Sunday, October 14, 2018

WIZARA YA AFYA YAPOKEA MSAADA WA VIFAA VYA HOSPITALI KUTOKA SHIRIKA LA HHRD



Katibu Mkuu Shirika la HHRD la Marekani Ayoub Mohd akimkabidhi hati ya mkabidhiano ya vifaa vilivyotolewa na Shirika hilo katika hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja, Mjini Zanzibar.
Meneja Mkaazi wa Shirika la HHRD Ofisi ya Nairobi Musa Ibrahim akieleza kuridhishwa na watendaji wanpopkea misaada wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya Hospitali iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja.
Katibu Mkuu Shirika la HHRD Ayoub Mohd akizungumza baada ya kumkabidhi Waziri wa Afya msaada wa vifaa vilivyotolewa na Shirika hilo katika hafla iliyofanyika Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akitoa shukrani zake kwa Shirika la HHRD kwa msaada waliotoa kwa ajili ya wananchi wa Zanzibar.
Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed akimkabidhi mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wenye Ulemavu Zanzibar Haidar Hassan Madoea moja ya baskeli zilizotolewa msaada na Shirika la HHRD .Picha na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar

………………………..

Na Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar

Msaada wa Dawa na Vifaa Tiba unaotolewa na wafadhili mbali mbali unaweza kupunguza matumizi ya Serikali yaliyopangwa katika bajeti ya mwaka 2018/19 iwapo Wafanyakazi wa Wizara ya Afya watachukua juhudi ya kuilinda na kuitunza misaada hiyo.

Waziri wa Afya Hamad Rashid Mohamed alieleza hayo Ofisini kwake Mnazimmoja wakati wa hafla ya kupokea msaada wa vifaa tiba na vitendea kazi vya Hospitali kutoka Shirika linalotoa misaada ya Kijamii la Marekani la HHRD kupitia Jumuiya ya Muzdalifa ya Zanzibar.

Alisema Serikali inaendeleza mashirikiano na Mashirika na Taasisi za ndani na nje ya nchi ili kuona huduma za Afya zinaimarika na wananchi wanapata huduma bila usumbufu. Waziri Hamad alilipongeza Shirika la HHRD kwa msaada huo na kulishauri kuangalia uwezekano wa kusaidia zaidi katika maeneo ya mama na mtoto na kuwapatia mafunzo wafanyakazi wa Hospitali.

Alikumbusha kuwa pamoja na misaada inayotolewa na wafadhili, Serikali imeweka Bajeti ya kutosha kwa ajili ya dawa na amewataka wafanyakazi wanaosimamia uagiziaji wa dawa kuwa waangalifu kuepuka kununua dawa ambazo zipo kwa wingi katika Hospitali na vituo vya afya.

Amewashauri watendaji hao kuangalia maeneo ambayo yanaupungufu wa dawa na mahitaji yake ni makubwa na kuepuka kuingiza dawa ambazo matumizi yake ni madogo na hatimae kuharibika. Meneja Mkaazi wa Shirika la HHRD Ofisi ya Nairobi Musa Ibrahim alieleza kuridhishwa na uwajibikaji wa Serikali wanapoleta misaada kwa kusimamia na kuhakikisha inafika kwa waliokusudiwa.

Alisema kutokana na uaminifu na juhudi zinazochukuliwa na watendaji mbali mbali wanakusudia kuongeza misaada mengine yenye lengo la kupunguza matatizo katika jamii. Katibu Mkuu wa Muzdalifa Sheikh Farouk Hamad Khamis alisema Taasisis hiyo itaendelea kufanya juhudi ya kutafuta mashirika yenye nia ya kutoa misaada ya kibinadamu isiyokuwa na masharti ili kuwapatia wanaoihitaji.

Amewahakikisha wananchi kuwa msaada hasa wa dawa na chakula unaotolewa na Taasisi hiyo Uko salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu hivyo wasiwe na shaka kuitumia. Katibu Mkuu wa HHRD Ayoub Mohd alimkabidhi Waziri wa Afya msaada wa mafriji matano ya kuhifadhia damu, vigari vya walemavu 17, gloves boksi 20, mipira ya wazazi boksi 20 na vyakula vya lishe kwa ajili ya watoto vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya shilingi 33 milioni.

No comments: