Wednesday, November 21, 2018

KAMPUNI SABA KUTOKA NCHINI UTURUKI WAONESHA NIA KUWEKEZA NCHINI,TIC,BALOZI KIONDO WATOA NENO

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

KAMPUNI saba kutoka nchini Uturuki zimekuja nchini Tanzania na kuonesha nia ya kuwekeza katika ujenzi wa maduka makubwa ya nguo, uwekezaji katika sekta ya nishat ya umeme, hoteli zenye hadhi ya nyota tano katika Jiji la Dodoma na uuzaji wa bidhaa.

Ujio wa kampuni hizo ni muendelezo wa jitihada zinazofanywa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania(TIC) kwa kushirikiana na wadau katika kuhakikisha wanaendelea kuhamasisha nchi mbalimbali kuja kuwekeza nchini.

Akizungumzia ujio wa Kampuni hizo kutoka nchini Uturuki,Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Elizabert Kiondo amesema nchi yetu kwa sasa ipo kimkakati katika kuelekea uchumi wa viwanda na hivyo ujio wa kampuni hizo ambazo zitawekeza n chini zitasaidia kuongeza juhudi kwa vitendo.

Amesema nchi ya Uturuki inatambua hali tulivu ya n chini Tanzania katika masuala ya uwekezaji na hivyo moja ya jukumu ambalo amelifanya ni kuhamasisha kampuni mbalimbali za nchi hiyo zinakuja kuwekeza kwa maslahi ya Watanzania wote."Nchi yetu ipo kwenye mkakati madhubuti wa kuhakikisha tunaimarisha uchumi wetu kupitia viwanda na uwekezaji.Wenzetu wa Uturuki wameelewa tunakoelekea na hivyo sasa wamekubali kuja nchini kuwekeza.

" Hizi kampuni saba ambazo nimekuja nazo zimeonesha nia ya kuwekeza kwenye maduka makubwa ya nguo, kujenga hoteli zenye hadhi ya nyota tano,kushiriki kwenye sekta ya umeme na kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na kilimo,"amesema Balozi Kiondo.

Amefafanua kuwa kampuni hizo zimeonesha kuamini Tanzania kuna soko la uhakika na kubwa zaidi baada ya kuanza shughuli zao hakutakuwa na sababu ya msingi kusafiri kwenda katika nchi hiyo kupata bidhaa kwani zitapatikana hapa hapa nchini Tanzania.Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uhamasishaji Uwekezaji kutoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC)John Mnali amesisitiza kampuni hizo saba kuonesha nia ya kuwekeza nchini katika nyanja mbalimbali.

Ametumia nafasi hiyo kutoa rai kwa taasisi nyingine na mamlaka za ngazi mbalimbali kutoa msaada ambao utasaidia kampuni hizo kufikia malengo yao ya kuja kuwekeza nchini."Tuhakikishe tunashirikiana katika kuwasaidia mambo muhimu wanayohitaji ili watimize azma ya nia yao njema kwetu,"amesema Mnali.

Wakati huo huo Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Ali Dovutoglo amesema hali ya uwekezaji nchini ni nzuri na kuna utashi mkubwa wa kisiasa wa kuhimiza uwekezaji na hivyo nchi yao imeona hana ya kuunga mkono kwa vitendo ikiwa pamoja na ujio wa kampuni hizo.

Akizungumzia ujio wa kampuni hizo, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ulaya na Amerika kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani Jestas Nyamanga amesema uhusiano katika nchi hizo mbili upo imara na matokeo yake ni kuona Raia wa Uturuki wanaamua kuja kuwekeza nchini.Amesema Rais Dk.John Magufuli mwaka 2016 aliamua kufungua Balozi ya Tanzania nchini Uturuki na baada ya hatua hiyo kumekuwa na muamko mkubwa wa kimahusiano ambayo yameanza kuzaa matunda.

"Ubalozi wa Tanzania nchini Uturuki ilianza baada ya Rais tu kuingia madarakani na ilipofika mwaka 2016 akaanzisha Balozi hiyo ambayo hakika imefungua milango na fursa kwa pande zote mbili," amesema.

Mkuu wa msafara wa kampuni hizo kutoka nchini Uturuki Cengiz Ertas amesema uwezo wa kila kampuni ambazo wamekuja nazo uwezo wake ni dola za Marekani Milioni 100 na kwamba Februari mwaka 2019 watakuja na kampuni nyingine ambazo nia yao ni kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda vya saruji

No comments: