Friday, November 30, 2018

NDITIYE: TAKUKURU FUTUATILIENI UJENZI WA GATI YA BANDARI YA LINDI

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye ameilekeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia na kuchunguza thamani ya fedha zilizotumika kujenga gati ya bandari ya Lindi ili kuweza kubaini kama gharama iliyotumika inaendana na ujenzi uliofanyika
 
Hayo yameelezwa na Nditiye wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa gati ya bandari ya Lindi mkoani humo ambapo amebaini kuwa kasi ya utendaji kazi kwenye gati hilo hairidhishi na kuongeza kuwa kazi ni ya mwaka mmoja ila imechukua miaka mitatu hadi sasa na bado haijakamilika. “Naielekeza TAKUKURU waje wafuatilie thamani ya fedha zilizotumika kujenga gati hili,” amesema Nditiye. 

Nditiye amesema kuwa kwa bahati mbaya miradi ya maendeleo ya Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inayotekelezwa nje ya bandari ya Dar es Salaam haitekelezwi ipasavyo, tufike mahala tuheshimu fedha za Serikali na za wananchi. “Kwa bahati mbaya TPA hamfiki eneo la mradi wakati wa kuandaa nyaraka na hata ujenzi wa miradi husika inavyoendelea hivyo tunaingia hasara,”amesema Nditiye .

Mhandisi Ujenzi wa Bandari ya Mtwara Twaha Msita wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa gati hiyo kwa Nditiye amesema kuwa Kampuni ya Comfix & Engineering Ltd ilipewa kazi na TPA ya kujenga gati hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja kuanzia mwezi Mei mwaka 2015 na kutakiwa kukamilika mwezi Mei mwaka 2016 kuendana na mkataba husika kwa gharama ya shilingi bilioni 3.1 ambapo baada ya muda ilionekana kazi zimeongeza na hivyo kuongezewa fedha hadi kufikia shilingi bilioni 3.5 .

Nditiye amesema kuwa tayari mkandarasi amelipwa shilingi bilioni 2.448 na kazi hiyo ilisimama kwa kipindi cha mwaka mzima mwaka 2017 na kuanza tena ambapo hadi sasa haijakamilika na imechukua kipindi cha miaka mitatu tofauti na mkataba wa awali ambapo ilitakiwa ijengwe kwa kipindi cha mwaka mmoja. “Serikali hatuwezi kuvumilia jambo hili kwa kuwa tunawatesa wananchi kwa kukosa huduma na kutumia vibaya fedha za Serikali,” amesema Nditiye
 
Naye Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga amesema kuwa bandari ya Lindi ni muhimu sana kwa uchumi wa watu wa Lindi kwa kuwa tuna korosho na kiwanda cha Jeshi cha kubangulia korosho. Amekiri kuwa kazi hairidhishi na kuna tatizo la kujaa kwa mchanga hivyo tuombe wahusika wakamilishe ili bandari hii iweze kutoa huduma kwa wananchi .

Katika hatua nyingine, Nditiye ametoa rai kwa Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Phillip Mpango kuwachukulia hatua watendaji wa Mamlaka ya Mapato Tanzania wa Mkoa wa Lindi wanaosimamia Bandari ya Lindi kwa kuikosesha Serikali mapato kwa kuwasaidia wafanyabiashara kukwepa kodi na kuvusha biashara za magendo. “Wafanyakazi wa TRA waliopo bandari ya Lindi wameoza, Waziri wa Fedha na Mipango tafadhali safisha uozo huo kwa kuwa wamepitisha madumu ya mafuta 650 mwezi huu Novemba yaliyopakiwa Zanzibar na kushushwa Lindi yakiwa madumu 30 tu na kusema kuwa yako tupu,” amesema Nditiye. Pia, amefafanua kuwa alimuagiza Mkuu wa Wilaya awaite ila wamedharau na hawakufika kwenye kikao na ziara yake mkoani humo. 

Vile vile, amemuelekeza Mkuu wa Wilaya hiyo kushirikiana na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilayani humo kudhibiti bandari bubu zilizopo na kuwachukulia hatua wafanyabiashara wasio waaminifu wanaokwepa kodi, hivyo kuikosesha Serikali mapato kwa kufanya biashara za magendo kwa kutumia bandari bubu na kushusha mizigo na bidhaa zao kwenye pori lililopo karibu na eneo la Uwanja wa Ndege wa Lindi ambapo unaweza kuhatarisha usalama wa uwanja huo
Nditiye pia amekagua uwanja wa ndege wa Mkoa wa Lindi na kuwaeleza kuwa uwanja huo umewekwa kwenye viwanja 11 na Serikali ambavyo vimepangwa kukarabatiwa na kuendelezwa na kiwanja hicho kimetengewa shilingi bilioni 2.95 na Serikali katika mwaka wa fedha wa 2018/2019 za kuwezesha kuanza kwa ukarabati huo .

Vile vile, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa gati ya bandari ya Nyamisati iliyopo Kibiti mkoani Lindi inayowawezesha wananchi kusafiri kwenda Mafia ambapo ujenzi huo ni pamoja na majengo ya ofisi, sehemu ya kupumzika abiria na vyoo na kubaini kuwa ujenzi huo unaendelea vizuri ambapo unagharimu shilingi bilioni 14.4 ambao ni wa kipindi cha mwaka mmoja ambao ulionza mwezi Machi 2018 na unatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2019. 


Meneja Mradi huo wa TPA, Mhandisi Erick Madinda amemueleza Nditiye kuwa mradi wa ujenzi huo unagharamiwa na TPA na tayari mkandarasi Alpha Logisitics Tanzania Ltd & Southern Engineering Company Ltd ameshalipwa shilingi bilioni 2.4 kati ya shilingi bilioni 14.4 ambazo ni gharama za ujenzi atakazotakiwa kulipwa mara kazi itakapokamilika.
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati) akitoa maelekezo kwa Mhandisi Ujenzi wa Bandari ya Mtwara, Twaha Msita (hayupo pichani) kuhusu kutoridhishwa na ujenzi wa gati ya bandari ya Lindi wakati wa ziara yake ya kukagua bandari hiyo mkoani humo. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga.

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (aliyevaa fulana ya bluu) akikagua ujenzi wa gati ya bandari ya Lindi unaosuasua wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi huo mkoani Lindi. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Lindi Shaibu Ndemanga

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa pili kulia) akipata maelezo ya maendeleo ya ujenzi wa gati ya bandari ya Nyamisati wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi huo Kibiti, Lindi. Meneja Mradi wa TPA Mhandisi Erick Madinda akitoa maelezo

No comments: