Sunday, October 7, 2018

SERIKALI KUHIFADHI UTAMADUNI WA MAKABILA YALIYO HATARINI KUPOTEA

Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi.Suzan Mlawi akipongeza uongozi wa Four Corner Cultural Programme (4CCP) kwa kuendesha lenye kuenzi Utamaduni,Mila na Desturi za makabila manne yanayopatikana barani Afrika ambayo niyakujivunia leo katika sherehe za kufunga tamasha hilo lililofanyika katika Kijiji cha Hydom Wilaya ya Mbulu Vijijini.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi.Suzan Mlawi akimkabidhi cheti cha ushiriki muwakilishi wa Taasisi ya Hifadhi ya Ngorongoro Bw.Gibson Ngolongolo leo katika sherehe za kufunga tamasha la saba la 4CCP lililofanyika katika Kijiji cha Hydom Wilaya ya Mbulu Vijijini .
Mbunge wa Mbulu Vijijini Mhe.Flatei Massey na Mratibu wa Kituo cha Four Cultural Programme Bi.Eliminata Awet wakiwa wamejiwekea nyoka mabegani anayetumika kuchezea ngoma ya kikiundi cha wasukuma kutoka Mwanza wakati wa Sherehe za Kufunga Tamasha la Four Corner Cultural Festival liloandaliwa na 4CCP na kufanyika leo katika Kijiji cha Hydom Wilaya ya Mbulu Vijijini,wapili kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi.Suzan Mlawi.
Baadhi ya Vijana kutoka Jamii ya Kidatooga wakicheza ngoma ya asili ya kumkaribisha mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi.Suzan Mlawi(hayupo pichani) katika himaya ya nyumba yao iliyopo katika kituo cha makumbusho ya Four Corner Cultural Programme (4CCP) leo katika sherehe za kufunga tamasha la saba la Four Corner Cultural Festival lililofanyika Kijiji cha Hydom,Wilaya ya Mbulu Vijijini.
Jamii ya Wadzabe wakicheza ngoma ya asili mbele ya mgeni rasmi Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi.Suzan Mlawi (hayupo pichani) katika sherehe za kufunga Tamasha la Saba la Four Corner Cultural Festival lililoandaliwa na uongozi wa 4CCP na kufanyika leo Kijiji cha Hydom,Wilaya ya Mbulu Vijijini. 

……………………. 

Na Anitha Jonas – WHUSM – Hydom,Manyara. 

Serikali imejipanga kuanzisha programu ya kukusanya na kuhifadhi taarifa jamii za kitanzania ambazo asili ya utamaduni wake upo hatarini kupotea. 

Kauli hiyo imetolewa leo katika Kijiji cha Hydom,Wilaya ya Mbulu Vijijini, Mkoani Manyara na Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bi. Suzan Mlawi alipokuwa akifunga Tamasha la Saba la Utamaduni wa Pembe Nne (7th Four Corner Cultural Festival) kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Dkt.Harrison Mwakyembe ambaye ndiye alikuwa afunge tamasha hilo. 

Bi.Mlawi alitoa pongezi kwa waandaaji wa tamasha hilo linahusisha makundi manne ya lugha yanayopatikana barani Afrika ila kwa Tanzania yanapatikana mkoani Manyara na jirani ambapo kwa sasa yameanza kupoteza asili yao na utamaduni wake ambayo ni Wahdzabe-Khoisan,Iraqw-Cushits,Datooga-Nilotic na Wabantu-Wanyiramba/ Wanyisanzu. 

“Kupitia Idara ya Utamaduni iliyo chini ya Wizara hii nitaunda Kitengo kitakacho kuwa kinashughulikia suala la ukufanyaji wa taarifa za makabila mbalimbali nchini katika mfumo wa picha jongefu pamoja na uandishi wa historia fupi makabila hayo kwa lengo la kuweza kuhifadhi taarifa hizo kwa maslai ya vizazi vijavyo”alisema Bi.Mlawi. 

Katibu Mkuu huyo aliendelea kueleza kuwa serikali inatambua changamoto ya utandawazi na elimu ambazo ni moja ya sababu ya baadhi ya tamaduni kuanza kupotea na katika hili serikali itasimamia kuendeleza tamaduni zile zilizo nzuri ila kwa zile zilizo mbaya kama ukeketaji kwa watoto wakike serikali itaendelea kupiga vita. 

Kwa upande wa Mratibu wa Kituo cha Pembe Nne za Utamaduni (Four Corner Cultural Programme – 4CCP) Bi.Eliminata Awet alieleza kuwa kituo hicho kilianzishwa kwa lengo la kuhifadhi historia ya makundi ya lugha ya jamii hizo nne ambazo zinapatikana barani Afrika baada kuoneka katika Mkoa wa Manyara umebarikiwa kuwa na jamii zote nne ambapo ni suala la kujivunia na kulitangaza duniani. 

“Kituo cha 4CCP kimekuwa kikiandaa tamasha hili kwa mara ya saba sasa ikiwa lengo ni kutangaza tunu hii ya nchi hii kubarikiwa kuwa na makabila haya manne yanayopatikana barani Afrika na yanaonekana kuanza kupotea kufuatia mabadiliko mbalimbali ya kijamii kama elimu na utandawazi,”alisema Bi Awet. 

Halikadhalika nae Mbunge wa Mbulu Vijijini Mhe. Flatei Massey aliipongeza wizara hiyo yenye dhamana na masuala ya utamaduni kwa namna inavyojitahidi kuwa karibu na wadau wake wa kisekta kwani hii inatia faraja ya kuona kuwa serikali inajali shughuli zao. 

Hata hivyo Katibu Mkuu huyo aliagiza kila mkoa kuanzisha kituo cha kiutamaduni ambacho kitahifadhi historia ya kabila la watu wa mkoa huo pamoja na mila na desturi zao kwa ajili ya vizazi vijavyo kutokana hali ya utandawazi kuanza kupoteza masuala ya kiutamaduni na vituo hivyo vinaweza kutumika kama sehemu ya utalii wa kiutamaduni.

No comments: