Wednesday, October 24, 2018

RC Wangabo aagiza kushughulikia udumavu kuongeza ufaulu

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewaagiza wakurugenzi kushirikiana na madiwani kuhakikisha suala la kupunguza udumavu katika mkoa wa Rukwa linakuwa ni ajenda ya kudumu katika vikao vya mabaraza ya madiwani pamoja na mikutano ya hadhara katika kuwaeleimisha wananchi juu ya athari ya udumavu.

Amesema kuwa suala la udumavu lisisahaulike pindi tunapoangalia ufaulu wa watoto wetu mashuleni, na kuwa mstari wa mbele kutoa ahadi za kuhakikisha watoto wanaongeza ufaulu huku udumavu ukiwa bado haujashughulikiwa.

“Tuone kwamba kama huna hali mbaya ya matokeo ya kielimu yanachangiwa pia na udumavu kwasababu udumavu umekuwa wa muda mrefu na kama tunaukubali upo, sasa kwanini usikubaliane pia na matokeo yanayotokea, tuweke jitihada kubwa sana kuondoa udumavu ili watoto wetu waongeze ufaulu,” Alisisitiza.

Ameongeza kuwa kama si hivyo basi itabidi takwimu udumavu ziangaliwe upya, ama kama kwenye elimu kuna kupasi sana basi kuna wizi wa mitihani ama kuna wageni wengi sana wanaotoka nje kuja kusoma Kwetu.

Mwanzoni mwa mweze wa nane Mh. Wangabo aliingia mkataba wa utendaji kazi na kusimamia shughuli za lishe baina ya Ofisi yake pamoja na wakuu wa wilaya ambapo ni utekelezaji wa maagizo ya Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa mikoa juu ya kupunguza utapiamlo ambao kitaifa ni asilimia 34.

Kwa upande wake mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu alisema kuwa utapiamlo unasababisha udumavu wa akili na mwili na ubongo wa mtoto unaendelea kukua tangu ujauzito mpaka anapofikisha miaka mitano.

“Wananchi wengi hawana uelewa wa kutosha juu ya masuala ya lishe bora na athari za utapiamlo.  Pamoja na kuwa Mkoa unazalisha vyakula vya aina mbalimbali tena kwa wingi, lakini wananchi wengi bado wanatumia aina moja au aina za vyakula vilivyozoeleka kwa muda mrefu bila kuchanganya na aina nyingine za vyakula ili kufikia mahitaji halisi ya virutubishi.” Alisema.

Mkoa wa Rukwa una kiwango cha utapiamlo cha asilimia 56.3 wakati kitaifa ni asilimia nne, na kitaifa mkoa wa rukwa umeshika nafasi ya 19 mwak huu tofauti na mwaka jana ulikuwa wa 15 kitaifa katika matokeo ya darasa la saba. 

No comments: