Saturday, November 10, 2018

CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM) CHAENDELEA KUKEMEA UMIMI, UBINAFSI NA MAKUNDI NDANI YA CCM ILI KUIMARISHA UIMARA, UMOJA NA UMADHUBUTI WA CCM

Katika kikao cha Halmashauri Kuu Maalumu ya CCM Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinakemea vikali umimi, ubinafsi na makundi ndani ya CCM ili kuimarisha uimara, umoja na umadhubuti wa CCM.

Akieleza kwa kina suala hilo Ndg. Polepole amesema umimi, ubinafsi na makundi ni kinyume na Katiba, Kanuni na Taratibu nzuri za CCM na kuwa ndani ya CCM Makundi hayana nafasi hususani katika kipindi hiki ambacho muelekeo wa CCM ni kushughulika na utatuzi wa shida za wananchi.

Aidha Ndg. Polepole amewataka wanaCCM na Viongozi kuwa wamoja, kushikamana, kushirikiana na kupendana ili CCM izidi kuwa imara na iendelee kuwa hudumia wananchi ipasavyo.

“Chama hiki nikikubwa kuliko mtu mmoja, hatuwezi tukaruhusu tabia za hovyo ambazo tumezikataza, tabia za makundi, hata Ndg. Magufuli Mwenyekiti wetu mpendwa hapendi makundi kwa sababu makundi hayatujengi na yanadhoofisha umoja wa  Chama chetu” amesema Ndg. Polepole

Wakati uo huo Ndg. Polepole amewapongeza sana Viongozi wote wa CCM kwa kufanikisha kupatikana kwa ushindi wa CCM Wilaya ya Serengeti ambapo CCM imepita bila kupigwa kwenye nafasi ya Ubunge  na udiwani na kuwa na nafasi nzuri zaidi ya kuongoza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti.

Awali Ndg. Polepole akiambatana na Viongozi wa CCM Wilaya na Mkoa wakiongozwa na Ndg. Samweli Niboye (Namba tatu) Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara wamekagua eneo la ujenzi wa chujio la Maji Mugumu katika Bwawa la Manchira  ambapo Ndg. Polepole pamoja na Viongozi wa CCM wamesikitishwa sana na namna ambavyo mradi huo unavyosuasua licha ya kuwa Serikali ya CCM imekwisha weka fedha ya kutosha kwenye mradi huo.

"Ndg. Magufuli Mwenyekiti wetu wa CCM alipofika hapa Mkoa wa Mara na Wilaya ya Serengeti maelekezo yake yalikuwa mradi huu ukamilike mara moja ili wananchi wapate maji safi na salama,  tumesikitishwa na kusuasua kwa mradi huu,   tunaitaka Wizara ya maji ije hapa Serengeti, ifuatilie na itoe majibu kuhusu mradi huu na ni lini maji safi na salama yatapatikana". amesisitiza Ndg. Polepole

Huu ni muendelezo wa kazi za Chama ndani ya Chama, kazi za Chama nje ya Chama ndani ya Jamii katika uimarishaji wa CCM, na kuuhisha dhana ya Chama imara hujenga Serikali imara.

Imetolewa na,
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI (CCM)
  Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Ndg. Humphrey Polepole akizungumza jambo kwenye kikao cha Halmashauri Kuu Maalumu ya CCM Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara ,ambapo alieleza kuwa  Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinakemea vikali umimi, ubinafsi na makundi ndani ya CCM ili kuimarisha uimara, umoja na umadhubuti wa CCM.
 Ndg. Polepole akiambatana na Viongozi wa CCM Wilaya na Mkoa wakiongozwa na Ndg. Samweli Niboye (Namba tatu) Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara walikagua  eneo la ujenzi wa chujio la Maji Mugumu katika Bwawa la Manchira  ambapo Ndg. Polepole pamoja na Viongozi wa CCM wamesikitishwa sana na namna ambavyo mradi huo unavyosuasua licha ya kuwa Serikali ya CCM imekwisha weka fedha ya kutosha kwenye mradi huo.

No comments: