Friday, November 16, 2018

JWTZ WAANZA UTEKELEZAJI WA AGIZO LA RAIS WILAYA YA NEWALA MKOANI MTWARA

Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii Newala, Mtwara

Mkuu wa Wilaya ya Newala Aziza Mangosongo leo amepokea ujumbe wa Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ )ambao umeanza kukagua Maghala yote ya kuhifazia korosho katika Wilaya hiyo kama ilivyoagizawa na Rais John Pombe Magufuli kufuatia Wafanyabiashara kutaka kuwalangua wakulima kwa kununua kwa bei isiyokuwa na Maslahi.

Ujumbe huo ambao ulipata nafasi ya kutembelea Maghala yote Makubwa ambayo yapo katika Wilaya yake hili waweze kuanza zoezi la kununua korosho kwa kuwalipa wananchi kupitia benki ya kilimo.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Newala mkoani Mtwara, Daniel Zenda amesema sababu kubwa ya kupungua kwa uzalishaji wa zao la korosho msimu huu ni kutokana na mvua iliyonyesha katikati ya msimu na kusababisha dawa ya Sulpher kushindwa kufanya kazi vizuri.

Akitoa muhtasari kwa vyombo vya habari jana mjini Newala juu ya shughuli zilizofanyika hadi sasa tangu serikali kutoa mwongozo wa ununuzi wa korosho, Zenda alisema propaganda zinaoenezwa kuwa upungufu wa uzalishaji umetokana na wakulima kutokupewa fedha za ushuru wa kusafirisha nje ( export levy) hazina ukweli wowote.

"Upungufu wa uzalishaji wa korosho haujasababishwa na kukosekana kwa fedha za export levy kama inavyoelezwa na baadhi ya wanasiasa badala yake mavuno yamepungua kwasababu mvua zilinyesha katikati ya msimu na kusababisha athari kwa dawa ya sulpher kushindwa kufanya kazi vizuri kwenye mazingira hayo," alisema Zenda.

Kwa mujibu wa Afisa masoko wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Tandaimba na Newala (TANECU), Juma Seleman, wanatarajia kupata tani 120,000 kwa msimu huu wa mwaka 2018/19 na kwamba zoezi la kukusanya kwenye maghala makuu kutoka vyama vya msingi linaendelea.

Alisema hadi sasa korosho iliyoingia kwenye maghala makuu ni tani 38,000 na bado zinaendelea kukusanywa kutoka vyama vya msingi na uvunaji unaendelea mashambani.Akizungumzia uamuzi wa serikali kununua korosho yote, Seleman alisema kama TANECU wanaunga mkono uamuzi wa serikali kupeleka fedha moja kwa mija kwa wakuoima bila kukatwa na kwamba wao wanaangalia kwanza maslahi ya wakulima hao kwani ndiyo kazi yao.

"Tayari utaratibu wa malipo umeshaanza kufanyika na pia utaratibu wa kuwatambua na kuwahakiki wakulima umeanza na tukimaliza haya tunaanza kuwalipa wakulima moja kwa moja kwenye akaunti zao," alisema Selema.

Alisema katika uhakiki wa wakulima wanashirikiana na vyama vya msingi vya ushirika wa wakulima ambapo taarifa zitapelekwa na kisha kila mkilima atakwenda kuhakiki kama taarifa zake ni sawa na baada ya hapo malipo yatafanyika.

Katika hatua nyingine Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) limeanza Operesheni Korosho kwa ukaguzi wa maghala na viwanda vya Korosho vilivyopo Newala likiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya hiyo, Aziza Mangosongo.Akizungumzia operesheni hiyo Zenda ambaye pia alikuwa kwenye msafara huo, alisema kikosi cha JWTZ kimetembelea maghala matatu na kiwanda kimoja kujionea shughuli zinazoendelea.

"Lengo kubwa la operesheni hii kwanza ni kuhakikisha korosho iliyopo kwenye maghala haitoki na hakuna korosho inayoingizwa kutoka nje ya nchi na kisha baadae wataanza kuzibeba na kuzipeleka kwenye kiwanda cha kubangua," alisema Zenda.Maghala yaliyotembelewa na timu hiyo ni pamoja na maghala mawili yanayomilikiwa na TANECU, ghala la Micronix System Limited lenye uwezo wa kuhifadhi tani 13,000 na ghala la Agrofocus ambayo yanamilikiwa na watu binafsi.

Aidha katika operesheni hiyo Zenda alisema DC Aziza kwa kushirikiana na kamati ya ulinzi juzi Novemba 13 walifanikiwa kukamata zaidi ya tani tisa za shehena ya korosho iliyokuwa imeingizwa nchini kutokea Msumbiji.Alisema hali hiyo inatokana na uamuzi wa serikali kununua korosho kwa bei nzuri hivyo wafanyabiashara wasio na nia njema kutumia hiyk kama fursa ya kuingiza korosho za magendo kutafuta soko Tanzania.

"Mkuu wa Wilaya ya Newala na timu yake jana (juzi) walifanikiwa kukamata magunia 91 yenye uzito wa zaidi ya kilo 100 pamina na trekta moja lioilokuwa limebeba shehena hiyo na raia mmoja mtanzania ambaye ndiye mmiliki wa mzigo huo alikamatwa na yupo chini ya ulinzi," alisema.Alisema mara nyingi korosho huvushwa kwa mitumbi kutoka Msumbiji na kisha kupakiwa kwenye magari kuingia Tanzania kwa kuvuka mipaka isiyo rasmi.

Alisema waligundua mzigo huo iliingia kupitia mpaka wa Newala na Msimbiji na kisha kupelekwa kwenye Chama cha Msingi cha Masasi ambapo ulikuwa unapimwa ili uingie kwenye maghala yetu.

Katika hatua nyingine wakulima wilayani Newala wamempongeza Rais Dk. John Magufuli kwa uamuzi wake wa kutouza korosho kwa wafanyabiashara na badala yake serikali kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kununua kwa Sh. 3,300.

Masoud Mbelenje mkazi wa kijiji cha Moneka Kata ya Mtonya ambaye pia ni Diwani wa kata hiyo alisema wanafurahia uamuzi wa Rais Magufuli kwani amewaondolea tatizo la kila mara la kotokuwa na soko la uhakika licha ya kutumia gharama kubwa katika kilimo hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Newala AkiongozaUjumbe wa Kikosi cha Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) Ambao wamefika Wilayani hapo kwa ajili ya kukagua Maghal ya Korosho hili waanze zoezi la ununuzi na kulipa fedha kwa wakulima kama ilivyoagizwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr . John Magufuli kuwa Korosho zote zitanunuliwa na jeshi .
Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wakiwa ndani ya Ghala la Kiwanda cha Ubanguaji wa korosho Microfonix kilichopo Wilaya ya Newala Mkoani Mtwara
Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wakiwa ndani ya Ghala la Agro focus kilichopo Wilaya ya Newala Mkoani Mtwara
Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wakiwa ndani ya Kiwanda cha Ubanguaji wa korosho Microfonix kilichopo Wilaya ya Newala Mkoani Mtwara na kushuhudia zoezi la usafishaji wa korosho.

Wafanyakazi wa Kiwanda cha Ubanguaji wa Korosho cha Microfonix wakiendelea na kazi ya ubanguaji wa korosho na kusafisha katika Kiwanda hicho

No comments: