Sunday, November 18, 2018

Makamba awataka wataalam elekezi mazingira kubadilika kiutendaji

WAZIRI wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),Bw.
January Makamba amewataka wataalamu elekezi wa tathmini ya athari kwa mazingira kubadilika kiutendaji ili tasnia hiyo iendelee kukua na
kutoa mchango stahiki katika maendeleo ya taifa. 

Akifungua Mkutano wa Pili wa Mwaka wa Chama cha Wataalamu Elekezi wa
Tathmini Athari kwa mazingira, ukaguzi na vibali vya awali jijijni
Dar es salaam mwishoni mwa wiki, Bw. Makamba alisema wataalamu elekezi wa mazingira wana umuhimu mkubwa katika ujenzi wa uchumi,lakini lazima wabadilike namna ya utendaji wao wa kazi.

‘’Katika changamoto za namna ya ufahamu na ufanywaji wa
tathimini na ukaguzi wa mazingira nyie kama chama mnauwezo wa
kujipanga kuanzisha programu za mafunzo na kubadilishana uzoefu (
Capacity Building) kwa kufanya hivo itasaidia kuboresha na kuimarisha
uwezo wenu wa kiutendaji,’’ alisema Waziri Makamba.

Waziri Makamba alisema suala la tathimini za athari kwa mazingira
linapewa kipaumbele ili kwenda sambamba na azma ya Serikali ya Awamu
ya Tano ya kujenga Uchumi wa Kati na Viwanda ifikapo mwaka 2025.
“Kuna changamoto kadhaa kwenye usajiri wa wataalam elekezi wa
mazingira kuhusu ulipwaji wa ada za mwaka ambapo serikali inapoteza
mapato yake. Taarifa ya NEMC inaonyesha kuwa mwaka 2018 wataalam
binafsi wanadaiwa jumla ya shilingi milioni 600, na makampuni
yanadaiwa jumla ya milioni 250 kama ada za mwaka,” alisema.

Bw. Makamba alisema serikali inawatambua wataalam na kazi zao kwa wale
wasiolipa ada za mwaka katika tasnia hii walipe mara moja kabla hatua
kali za kisheria hazijachukuliwa.Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa Usimamizi wa Mazingira (NEMC),Bw.Vedast Makota alisema kama Baraza limejipanga kufanya marekebisho kwenye kanuni ya tozo na ada pamoja na kanuni ya tathimini athari kwa mazingira .

Dkt. Makota alisema hadi kufikia mwezi wa nne mwaka huu, NEMC
ilifanikiwa kutoa kanuni mpya ya ada na tozo ya Baraza ambapo
kimsingi ilizingatia malalamiko ya wananchi ambao walikuwa wanatozwa
katika ada na tozo mbalimbali.‘’Hapo awali miradi ilikuwa inatozwa kwa asilimia ya gharama ya uwekezaji lakini kwa sasa tumeliondoa na kuweka viwango ambavyo vitakuwa rafiki kwa wawekezaji ’’ alisema Dkt. Makota.

Alisema kwa sasa miradi midogo inatozwa kuanzia milioni mbili
tofauti na hapo awali ilikuwa inatozwa kuanzia milioni Kumi ambapo
miradi ya serikali inatozwa milioni 50 kulingana na gharama za
uwekezaji wa mradi lakini ilikuwa milioni 500 hadi milioni 600.

Dkt. Makota alisema Kanuni mpya walizozitoa Septemba mwaka huu kwa
upande wa sekta ya viwanda, mwekezaji anaruhusiwa kuomba kibali hata
kama hajakamilisha matakwa ya msingi kwenye andiko la awali ambapo
masharti yanamtaka kuwa ndani ya miezi 4 awe amepata cheti.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wataalam eEekezi wa Mazingira
Tanzania, Prof. Hussein Sosovele alisema kama Chama kimejipanga
kufanikisha azma ya serikali ya awamu ya Tano ya ya kufikia uchumi
wa kati na viwanda ifikapo 2025 kwa kufanya uchambuzi yakinifu juu
ya tathmini ya uwekezaji na kuainisha namna uwekezaji huo utakavyo
leta tija bila kuaribu mazingira.

“Chama kitaishauri serikali juu ya namna bora ya kutumia rasilimali
bila kuharibu mazingira kwa kiasi ambacho hakitaweza kurekebishika,’’
alisema Prof. Sosovele.

Kwa upande wake Mtaalam wa Mzingira Bw. Peter Luena alisema
Mkutano huo una manufaa makubwa kwao na kuamini kuwa serikali
itayafanyia kazi mapendekezo yao waliyoyatoa na watanzania
wategemee mambo makubwa katika usimamizi na utunzaji wa mazingira.

No comments: