Friday, November 30, 2018

Washiriki Master Tanzania kutambulishwa Forty Forty Tabata leo

WASHIRIKI wa Shindano la Master Tanzania 2018/19, wanatarajiwa kutambulishwa leo Forty Forty Club, iliyopo Tabata Bima, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mratibu wa shindano hilo, Michael Maurus, alisema kuwa utambulisho huo ni sehemu ya maandalizi ya shoo ‘bab kubwa’ ya mchujo itakayofanyika wikiendi ya pili ya mwezi huu katika ukumbi utakaotangazwa.

Alisema kuwa jumla ya washiriki 30 watakuwapo Forty Forty leo ambapo watapata nafasi ya kujitambulisha mbele ya wadau wa sanaa ya uanamitindo na burudani kwa ujumla.“Tunaushukuru uongozi wa Forty Forty kwa kutupa nafasi hii, wadau wa burudani waje kwa wingi kuwaona vijana wanatashati watakaoshiriki shindano letu ambalo fainali zake zitafanyika Februari mwakani kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam,” alisema Maurus.

Maurus alisema kabla ya fainali za shindano hilo, kutakuwa na hatua ya robo na nusu fainali ambapo lengo lao ni kuwa na washiriki wa awali 50.

“Lengo letu ni kuwa na washiriki 50 na kesho (leo) ni siku ya mwisho kwa vijana wanaopenda kushiriki mashindano hayo kujiandikisha, baada ya hapo watalazimika kulipia fomu. Hivyo kwa wanaopenda kushiriki, waje pale Forty Forty kuanzia saa 2:00 usiku wachukue fomu, wazijaze na kuzirejesha hapo hapo,” alisisitiza Maurus.

Juu ya zawadi za shindano hilo, Maurus alisema hadi sasa wamna uhakika wa mwaliko wa washindi watano kwa kwanza kwenda Marekani kutembelea maeneo mbalimbali maarufu ya Hollywood, yakiwamo yale yaliyochezewa sinema zilizowahi kutamba, ikiwamo ya Coming To America iliyochezwa na wakali kadhaa, akiwamo Eddie Murphy.

Maurus alisema kuwa pia kutakuwa na zawadi nyinginezo za fedha, huku akisisitiza wameomba wenyeji wao mabosi wa Hollywood kuongeza idadi ya waalikwa ili waweze kupeleka huko washiriki 10 na waandishi wa habari watakaoripoti zaidi shindano lao.

Shindano la Master Tanzania lilizinduliwa kwa mara ya kwanza Machi mwaka huu, likiratibiwa na Kampuni ya Kiafrika Zaidi chini ya Rais wake, Mtanzania Winny Casey anayefanya shughuli zake Marekani ambaye pia ni Balozi wa Hollywood hapa nchini.
Baadhi ya washiriki Master Tanzania 201819

No comments: