Thursday, November 1, 2018

CCM NYAMAGANA YAWATIMUA MAKATIBU WAWILI KWA UDHALILISHAJI

NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nyamagana kimewavua uongozi Makatibu wa Siasa na Uenezi wa kata za Buhongwa na Mkolani wilayani humo kwa tuhuma na makosa ya kukidhalilisha na kukichafua kwenye jamii.
Pia kimelaani matukio hayo yaliyofanywa na viongozi hao wasio na hofu ya Mungu,katiba na sheria za nchi ambao wanakiangusha CCM kwa kufanya vitendo viovu na mambo ya ovyo yanayodhalilisha.

Akitoa tamko la kuwavua nyadhifa za uongozi makatibu hao wa Uenezi kwenye mkutano wa dharura wa Kamati ya Siasa ya Wilaya mbele ya vyombo vya habari Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana Salum Kalli alisema viongozi wa namna hiyo hawatavulimiwa kwa sababu wanafedhehesha chama.

“CCM inalaani vikali mambo yaliyofanywa na viongozi hao kwenye jamii na hatua hii itakuwa fundisho kwa viongozi wenye tabia kama hizo,maana si utamaduni na maadili ya CCM kwani inawataka wawe waadilifu na waaminifu kwenye nafasi zao.Hivyo tutafuatilia tabia, mienendo na maadili ya kila kiongozi wa CCM aliyepo madarakani,”alisema.

Kalli alieleza kuwa Kamati ya Siasa ya Wilaya imechukua hatua hiyo na kutoa tamko hilo Watanzania wajue ili viongozi wenye tabia chafu zisizofaa kwenye jamii waache kwa kuwa CCM haitawavumilia.

Alifafanua kuwa Katibu wa Siasa na Uenezi wa Kata ya Buhongwa Hassani Bushagama, anadaiwa kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha tatu wa shule moja ambayo haikutajwa ambapo alitoroka na kutokomea tangu Julai mwaka huu.

Kallia alisema Katibu wa Siasa na Uenezi wa Kata ya Mkolani Zephelin Maiko Shibugulu naye amekumbwa na panga hilo akidaiwa kukutwa akimlawiti kijana wa kiume mwenye umri kati ya miaka 16 na 19 , Oktoba 26 mwaka huu saa 11:00 jioni baada ya kumnunulia supu ya nyama sahani tatu kabla ya kumfanyia kitendo hicho, kinyume na katiba ya CCM toleo la 2017 na kanuni za uongozi na maadili.

Hata hivyo mtuhumiwa pamoja na kijana huyo walichoropoka na kukimbia na haijulikani walipo na kutokana na kitendo hicho Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ilimvua Bushagama uongozi Oktoba 23, mwaka huu na kutangaza nafasi hiyo ijazwe na kiongozi mwenye sifa Novemba 3, mwaka huu, huku halmashauri hiyo ikimvua Shibugulu wadhifa huo Oktoba 29.

Awali akifungua kikao kazi cha kamati ya siasa ya wilaya kabla ya tamko hilo, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana Zebedayo Athuman alisema wamehangaika kukitoa chama kwenye hali mbaya lakini viongozi hao na wengine wenye tabia hizo wanachafua taswira na sura ya chama hicho.

Alidai kuwa viongozi wa aina hiyo ni zao la mchujo rahisi wakati wa kutafuta na kupata viongozi, mchujo ambao umesababisha CCM ipate viongozi wa ajabu wasio na nidhamu, wanaokiuka maadili na kufanya mambo ya ovyo kwenye jamii wanakati wanapaswa kuwa kioo.

Zebedayo alisema kuwa wanataka kujenga nidhamu kati ya watendaji wa chama maana nidhamu haipo na wengine wanafanya mambo yasiyofurahisha na kuwataka viongozi kuwa makini wanaposhughulikia tuhuma, wafuate taratibu bila kuathiri vyombo vya dola.

“ Zipo tuhuma mbaya zinakifedhehesha chama na zikithibitika tutakuomba uturejeshee uanachama wetu.Pia tukifanya maamuzi kwa mihemko, kesho utakuta Zebedayo kasingiziwa ni muhimu taratibu zifuatwe na ili kuepuka kupata viongozi wanaoharibu sifa ya CCM, tutaomba juu watupe nafasi ya kuchuja watu tupate wenye maadili na uadilifu uliotukuka,”alisema.

Mwenyekiti huyo alisisitiza kuwa kitendo cha viongozi hao kuchafua sura ya CCM lazima wakae pembeni na akaonya wasifanye mzaha na mambo ya chama kwani cheo ni dhamana na lazima wajue hivyo.


Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana Salum Kallia akisoma tamko la kuwavua uongozi makatibu wa Siasa na Uenezi wa kata za Buhongwa na Mkolani, Hassani Bushagama na Zephelin Maiko Shibugulu, mbele ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu wilayani Nyamagana jana.
Katibu wa CCM Wilaya ya Nyamagana Salum Kallia akisoma tamko la kuwavua uongozi makatibu wa Siasa na Uenezi wa kata za Buhongwa na Mkolani, Hassani Bushagama na Zephelin Maiko Shibugulu, mbele ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu wilayani Nyamagana jana.waliokaa mbele kutoka kushoto ni Mwenyekiti wa Zebedayo Athuman, Meya wa Jiji la Mwanza James Bwire na wa kwanza kulia ni Katibu wa Siasa na Uenezi Musptapha Banigwa
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Zebedayo Athuman akifungua kikao kazi cha kamati ya siasa ya wilaya hiyo jana, kushoto ni Katibu wa Chama wilayani humo Salum Kalli na kutoka kulia wa kwanza ni Katibu wa Siasa na Uenezi Mustapha Banigwa na Meya wa Jiji la Mwanza James Bwire.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Nyamagana, Zebedayo Athuman akifungua kikao kazi cha kamati ya siasa ya wilaya hiyo jana, kushoto ni Katibu wa Chama wilayani humo Salum Kalli na kutoka kulia wa kwanza ni Katibu wa Siasa na Uenezi Mustapha Banigwa na Meya wa Jiji la Mwanza James Bwire. Picha na Baltazar Mashaka

No comments: