Monday, October 15, 2018

Rock City Marathon yazidi kuwavutia washiriki wa kimataifa

Rock City Marathon yazidi kuwavutia washiriki wa kimataifa
Zikiwa zimebaki wiki chache kabla ya kufanyika  kwa mbio za Rock City Marathon, idadi kubwa ya wanaridha wa kimataifa wameonyesha nia ya kuja nchini  ili kushiriki katika mbio hizo zinazotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya mbio hizo wanariadha walioonyesha nia ya kushiriki mbio hizo wengi wanatoka katika nchi za Ethiopia, Ghana, Afrika Kusini, Marekani, Canada, China, Rwanda, Burundi, DRC Congo huku Kenya ikiendelea kuongoza katika orodha ya mataifa ya nje yanaoleta washiriki zaidi katika mbio hizo.
“ Zikiwa zimebaki takribani wiki mbili kabla ya kufanyika kwa mbio hizo tayari zaidi wa washiriki 200 kutoka nje ya nchi wameonyesha nia ya kushiriki mbio hizi na kinachosubiriwa kwasasa ni wao tu kufuata taratibu kupitia Shirikisho la Riadha Taifa (RT). Lengo letu ni kupata washiriki zaidi ya 5000 katika msimu huu,’’ alisema Ngowi katika taarifa yake aliyoitoa kwa vyombo vya habari mapema leo.
“Ni taarifa njema kwetu kuona kwamba baada ya muda mrefu sasa si watanzania bali ulimwengu mzima umeanza kutuelewa nini tunakifanya Kanda ya Ziwa hususani katika jiji la Mwanza…ni ushindi pia kwa sekta ya utalii katika kanda hii.’’alibainisha
Kwa mujibu wa Ngowi, katika kuhakikisha kwamba mbio hizo zinalitangaza vyema  jiji la Mwanza, njia ambazo zimekuwa zikitumika kwa wakimbiaji zinahusisha alama muhimu za jiji hilo ikiwemo jiwe la Bismarck lililopo kwenye fukwe ya Ziwa Victoria, makutano ya mzunguko wa  samaki (The Vic Fish Roundabout), jengo la Rock City Mall pamoja na Daraja la Furahisha na hatimaye kuishia Uwanja wa CCM Kirumba.
Hata hivyo, alishukuru jitihada zinazofanywa na vyombo vya habari nchini kwa kutangaza mbio hizo.
“ Kwa mfano matangazo ya moja kwa moja yaliyofanywa katika kilele cha mbio hizi msimu uliopita yaliwezesha maelfu wa watanzania kuweza kufuatilia mbio hizi wakiwa majumbani kwao nchini kote…mwaka huu pia mbio zitaoneshwa moja kwa moja kupitia telesheni,’’
 “Zaidi kupitia uwekezaji wa jitiahada zetu kwenye mitandao ya kijamii umetuwezesha kuwa karibu na wadau wengi wa mchezo wa riadha hususani nje ya nchi hatua ambayo imetusaidia kuweza kuwavuta kwa urahisi kuja kushiriki katika mbio hizi zinazolenga kutangaza utalii katika kanda ya Ziwa,’’
  “Mipango yetu ya muda mrefu kwa kushirikiana na wadau wetu wakiwemo Puma Energy Tanzania, Tiper, Tanapa, Ttb, Nssf, Gold Crest, New Mwanza Hotel,  Cf Hospital, Dasani,  CocaCola, Metro Fm, Ef Outdoor,  Kk Security, Belmont Fairmount Hotel , Bigie Customs na Global Education Link zinatupeleka tulipotarajia,’’ aliongeza.
Bw Ngowi alivitaja vituo vinavyoendelea na usajili huo kwasasa kuwa ni pamoja na New Mwanza Hotel , Rock City Mall, The  Gym Buzuruga, Nyakato  mecco sokoni, Buzuruga Stand, Biggie co. ltd Mwanza,  Ladies  Collection shop –Kirumba Sokoni, Magu Simiyu, Viwanja vya Nyamagana, Radio Metro Fm, Semira  Eletronics, Lake Radio na Nyegezi  Stand.
Alisema usajili huo pia utahusisha ofisi zote za riadha mikoa ya Geita, Simiyu na Shinyanga huku akiongeza : “Kwa upande wa Dar es Salaam Fomu za ushiriki pia zinapatikana katika jengo la SHAMO Tower, Mbezi Beach , jijini Dar es, Salaam ” 


 Baadhi ya washiriki wa mbio za Rock City Marathon mwaka jana. 

No comments: