Tuesday, October 23, 2018

WAKULIMA SKIMU YA UYOLE WAOMBA KUTEMBELEWA NA WAKALA WA VIPIMO

Wakulima, katika skimu ndogo ya kilimo cha mbogamboga ya Iganjo Iliyopo Iliyopo Uyole nje kidogo ya jiji la Mbeya, wameomba wataalam kutoka wakala wa vipimo kuwatembelea ili kuweza kusaidia tatizo la vipimo halisi vya mazao yao ambavyo vinafanywa katika hali ya udanganyifu na kuwasababishia hasara. 

Hayo yemeelezwa na Mwenyekiti wa chama cha Wamwagiliaji Iganjo Bw. John Soda alipokuwa akizungumza katika eneo hilo mbapo alisema kuwa suala la kuzidisha ujazo unaotakiwa (lumbesa) bado ni tatizo jambo ambalo linawasababishia wao kama wakulima kuuza mazao yao kwa bei ya hasara.

Bwana Soda alisema kuwa kumekuwa na tatizo la upimaji wa mazao katika magunia ambapo magunia yanayokaguliwa yanakuwa na vipimo halisi lakini magunia yanayokwenda sokoni yanakuwa hayana uhalisia. Tunawaomba wakala wa vipimo waweze kuja kututembelea na kusimamia kwa ukaribu swala hili la udanganyifu katika vipimo, jambo ambalo kwa kiasi fulani limekuwa likitusababishia hasara sisi wakulima wa mboga mboga hasa katika zao la viazi, vitunguu na karoti, Pamoja na hilo naiomba serikali iweke utaratibu wa kuuza mazao na kutoa bei elekezi.” Alisema Bwana Soda.

Kwa Upande wake Bwana Solomon Soda Mkulima katika skimu hiyo aliishukuru Serikali kwa ukarabati na ujenzi wa miundombinu katika skimu hiyo na kuiomba iendelee kuwasaidia waweze kupata pembejeo kwa bei ya ruzuku, na kumalizia kuboresha miundombinu katika sehemu iliyobakia.

Aidha Bw. Solomon alisema kuwa, katika skimu hivyo ambayo ipo pembezoni mwa mto Nkwanana kumekuwa na upandaji wa miti ya mikaratusi ambayo inafyonza maji na kusababisha mto huo kukauka maji hivyo “ Naiomba Serikali itusaidie tuitoe miti hii na kupanda miti mingine ambayo ni rafiki kwa mazingira maaana miti ya mikaratusi inatabia ya kunyonya maji na inaweza kusababisha mto huu kukauka au kupelekea upungufu wa maji.”

Sambamba na hilo Bw. Solomon aliiomba serikali na mamlaka husika kufanya ukaguzi katika maduka yanayouza madawa ya kilimo mkoani Mbeya kwani kuna wasiwasi kuwa madawa mengi yanakuwa yamepitwa na wakati.

Kwa upande mwingine wakulima hao wameeleza kuwa kilimo cha umwagiliaji kimewapa manufaa makubwa ikiwa ni pamoja na kujenga na kuishi katika nyumba za kisasa, kuwasomesha watoto na kuongeza kipato familia na kuchangia katika maendeleo ya eneo hilo kwa ujumla.

Skimu ya kilimo cha umwagiliaji Uyole imekarabatiwa kwa fedha za serikal kupitia mfuko wa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji Wilayani Mbeya.

Katika picha ni Miundombinu mfereji wa maji unaopeleka maji katika skimu ya umwagiliaji Iganjo Uyole mkoani Mbeya, pembeni yake ni shamba la mahindi yanayomwagiliwa kwa kutumia maji yanayopita katika mfereji huo. 

Bwana John Soda mkulima katika skimu ya Iganjo Uyole Mkoani Mbeya akizungumza kuhusu ukarabati uliyofanywa na Serikali ya awamu ya tano katika skimu hiyo, inayoonekana kwa nyuma ni sehemu ya miundombinu hiyo.

Katika Picha ni banio linaloruhusu maji toka chanzo cha maji cha mto Nkwanana kupeleka katika skimu ya umwagiliaji ya iganjo iliyopo Uyole mkoani Mbeya.

No comments: