Wednesday, October 17, 2018

ZAWADI ZATAJWA KICHOCHEO CHA UKEKETAJI TARIME

NA BALTAZAR MASHAKA, TARIME

ZAWADI zimetajwa kuwa chanzo na kichocheo kikubwa cha vitendo vya ukeketaji na tohara kwa watoto wa kike na kiume wilayani Tarime katika Mkoa wa Mara.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya wanafunzi walioshiriki tamasha la kupinga Ukatili wa kijinsia lililoandaliwa na Shirika la ATFGM Masanga na kufanyika katika Shule ya Sekondari Kemambo kwa ufadhili wa Terre des Homes tamasha ambalo lilishirikisha shule 10 mbili za msingi na nane za msingi wilayani Tarime.

Wanafunzi hao walieleza kuwa kipindi cha ukeketaji mabinti (watoto wa kike) wanapotoka kukeketwa huzunguka kwenye jamii inayowazunguka ili kupatiwa zawadi ya fedha, nguo na vitu vingine jambo ambalo huwashawishi wengine ambao hawajakeketwa kwenda kufanyiwa vitendo hivyo vya ukatili ili nao wapatiwe zawadi.

Pia waliishauri serikali kusimamia Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na kanuni zake kupiga marufuku vishawishi vya zawadi za nguo na fedha ili kudhibiti uketetaji wa watoto wa kike na tohara isiyo salama kwa vijana wa kiume.

“Mtoto mmoja anaweza kupata nguo (vitenge) na fedha nyingi ambazo huzibana kwa pini kichwani hivyo wale ambao ni wadogo kama hawajakeketwa wakiona hizo zawadi wanatamani na kushawishika kukeketwa, hivyo serikali ipige vita zawadi hizo kwa kusimamia Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 na kanuni ” alisema ( Maria Marwa jina la linahifadhiwa) mwanafunzi huyo wa Shule Msingi Nyabusara.

Aidha, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kemambo Mussa Issack alisema kipindi cha tohara kwa wanaume, vijana hutembea umbali mrefu baada ya kutahiriwa huku baadhi yao wakitokwa damu nyingi na wengine kukimbizwa hospitalini jambo ambalo ni hatari kwa maisha yao.

“ Jambo hili ingawa linaonyesha ujasiri na ushujaa lakini ni hatari kimaisha hivyo suala tohara kwa vijana wa kiume niombe lifanyike kitaalamu ili kunusura watoto wasipoteze maisha kwa kutokwa na damu nyingi baada ya tohara.Pia sehemu inayotumika kutahiria na vifaa vyake si salama kwa afya yao,”alisema mwanafunzi huyo.

Akifunga tamasha hilo jana mgeni rasmi Mkuu wa Shule ya Sekondari Kemambo, Matinde Gimonge alisema elimu ya kupinga ukatili wa kijinsia inayotolewa kwa watoto hao tawanya waendelee kuwa mabalozi kwa kuelimisha jamii inayowazunguma ili kukomesha mila na tamaduni hizo potofu.

“Ni muhimu elimu hii inayotolewa kwa watoto ikawa chachu ya kuachana na vitendo vya ukatili na hivyo waendelee kuwa mabalozi ili kuifanya jamii salama isiyo na ukatili,”alisema Gimonge.

Kwa upande wake Mratibu wa Haki za Watoto wa Shirika la ATFGM Masanga Emmanuel Omenda alieleza kuwa matokeo hanya (faida) yaliyopatikana tangu kuundwa kwa klabu za kupinga ukatili kwa watoto wa shule za sekondari na msingi ni matukio mbalimbali ya ukatili kuripotiwa na kufanyiwa kazi pamoja na baadhi ya wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.

Aliongeza kuwa zaidi ya watoto 1,500 wa shule 40 kabla na baada ya kufanyika kwa tamasha hilo wamepatiwa elimu ya kupinga Ukatili wa Kijinsia, Ukeketaji, Ndoa na Mimba za utotoni na anaamini watakuwa mabalozi wazuri katika kufikisha elimu hiyo kwa jamii wilayani Tarime na maeneo mengine ya Mkoa wa Mara ili kutokomeza vitendo hivyo vya ukatili. 
 Mwanasheria wa Shirika la Kupinga Ukatili wa Kijinsia la ATFGM Masanga wilayani Tarime, Dora Luhimbo akitoa elimu ya kupinga masuala ya ukeketaji na ndoa za utotoni lililoandaliwa na shirika hilo na kukutanisha shule 10 za msingi na sekondari ambalo lilifanyika katika Shule ya Sekondari Kemambo wilayani humo. 
 Wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za kata za Matongo na Kemambo wakiwa katika tamasha la elimu ya kupinga Ukatili wa Kijinsia, Ukeketaji, Ndoa na Mimba za utotoni lililoandaliwa na shirika la ATFGM Masanga Tarime. 
 Mwanasheria wa Shirika la Kupinga Ukatili wa Kijinsia wilayani Tarime, Mara ( ATFGM Masanga) Dora Luhimbo akicheza muziki na baadhi ya wanafunzi katika tamasha hilo la kupinga ukatili wilayani humu.
Mgeni rasmi, Mkuu wa Shule ya Sekondari Kemambo Matinde Gimonge akifungua tamasha la kupinga Ukatili wa Kijinsia na kuwataka wanafunzi kuwa mabalozi wazuri wa kufikisha elimu kwa jamii, elimu ambayo wanaipata kupitia kwenye matamasha ya namna hiyo. 

No comments: