirika la Ndege la Tanzania ATCL, wameandaa ziara ya utangazaji nchini China ambapo pamoja na kushiriki maonyesho ya CIIE watafanya ziara ya utangazaji katika miji mbalimbali.

Amesema miji hiyo ni Shanghai (12 Novemba, 2018), Guangzhou (14 Novemba, 2018), Hong Kong (16 Novemba, 2018), Chengdu (19 Novemba, 2018) na Beijing (20 Novemba, 2018). Misafara hii itatuwezesha kukutana na wafanyabiashara wa utalii wakubwa katika miji hiyo na wawekezaji wakubwa katika sekta ya utalii pamoja na vyombo vya habari mbalimbali vya China.

 Aidha, Mihayo amesema Shirika  la N dege la Tanzania (ATCL) litatumia ziara hii kama fursa ya kutangaza kuzinduliwa kwa safari mpya kwa kutumia ndege aina ya 4 Dreamliner kwenda katika mji wa Guangzhou.

 "Tunaamini ziara hii itasaidia kuongeza idadi ya watalii kutoka China.na  Ujumbe utakaoshiriki katika ziara utaongozwa na Naibu katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii akiongozana na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTB,'amesema Mihayo.

"China ni miongoni mwa masoko mapya yanayokuwa kwa kasi sana kwa Tanzania, na ni soko la sita miongoni mwa masoko yanayotuletea watalii wengi ambapo kwa takwimu za mwaka 2017Tanzania ilipokea watalii 29,224 kutoka China. Nchi ya kwanza ni Marekani (87,238); ikifuatiwa na Uingereza (66,491); Ujerumani (58,390); Italia (49,909) na India (39,115),"

Mihayo ameeleza, Taasisi zitakazoshiriki ni Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Hifadhi za Taifa (TANAPA), Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL), Kituo Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro(NCAA) na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS). Pamoja na Kampuni 15 za utalii kutoka Tanzania Bara na Viziwani.

Kwa upande wa Meneja Masoko na Usambazaji Edward Mkwabi amesema kuwa kuzinduliwa kwa safari za ndege hiyo kuelekea China kutatoa fursa kwa watalii, wafanyabishara pamoja na wanafunzi.

Mkwabi amesema kuwa, safari za ndege rasmi zitaanza mwezi Februari na ndege itapitia Bangkok kuelekea China, pia ili kuwapa fursa watumiaji wa ndege hiyo ya BOEING -DREAMLINER 787 itaondoka saa 7 usiku kwa siku za Jumanne, Alhamis na Jumamosi.

  Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB)  Jaji Mstaafu Thomas akizungumzia safari ya China na ushiriki wao wa Maonesho  makubwa  yajulikanayo kama China International Impact Expo (CIIE) yatafanyika katika jiji la Shanghai kuanzia  5-10 Novemba, 2018, Kushoto ni  Mihayo    Meneja Masoko na Usambazaji Edward Mkwabi.

No comments: