Wednesday, November 14, 2018

KAMATI YA BARAZA LA WAWAKILISHI INAYOSIMAMIA OFISI ZA VIONGOZI WAKUU ZANZIBAR YAVUTIWA NA MAFANIKIO YA TASAF.

NA Estom Sanga- TASAF. 

Wajumbe wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi inayosimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar wamepongeza hatua ya Serikali ya Muungano na ile ya Mapinduzi kwa usimamizi thabiti wa utekelezaji wa shughuli za Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF. 

Wakizungumza jijini Dar es salaam baada ya kupokea taarifa ya Utekelezaji wa Shughuli za TASAF mwanzoni mwa ziara ya siku NNE ya kutembelea miradi ya Mfuko huo, Wajumbe hao wameeleza kuridhishwa kwao na namna Mfuko huo ulivyoleta hamasa ya wananchi kujinasua na tatizo la umaskini uliokithiri. 

Wamebainisha kuwa miradi iliyotekelezwa na TASAF nchini inaonyesha taswira nzuri ya uwajibikaji na utekelezaji wa maagizo ya serikali yenye lengo la kuboresha maisha ya wananchi na kuondoa kero ya umaskini. 

Wametolea mfano wa miradi ya Shule ,Afya,Maji na hata uanzishaji wa miradi ya midogo midogo ya kiuchumi kwa wananchi kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini kuwa kichocheo kikubwa cha ukuaji wa shughuli za kujiongezea kipato . 

Aidha Wajumbe hao wameiomba serikali kupitia TASAF kuhakikisha kuwa inatoa fursa nyingine ya Wananchi wanaokabiliwa na umaskini ambao hawakupata fursa ya kuandikishwa kwenye shughuli za Mpango huo unaohudumia takribani Kaya Milioni MOJA na Laki Moja Tanzania Bara ,Unguja na Pemba. 

Awali akiwakaribisha Wajumbe hao Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii –TASAF,Bwana Ladislaus Mwamanga amesema maandalizi ya awamu ya pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambayo italenga zaidi katika kuwashirikisha Walengwa kufanya kazi katika kutekeleza miradi ya maendeleo yako katika hatua za mwisho na inatarajiwa kuanza mwezi Aprili mwaka ujao. 

Amezishukuru Serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar na wadau wa Maendeleo kwa kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa Shughuli za TASAF jambo ambalo amesema limewezesha kupatikana kwa mafanikio huku akipongeza hatua ya Walengwa kuanza kutumia huduma za TASAF katika kuleta mabadiliko kwenye maisha yao. 

Akitoa taafa ya utekelezaji wa shughuli za TASAF, Mkurugenzi wa miradi wa TASAF,Amadeus Kamagenge amesema kwa kiwango kikubwa Mfuko huo umetekeleza miradi yake kwa ufanisi mkubwa na hivyo kutekeleza azma ya serikali ya kuwaondoa wananchi kwenye dimbwi la umaskini.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF ,Bw. Ladislaus Mwamanga (aliyesimama) akizungumza kwenye kikao cha Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa Zanzibar wa liotembelea taasisi hiyo kuona utekelezaji wa shughuli zake.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia Ofisi za watendaji wakuu wa kitaifa katika baraza la wawakilishi Mhe. Ali Suleimani Ali akizungumza kwenye kikao na Watendaji wa TASAF baada ya kupokea taarifa ya miradi ya TASAF.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais –Zanzibar Mhe. Mihayo Juma N’hunga akizungumza wakati wa kikao cha pamoja katika wajumbe na menejimenti ya TASAF juu ya utekelezaji wa shughuli za mfuko huo.
Mkurugenzi wa Miradi wa TASAF ,Bw. Amadeus Kamagenge(aliyesimama ) akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za TASAF kwa wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa kitaifa Zanzibar.
Mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa kitaifa akichangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za TASAF kwenye kikao kilichofanyika kwenye ofisi za TASAF jijini Dar es salaam.
Wajumbe wa Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi wakuu wa kitaifa wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa TASAF baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya taasisi hiyo jijini Dar es sdalaam.

No comments: