Sunday, October 14, 2018

WAGONJWA WA MACHO 379 KITETO WATIBIWA BURE

Mkazi wa eneo la Kibaya Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, akipatiwa maelezo ya matibabu bure ya ugonjwa wa macho. 
Mganga wa macho wa hospitali ya Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, akimpima macho mkazi wa mtaa wa Kaloleni, Juma Ally. 
Mganga wa macho wa hospitali ya Wilaya ya Kiteto, Mkoani Manyara, Dk Enock Awary akimpima macho mkazi wa Kibaya, Khadija Hamis ambapo watu 379 walipatiwa vipimo na matibabu bure
Baadhi ya wananchi wa kata ya Kibaya Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, walio na matatizo ya macho wakipewa maelezo ya namna ya kupata matibabu. 


WAGONJWA wa macho 379 wa Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara wamepatiwa huduma ya vipimo na matibabu ya macho bure kwenye maadhimisho ya siku ya macho duniani.

Katika kuadhimisha siku hiyo wataalamu wa afya kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la ‘Kilimanjaro Center for Community Opthmology ( KCCO) kupitia mradi wa (TRACHOMA SAFE) wametoa huduma ya kupima macho, ushauri, kutoa dawa sambamba na kuwapangia tarehe ya kurudi kwa ajili ya uchunguzi zaidi na upasuaji wagojwa ambao wameonekana kwamba matatizo yao ya macho yanahitaji upasuaji.

Akizungumza kwenye maadhimisho hayo Mganga mkuu wa wilaya ya Kiteto Dkt Malkiadi Paschal Mbota alisema ugonjwa wa Trakoma ni tatizo kubwa na idara ya Afya kwa kushirikiana na KCCO wamekuwa wakienda katika maeneo yote ya vijijini kutoa hudumaza ushauri, dawa, upasuaji, kutoa elimu juu ya umuhimu wa kusafisha uso kwa maji safi pamoja na usafi wa mazingira kwa ujumla kwa lengo la kutokomeza ugonjwa huo.

Dkt Mbota alitoa wito kwa jamii, hususani jamii ya kifugaji kujenga tabia ya kunawa uso kwa maji safi mara kwa mara ili kuepuka ugonjwa wa Trakoma. “Mikakati ya wilaya katika kukabiliana na ugojwa huo, kwa kushirikiana na KCCO tumekuwa tukienda kijiji hadi Kijiji kuwatambua wagonjwa na tukishawatambua, madaktari wetu na manesi wamejengewa uwezo wa kutosha kuwapatia huduma zote zinazotakiwa ikiwemo upasuaji, wanaweka mahema hukohuko vijijini wanawafanyia upasuaji,” alisema.

Daktari wa macho wa hospitali ya wilaya ya Kiteto, Dkt Enock Thomas Awary alisema wamejipanga kuhudumia watu wote watakaofika uwanjani hapo kwa lengo la kupata huduma za matibabu ya macho, na wale ambao hawatakuwa wamefikiwa, huduma hiyo itaendelea hadi mwisho wa wiki. 

Dkt Awary alisema huduma wanazotoa ni bure, hivyo watu wote wenye matatizo ya macho wasiache kufika ili wapate huduma hiyo itafika hadi vijijini. Alisema wameandika barua kwa waganga wafawidhi wa vituo vya afya na zahanati zote kuwaelekeza utaratibu, kuhakikisha watu wote wanaohitaji huduma wanafikiwa na huduma hiyo.Mratibu wa mradi wa Trakoma Mkoa wa Manyara, Agnes Lukumay alisema lengo la KCCO kufadhili utoaji wa huduma hizo za matibabu ya macho katika maadhimisho ya siku ya macho duniani ni kuzuia upofu unaozuilika.

Lukumay alisema takwimu zinaonyesha kuwa kwa mkoa wa Manyara ugonjwa huo uko juu zaidi kwa wilaya za Kiteto na Simanjiro.Alitoa wito kwa jamii kujitokeza kupata huduma hizo za matibabu ya macho kwa sababu zinatolewa bure, hivyo wasiache fursa hiyo iwapite.Shirika la Kilimanjaro Center for Community Opthmology’ limeanza kazi zake mwaka 2015, huku mkataba wake ukiwa ni wa miaka mitano. 

Dhima ya shirika hilo ni kutokomeza ugonjwa wa Trakoma ifikapo 2020.

Hadi sasa shirika limeshahudumia kwa kuwafanyia upasuaji wa macho wagonjwa wa Trakoma 600.

Katika maadhimisho hayo wagonjwa 379 wamefika uwanjani hapo kwa lengo la kupata matibabu, ambapo wagonjwa 205 wamehudumiwa na wengine waliobaki wanaendelea kuhudumiwa hadi mwisho wa wiki.

No comments: