ZAIDI ya washiriki 5000 kutoka mikoa ya Morogoro,Dodoma,Dar es Salaam ,Iringa na Zanzibar wanataraji kushiriki mbio mpya za Marathoni zijulikanazo kama “Morogoro Marathon 2018” zitakazofanyika katika mji wa Morogoro kwa mara ya kwanza Desemba 2 mwaka huu.
Miongoni mwa washiriki hao wamo pia wanariadha wanaoshiriki mashindano ya Kimataifa wa Tanzania na nchi jirani za Kenya ,Ethiopia na Sudani ya Kusini watakaochuana kuweka rekodi mpya katika riadha kutokana na hali ya hewa ya mji wa Morogoro.
Meneja Uhusiano na Masoko wa taasisi ya uwakala wa Michezo ya Itete “ITETE SPORTS AGENCY” ambao ndio waandaaji wa Mbio hizo ,Dixon Busagaga alisema tukio hilo litakuwa tukio la kwanza kubwa kuwahi kufanyika katika mkoa wa Morogoro na kukutanisha idadi kubwa ya washiriki.
“Kutokana na jiografia ya mkoa wa Morogoro kuwa lango la mikoa ya mikoa ya kusini na kupakana kwa ukaribu na baadhi ya mikoa ya nyanda za kati na Pwani ni wazi matazamio yetu litakuwa tukio kubwa kwa mkoa wa Morogoro”alisema Busagaga.“Tukio hili limebeba maudhui matatu makubwa ambayo ni ,uhamasishaji wa masula ya utunzaji wa Mazingira ,uhamasishaji katika masuala ya Afya pamoja na kutangaza vivutio vya utalii hasa vilivyopo kusini mwa nchi yetu . “alisema Busagaga .
Busagaga alisema hadi sasa vilabu zaidi ya 50 vya mazoezi “Jogging Clubs” kutoka mikoa ya Dar es Salaam ,Dodoma na Morogoro vimewasilisha maombi ya kushiriki katika tukio hilo pamoja na Vilabu zaidi ya 20 vya timu za mpira wa miguu za wachezaji wa zamani yaani Veterani.
“Tukio hili tunataka kulifanya la pekee,tutakuwa na siku mbili za tukio,siku moja kabla ya tukio kubwa la mbio,tutakuwa na shughuli za kuotesha miti zaidi ya 10,000 katika maeneo mbalimbali ya mji wa Morogoro”alisema Busagaga.
“Baada ya tukio hilo ,Timu za Veterani zitakazokuwa zimewasili na kujisalijili kwa ajili ya ushiriki wa Marathoni hiyo tumeandaa mashindano yao kwa jioni ya Desemba mosi ,ambapo washindi wa Bonanza hilo watakabidhiwa zawadi zao na mgeni rasmi siku ya tukio la Marathon.”alisema Busagaga
“Timu za Veterani zitakazosajili mapema zitapata kipaumbele cha kuwekwa kwenye ratiba ya Bonanza hilo , washindi watatu watapata zawadi na wengine watapata vyeti vya ushiriki na michezo itafanyika katika uwanja wa Jamhuri na viwanja vingine vya Michezo katika mji wa Morogoro kama timu zitakua nyingi.”aliongeza Busagaga.
Kuhusu tukio lenyewe Busagaga alisema washiriki kutoka maeneo mbalimbali ya nchi na nje ya nchi watashiriki Mbio za Km 21 na zile za kujifurahisha za Km 5 ambazo washiriki wake watakuwa ni Wazee wenye umri mkubwa,kina mama, watoto, wenye ulemavu na watakao penda kushiriki mbio hizo.
Chama cha riadha mkoa wa Morogoro kupitia katibu Mkuu wake ,Kibukila Chamrungu kilisema kimefarijika kwa Mashindano ya Marathoni kufanyika kwa mara ya kwanza katika mkoa wa Morogoro na kwamba kwa sasa kupitia mbio hizo watapatikana wanariadha wa kimataifa kutoka Morogoro.
“Kama chama cha riadha mkoa tunafarijika sana ,mkoa wetu umekuwa ukipeleka wanariadha kwenye mashindano madogo madogo lakini sasa mwaka huu ,tunaenda kushiriki na kushindana na wanariadha wa kimataifa hii kwetu imetupa faraja kwa sababu sasa mkoa wetu utatamburika rasmi katika riadha.”alisema Chamrungu.
No comments:
Post a Comment