Thursday, October 4, 2018

NDITIYE AMFUKUZA MSIMAMIZI WA UJENZI WA BANDARI YA NYEMIREMBE,WILAYANI CHATO.

Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye amemfukuza msimamizi wa ujenzi wa bandari ya Nyemirembe iliyopo wilayani Chato mkoani Geita kwa kukosa sifa na utaalam wa kusimamia ujenzi wa bandari hiyo na miundombinu yake na kuagiza aondolewe mara moja kwenye eneo hilo

Hayo yamejitokeza wakati wa ziara ya Nditiye ya kukagua hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa bandari hiyo na miundombinu yake ambapo mkandarasi wa kampuni ya V.J Mistry & Co. Ltd amepewa jukumu hilo na Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ya kujenga bandari hiyo kwa gharama ya shilingi bilioni 4.128.

Katika ziara hiyo, Nditiye amebaini kuwa msimamizi wa ujenzi wa bandari hiyo Bwana Pravin Rabadhia wa mkandarasi wa kampuni ya V.J Mistry & Co. Ltd, hana utaalamu, sifa wala vigezo vyovyote vya kusimamia mradi huo unaogharimu matumizi ya fedha nyingi zinazotokana na fedha za makusanyo ya kodi ya wananchi. Pia, alibaini uwepo wa Bwana Dipak Chaganlal, mfanyakazi wa kampuni hiyo ya mkandarasi aliyejitambulisha kwa Nditiye kuwa ana taaluma ya “storekeeper” akiwa msimamizi msaidizi wa mradi wa ujenzi wa bandari hiyo.

Nditiye alielekeza msimamizi huyo aondolewe eneo la mradi wa ujenzi wa bandari ya Nyemirembe na mamlaka husika za vibali vya ajira, uhamiaji na mamlaka nyingine za manunuzi, bodi za makandarasi nchini zimchunguze taaluma yake, uraia wake, uhalali wake wa kufanya kazi ya kuwa msimamizi wa mradi huo kwa kuwa katika mahojiano nae akiwa kwenye eneo la mradi huo, wasimamizi hao wenye asilia ya kiasia hawakuweza kutoa maelezo yoyote ya kitaalamu kuhusu maendeleo ya ujenzi wa bandari hiyo.

Nditiye ameelekeza kuwa kazi hiyo ya ujenzi wa bandari ya Nyemirembe isimame kwa muda wa wiki moja na amemtaka mkandarasi wa kampuni hiyo kufika na kuripoti ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita mara moja akiwa na wataalamu wanaohitajika kufanya kazi hiyo kuendana na matakwa ya mkataba husika na kuhakikisha kuwa wafanyakazi na vibarua wote wanalipwa fedha zao

Ameongeza kuwa, Serikali haiwezi kuvumilia jambo hili kwa kuwa tayari imemlipa mkandarasi malipo ya awali ya asilimia 20 kuendana na makubaliano ya mkataba wa ujenzi huo yenye thamani ya shilingi milioni 800 katika kipindi cha miezi miwili iliyoishia ambapo hamna dalili yeyote ya mkandarasi ya kuonesha uwezo wa kujenga bandari hiyo kwa kuwepo na ukosefu wa vifaa na wataalamu kwenye eneo la mradi wa ujenzi wa bandari hiyo

Naye Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel akiwa kwenye ziara hiyo amesema kuwa Serikali ya Mkoa wa Geita haiko tayari kufanya kazi na mkandarasi wa namna hii labda wakafanyie kazi zao nje ya Wilaya ya Chato na Mkoa wa Geita kwa kuwa Serikali imeifanya Wilaya ya Chato kuwa eneo la kimkakati la uwekezaji ili iweze kuhudumia mikoa ya Geita, Simiyu na Kagera. 
 
“tunapata hamasa kubwa kwa kuona bandari ya Nyemirembe iliyokufa inafanyiwa kazi ili biashara ya usafirishaji wa mizigo na abiria ifanyike na tutumie fursa zilizopo kwa kuwa Serikali inabadilisha matumizi ya pori la akiba la Biharamulo na kuwa hifadhi ya taifa, hivyo ujenzi wa miundombinu kutainua fursa na kuleta watalii,”amesema Gabriel. Naye Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon akiwa katika ziara hiyo alisema kuwa Chato ni kituo kikubwa cha uwekezaji, sekta ya utalii itatumia bandari hii. Bandari iwe ya kutosheleza abiria 200 hadi 300 na tuangalie namna ya kupanua eneo ili litoshe mahitai ya miaka 10 hadi 20 baadae

Kaimu Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria Bwana Morris Mtindichiusa amemweleza Nditiye kuwa, mkandarasi amesaini mkataba wa ujenzi wa bandari ya Nyemirembe na miundombinu yake ikiwemo gati la kupakia na kupakua mizigo, ujenzi wa jengo la abiria, ujenzi wa ghala la kuhifadhia mizigo, ujenzi wa mnara wa tanki la maji, ujenzi wa vyoo, jengola walinzi, jengo la kuhifadhia jenereta, uzio na mageti yake.

Ameongeza kuwa mkandarasi ameanza kazi rasmi tarehe 2 Agosti, 2018 ambapo mkataba ulisainiwa tarehe 13 Juni 2018 na mkandarasi alikabidhiwa eneo la mradi tarehe 17 Julai, 2018. Mkataba huo ni miezi 12, hivyo ujenzi wa bandari ya Nyemirembe na miundo mbinu yake unahitajika kukamilika katika kipindi cha mwaka mmoja.

Amefafanua kuwa bandari hiyo itakuwa na ghala la mizigo lenye uwezo wa kuhifadhi tani 3000 za mizigo na jengo la abiria litakuwa na uwezo wa kuchukua abiria 200 hivyo watazingatia maelekezo yaliyotolewa ili liweze kuchukua abiria 300. Pia, amesema kuwa kasi ya ujenzi wa bandari hiyo na miundombinu yake ni ndogo na hairidhishi kwa kuwa kwa kiasi cha fedha ambayo mkandarasi amelipwa alitakiwa awe amefikia asilimia 9 ya ujenzi badala ya asilimia 6 waliyofikia sasa. 
 
Hivyo, ameahidi kuzingatia na kutekeleza maelekezo yalitolewa ya kumuondoa msimamizi wa mradi huo kwenye eneo la ujenzi wa bandari hiyo na kuhakikisha kuwa mkandarasi wa kampuni hiyo anafika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Chato kuripoti na kujitambulisha ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa kampuni hiyo inaweka msimamizi wa mradi mwenye utaalamu na ujuzi unaotakiwa


Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano 


Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (kulia) akikagua maendeleo ya ujenzi wa bandari ya Nyemirembe iliyopo wilayani Chato, Geita. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel na wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo Mhandisi Mtemi Msafiri Simeon
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye akimhoji mfanyakazi wa mkandarasi wa kampuni ya V.J Mistry & Co. Ltd Bwana Dipak Chaganlal (mwenye asili ya kiasia) kuhusu maendeleo ya ujenzi wa bandari ya Nyemirembe iliyopo wilayani Chato, Geita. Mwenye kofia nyeusi ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel
Kaimu Meneja wa Bandari za Ziwa Victoria Bwana Morris Mtindichiusa akiandika maelekezo ya Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (wa kwanza kulia) kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya Nyemirembe iliyopo wilayani Chato, Geita. Mwenye kofia nyeusi ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhandisi Robert Gabriel 
Wafanyakazi wa kampuni ya mkandarasi ya V.J Mistry & Co. Ltd wakiendelea na kazi mbali mbali za ujenzi wa bandari ya Nyemirembe iliyopo wilayani Chato, Geita wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Uchukuzi n Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa bandari hiyo

No comments: