Friday, November 23, 2018

DKT. NDUGULILE AZIDI KUZISISITIZA NGOs KUZINGATIA VIPAUMBELE VYA TAIFA

  Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amezidi kuyasisitiza Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kuzingatia vipaumbele vilivyowekwa na Serikali
katika kutekeleza miradi ya Maendeleo nchini.

Ameyasema hayo mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya siku tatu kutembelea na kukagua shughuli mbalimbali katika sekta ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.  Dkt. Ndugulile amesema kuwa nia ya Serikali sio kuyabana Mashirika hayo ila kuyaratibu ili yaweze kufanya kazi katika mazingira mazuri ambayo yatawezesha kuwa na mgawanyiko mzuri wa rasilimali katika maeneo mbalimbali nchini.

Naibu Waziri Dkt. Ndugulile ameutaka uongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kuweka vipaumbele na kuzielekeza NGOs sehemu za kwenda na sio kuziweka NGOs nyingi mahala pamoja.  Dkt. Ndugulile pia amezitaka NGOs kufanya kazi katika misingi ya uwajibikaji na kufuata Sheria na taratibu za nchi ili kuendeleza ushirikiano kati yao na Serikali katika kuchangia juhudi za wananchi kupata Maendeleo jumuishi.  “Unakuta sehemu moja zimerundikana NGOs nyingi na mkoa huo huo maeneo mengine hakuna NGOs hata moja” alisisitiza Dkt. Ndugulile.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mgwira amesema Mkoa wake unapambana na changamoto mbalimbali katika Sekta ya Afya na Maendeleo ya Jamii na kuiomba Wizara kushirikiana nao ili kutatua changamoto zinazoukabili mkoa wake.  “Nikushukuru Mhe. Naibu Waziri kwa kutukumbuka kuja kututembelea ila naomba mtuangalie kwa jicho la tatu katika kutatua changamoto zetu hapa mkoani” Alisisitiza Mhe. Anna.

Naye Mganga Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Best Magoma amesema huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii zinazingatiwa na kuangaliwa kwa ukaribu ili kuendelea kumuwezesha mwananchi kufaidika na huduma hizo.  Msisitizo huu kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kufuata vipaumbele
vya taifa umekuja baada ya Serikali kuyataka Mashirika hayo kufanya kazi kwa kuzingatia uwazi na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya Maendeleo nchini.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Faustine Ndugulile yupo mkoani Kilimanjaro kwa ziara ya siku tatu kufuatilia utekelezaji wa sera na programu katika Sekta ya Afya na
Maendeleo ya Jamii.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (katikati) akizungumza na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Anna Mgwira (kulia) katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huyo kuhusu kuwaelekeza wadau wa NGO kupanga utekelezaji wa miradi yao kwa kufuata vipaumbele na kuwapangia sehemu sahihi wadau hao kufanya kazi katika maeneo ya pembezoni ili kuleta usawa katika mgawanyo wa rasilimali kushoto ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhandisi Aisha Amour. 
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akimsikiliza Mzee wa miaka 98aliyejulikana kwa jina la Daniel Mzava alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi. 
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile  kimjjulia hali mmoja wa Mtoto aliyekuwa akipata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kilimanjaro Mawenzi wakati wa ziara yake Hospitalini hapo.  Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW 

No comments: