Thursday, October 11, 2018

NYONGO AAGIZA AFISA MADINI,WATENDAJI,KUSIMAMIA UFUNGAJI NA UFUNGUAJI WA MADININaibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akisaini kitabu cha wageni katika Ofisi za Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Katavi kabla ya kuanza ziara yake katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini tarehe 09 Oktoba, 2018.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kulia) akisalimiana na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi, Mahmood Yass (kushoto) kabla ya kuanza ziara yake katika mgodi huo uliopo katika eneo la Singililwa Wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akiangalia sampuli ya makinikia ya dhahabu katika Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo katika eneo la Singililwa Wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi, Mahmood Yass (kulia) akimwonesha Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (kushoto) moja ya mawe yenye madini ya dhahabu.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akisalimiana na sehemu ya wafanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo katika eneo la Singililwa lililopo Wilayani Mpanda mkoani Katavi.

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) akiendelea na ziara katika Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo katika eneo la Singililwa Wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Mkaguzi wa Migodi kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Katavi, Paul Veran (kushoto) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (katikati) kwenye eneo yanapohifadhiwa makinikia ya dhahabu katika Mgodi wa Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo katika eneo la Singililwa Wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (wa nne kulia) akikagua shughuli za uchenjuaji wa dhahabu zinazofanywa na wachimbaji wadogo katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba yaliyopo katika kijiji cha Kapanda Wilayani Mpanda mkoani Katavi.
Sehemu ya wachimbaji wadogo katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba yaliyopo katika kijiji cha Kapanda Wilayani Mpanda mkoani Katavi wakifuatilia ufafanuzi uliokuwa unatolewa na Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani) katika machimbo hayo.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo akifafanua jambo alipokuwa akizungumza na wachimbaji wadogo katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba yaliyopo katika kijiji cha Kapanda Wilayani Mpanda mkoani Katavi (hawapo pichani).
Mmoja wa wachimbaji wadogo katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba yaliyopo katika kijiji cha Kapanda Wilayani Mpanda mkoani Katavi, Fatuma John akiwasilisha kero yake kwa Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo (hayupo pichani)…………………

Na Greyson Mwase, Katavi

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo ameagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Giliard Luyoka, Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Afisa Usalama wa Wilaya, na Mwakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuhakikisha wanakuwepo wakati wa ufungaji na ufunguaji wa lakiri (seal) kwenye madini ya dhahabu ili kudhibiti utoroshwaji wa madini kwenye migodi.

Ameyasema hayo leo tarehe 09 Oktoba, 2018 mara baada ya kumaliza ziara yake katika Mgodi Dhahabu wa Katavi & Kapufi uliopo katika eneo la Singililwa Wilayani Mpanda mkoani Katavi ikiwa ni sehemu ya ziara yake katika mkoa huo yenye lengo la kukagua shughuli za uchimbaji wa madini, kusikiliza na kutatua kero za wachimbaji wa madini.

Katika ziara yake Nyongo aliambatana na Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Salehe Mhando, Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Katavi (KATAREMA), William Mbongo, Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Giliard Luyoka, Wataalam wa Madini, Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na waandishi wa habari.

Alisema kuwa, ni kosa kubwa la kisheria kwa Afisa Madini Mkazi kufunga au kufungua lakiri (seal) pasipo kushirikisha Mkuu wa Wilaya, vyombo vya ulinzi na usalama na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kusisitiza kuwa iwapo itagundulika Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria.Akielezea mikakati ya Serikali kupitia Wizara ya Madini kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini Nchini, Nyongo alisema kuwa ni pamoja na uboreshaji wa Sheria ya Madini iliyolenga kuondoa mianya ya utoroshwaji wa madini nje ya nchi kwa kuzuia usafirishwaji wa madini ghafi nje ya nchi.

Alisisitiza kuwa, Serikali inakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi katika ujenzi wa mitambo ya kuchenjulia madini ndani ya nchi ili kuyaongezea thamani kabla ya kuuzwa nje ya nchi na kuongeza mapato.

Wakati huohuo akizungumza katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba yaliyopo katika kijiji cha Kapanda Wilayani Mpanda mkoani Katavi yanayomilikiwa na William Mbogo, Naibu Waziri Nyongo alimtaka mmiliki wa leseni kuhakikisha anaandaa mikataba na kusaini pamoja na wachimbaji wadogo wanaoendesha shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo hilo.

Alisema kuwa, Serikali kupitia Wizara yake haipo tayari kushuhudia migogoro kati ya wawekezaji na wachimbaji wadogo wa madini pasipo suluhu inayotokana na ukiukwaji wa Sheria za Madini na kanuni zake.

Katika hatua nyingine, Nyongo alimtaka mwekezaji huyo kutafuta mwekezaji mkubwa kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za uchimbaji madini katika eneo husika iwapo anakosa uwezo wa kuendeleza kama leseni ya madini inavyomtaka.

Aidha, alimwelekeza Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Katavi, Mhandisi Giliard Luyoka kuhakikisha anatafuta maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini, ili waweze kuchimba katika mazingira mazuri huku wakifuata sheria na kanuni za madini.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Nyongo aliwataka wachimbaji wadogo wa madini kuhakikisha wanalipa mrahaba na kodi mbalimbali Serikalini ili mapato yaweze kutumika kwenye uboreshaji wa sekta nyingine kama vile afya, elimu, maji na miundombinu.

Awali mbali na pongezi, wakiwasilisha kero mbalimbali wachimbaji wadogo wa madini wanaoendesha shughuli za uchimbaji madini katika machimbo ya dhahabu ya Mkwamba yaliyopo katika kijiji cha Kapanda Wilayani Mpanda mkoani Katavi yanayomilikiwa na William Mbogo walieleza changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na mitaji midogo, vifaa duni pamoja maeneo rasmi kwa ajili ya uchimbaji madini.

No comments: