Friday, October 12, 2018

Wenye Maeneo Makubwa ya Uwekezaji Watakiwa Kushirikiana na TIC.



Mkurugenzi na Mmiliki wa eneo la uwekezaji la Kilua lililopo Kijiji cha Disunyala Kata ya Kilangalanga Mlandizi Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani Bw.Mohammed Kilua (aliyesimama) akitoa maelezo kwa Kaimu Mkurugenzi wa huduma kwa wawekezaji wa TIC Bw.Ayoub Sizya (aliyekaa kushoto kwake), wengine ni baadhi ya walioonyesha nia ya kuwekeza viwanda kwenye eneo hilo lenye ekari 1,000.

Mkurugenzi na Mmiliki wa eneo la Kilua la ukanda wa uwekezaji wa viwanda lenye ekari elfu moja lililopo Kijiji cha Disunyala Kata ya Kilangalanga Mlandizi Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani Bw.Mohammed Kilua akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusiana na kulikabidhi eneo hilo kwa kituo cha Uwekezaji Tanzania TIC kwa ajili ya kuvutia wawekezaji,TIC imechukua eneo hilo na kuwataka wawekezaji kujitokeza kujenga viwanda. Picha na Jacline Amos-MAELEZO

Mmoja wa Wawekezaji Kampuni ya KAMAKA kwenye eneo la Uwekezaji la Kilua lililopo Kijiji cha Disunyala Kata ya Kilangalanga Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani Bw. Jurijs Matinovs (Kati kati)akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkurugenzi wa huduma kwa wawekezaji kutoka TIC Bw.Ayoub Sizya (aliyevaa suti na shati jeupe) kuhusiana na uwekezaji wanaotaka kuufanya wa ujenzi wa kiwanda kwenye eneo hilo. (Picha na Jackline Amos-MAELEZO)
Sehemu ya Kiwanda cha vyuma cha Kilua kilichopo Kibaha Mkoani Pwani, kiwanda hicho kipo kwenye eneo la ekari 1,000 eneo ambalo limekabidhiwa kwa kituo cha uwekezaji Tanzania TIC kwa ajili ya kuvutia wawekezaji wengi zaidi wa ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujenga viwanda vingine vingi. (Picha na Jackline Amos-MAELEZO).


Na Grace Semfuko-MAELEZO

Wananchi wenye viwanja na maeneo makubwa nchini ambayo yanafaa kwa uwekezaji wameshauriwa kwenda katika kituo cha uwekezaji Tanzania TIC ili kuona ni kwa namna gani wataweza kuyatumia maeneo hayo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda.

Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa huduma kwa wawekezaji kutoka katika Kituo cha uwekezaji Tanzania TIC Bw. Ayoub Sizya wakati akitembelea na kukagua eneo la ukanda wa uwekezaji na mauzo ya ndani na nje ya nchi la Kilua lililopo kijiji cha Disunyala Kata ya Mlandizi Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani.

TIC imeingia makubaliano na Mmiliki wa eneo la ukanda wa uwekezaji kwa ajili ya mauzo ya ndani na nje ya nchi la Kilua lililopo Kijiji cha Disunyala Kata ya Mlandizi Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani lenye zaidi ya ekari 1000 ambalo ni maalum kwa ajili ya ujenzi wa Viwanda.

“Sisi TIC tumeingia makubaliano na Ukanda huu wa uwekezaji wa Kilua lengo letu ni kuimarisha shughuli za uwekezaji,tunafanya hivi ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi,kama unavyojua eneo hili linamilikiwa na mtu binafsi,na ni eneo kubwa ,hivyo tukiungana tutaleta wawekezaji wengi zaidi na Tanzania ya Viwanda itazidi kusonga mbele” alisema Ayoub Sizya Kaimu Mkurugenzi wa huduma kwa wawekezaji TIC.

Mmiliki wa eneo hilo la ukanda wa uwekezaji Bw. Mohammed Kilua amesema watarajia kujenga viwanda zaidi ya 70 na kwamba mpaka sasa kiwanda kimoja kimekamilika ujenzi wake huku vingine saba vikiwa katika hatua mbalimbali za ujenzi ambapo ifikapo mwishoni mwa mwaka huu viwanda 20 vitakuwa vimeanza ujenzi.

“Tutajenga viwanda vingi, ni zaidi ya 70 na kwenye eneo hili tayari tumepata maombi ya zaidi ya ujenzi wa viwanda 20 kwa mwaka huu, Tanzania ya Viwanda itafanikiwa tu,lengo letu ni kuunga mkono juhudi za Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli” alisema Mohammed Kilua Mkurugenzi wa eneo la ukanda wa uwekezaji la Kilua Bw.Mohammed Kilua.

Kampuni ya Kamaka ni moja ya makampuni yanayowekeza kiwanda katika eneo hilo la Kilua, kwa upande wao wamesema ushirikiano baina ya kilua na TIC utaleta tija ya uzalishaji wa viwanda na kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli ya uchumi wa viwanda na kufikia uchumi wa kati.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo ya KAMAKA Bw. Jurijs Matinovs amesema wamejiandaa kuwekeza kwa nguvu zao zote na kwamba watahakikisha wanaendeleza juhudi za Rais Dkt John Pombe Magufuli.

Eneo hilo maalum la uwekezaji mpaka sasa litatumia zaidi ya shilingi bilioni 15 za kitanzania kwa ajili ya kuweka miundombinu ya umeme,maji na barabara ambazo zitawezesha kufikika kirahisi kwenye viwanda vitakavyojengwa.

No comments: