Monday, October 1, 2018

ZAIDI YA WATU 300 WAFANYIWA UPIMAJI WA MAGONJWA YA MOYO KIGAMBONI

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Smitha Bhalia akitoa maelekezo ya jinsi ya kutumia dawa kwa mkazi wa Kigamboni wakati wa maadhimisho ya siku ya Moyo Duniani ambapo Taasisi hiyo kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari wa Moyo Tanzania (THF) walifanya upimaji bila malipo katika viwanja vya Hospitali ya Vijibweni iliyopo wilaya ya Kigamboni. Katika upimaji huo makampuni mbalimbali ya dawa za binadamu yaligawa dawa bure kwa watu waliokutwa na matatizo yaliyohitaji kutumia dawa.


Na Genofeva Matemu – JKCI


1/10/2018 Zaidi ya watu 300 wamefanyiwa upimaji wa magonjwa ya moyo pamoja na kupewa elimu ya lishe bora kwa afya ya moyo katika maadhimisho ya siku ya moyo Duniani yaliyofanyika hivi karibuni katika viwanja vya Hospitali ya Vijibweni iliyopo wilaya ya Kigamboni.

Katika upimaji huo uliofanywa na madaktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari wa Moyo Tanzania (THF) jumla ya watu 169 wakiwemo watoto walipimwa kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO Cardiogram ECHO) na 135 ambao ni watu wazima walipima kipimo cha kuangalia jinsi umeme wa moyo unavyofanya kazi (Electrocardiography-ECG).


Akiongea na waandishi wa Habari leo jijini Dar es Salaam Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Samweli Rweyemamu alisema kwa upande wa watoto waliwaona 34 sita kati yao walikutwa na matatizo ya moyo na watu wazima 10 walikutwa na matatizo wote hao wamepewa rufaa ya moja kwa moja ya kwenda kutibiwa JKCI.

“Wananchi wengi tuliowaona na kuwafanyia vipimo wamekutwa na tatizo la shinikizo la juu la damu ambapo tumewapa dawa za kwenda kutumia pamoja na ushauri na wachache kati yao tumewapa dawa za ugonjwa wa kisukari”, alisema Dkt. Rweyemamu.

Wananchi hao walifanyiwa vipimo hivyo wakati Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Tanzania walipokuwa wakiadhimisha siku ya moyo duniani iliyofanyika hivi karibuni katika hospitali ya Vijibweni iliyopo Wilaya ya Kigamboni na kutoa dawa za moyo kwa asilimia 80 ya wananchi waliopimwa na wengine wachache kupewa dawa za kisukari

Akizungumza na wananchi wa Kigamboni waliohudhuria upimaji huo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndungulile aliwataka wananchi hao kutoishia kufanya upimaji kwenye siku za maadhimisho tu bali kujitokeza mara kwa mara kupima afya zao na kutunza mioyo yao kwa kula milo yenye lishe bora, kuwa na utamaduni wa kufanya mazoezi ya mara kwa mara, pamoja na kupunguza matumizi ya pombe na sigara.

“Wataalamu wa magonjwa ya afya tunaamini kwamba tiba sahihi za magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni kuyakinga; serikali imejipanga kuanzisha mpango wa taifa wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza ili tuweze kuzishusha huduma za magonjwa hayo hadi katika ngazi za kata katika vituo vyetu vya afya” alisema Mhe. Dkt. Ndungulile.

“Naipongeza sana Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kazi nzuri na kubwa wanayoifanya kwani imekua ikitumika kama shamba darasa kwa kutoa elimu kwa madaktari wengine waliopo mikoani lakini pia kutoa madaktari bingwa wa taasisi kwenda kwenye jamii kutoa huduma ya afya”, alisema Mhe. Dkt. Ndungulile

Siku ya moyo duniani huazimishwa Duniani kote kila mwaka tarehe 29 Septemba ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni , “kwa moyo wangu, kwa moyo wako, sote pamoja kwa mioyo yetu , tunatimiza ahadi”

No comments: