Na Mwandishi wetu, Kondoa
WAKULIMA
wa Mbaazi na Choroko hapa nchini wanatarajia kuondokana na adha ya
mazao yao kukosa soko baada ya wawekezaji kadhaa kujitokeza kuwekeza
katika ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao hayo katika mikoa ya
Arusha, Dodoma, Dar es Salaam na Morogoro.
Kauli
hiyo ya matumaini kwa wakulima hao imetolewa wilayani Kondoa mkoani
Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. Omari Mgumba, wakati akitoa
salaam kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Jimbo la
Kondoa, ambapo Mbunge wa Jimbo hilo, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, aliwasilisha taarifa ya
utekelezaji wa Ilani ya chama hicho kwa kipindi cha miaka 3 ya uongozi
wa Serikali ya Awamu ya Tano.
"
Kilimo kinategemewa na zaidi ya asilimia 65 ya watanzania, lakini zao
la mbaazi limekuwa na matatizo ya soko ndio maana Serikali imeamua
kuchukua hatua kwa kuwahamasisha wawekezaji kujenga viwanda vya
kusindika mazao hayo hapa hapa nchini, jambo ambalo limeanza
kutekelezwa" alisema Mhe. Mgumba
Alisema
hivi sasa viwanda vitatu vya kuchakata mbaazi vinajengwa mkoani
Arusha, Dar es Salaam na Morogoro katika eneo la Mtego wa Simba, huku
kiwanda kimoja na kusindika choroko kikijengwa mkoani Dodoma.
Alisema
kuwa lengo la hatua hizo ni kujibu kero ya muda mrefu ya wakulima wa
mazao hayo katika mikoa ya Manyara, Arusha, Dodoma na maeneo mengine
yanayolimwa mazao hayo kukosa soko la uhakika kwa kuongeza thamani ya
mazao hayo hapa hapa nchini.
"Ukiongeza
thamani ya hizi mbaazi unapanua soko katika dunia badala ya kutegemea
soko moja tu la nchini India, ambapo sasa mbaazi zitauzwa nchi
mbalimbali zikiwemo nchi za kiarabu, Ulaya na Marekani" Alisisitiza
Mgumba.
Awali,
Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na Mbunge wa Jimbo la Kondoa, Dkt.
Ashatu Kijaji alimweleza Naibu Waziri huyo wa Kilimo kwamba Wilaya ya
Kondoa ina wakulima wengi ambao wanahitaji kuboreshewa mazingira yao ya
kilimo ili waweze kujikwamua kiuchumi
"Watu
wanasema Kondoa ni vijijini kwa asilimia 100 lakini kwa kasi
tunayokwenda nayo, baada ya miaka 5 Jimbo hili litakuwa miji mitupu
katika kata zote 21 na kitakacho tuvusha kwenda kwenye miji hiyo ni
kilimo" alisisitiza Dkt. Kijaji
Mbaazi
imekosa soko katika miaka mitatu mfululizo ambapo bei hiyo ilishuka
kutoka shilingi 2,500 na 3,000 kwa kilo mwaka 2015 na kufikia bei ya
shilingi 250 hadi 300 kwa kilo jambo linalowakatisha tamaa wakulima huku
wafanyabiashara na baadhi ya wakulima wakiwa na shehena ya zao hilo
kwenye maghala wakisubiri kupanda kwa bei.
Naibu
Waziri wa Kilimo, Mhe. Omari Mgumba, akitoa salaam kwenye Mkutano Mkuu
Maalumu wa Chama cha Mapinduzi CCM, Jimbo la Kondoa, ambapo Mbunge wa
Jimbo hilo, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt.
Ashatu Kijaji, aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya chama
hicho kwa kipindi cha miaka 3 ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano,
katika Jimbo la Kondoa, uliofanyika katika Kata ya Pahi, Wilayani
Kondoa.
No comments:
Post a Comment