Thursday, October 11, 2018

NBS: Utafiti wa Huduma za Uzazi wa Mpango na Huduma za Uzazi Kufanyika hivi Karibuni

Mkurugenzi wa Shughuli za Kitakwimu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Irenius Ruyobya akizungumza leo mkoani Morogoro kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NBS, Dkt. Albina Chuwa wakati wa ufunguzi wa Semina ya mafunzo ya wadadisi wa Utafiti wa kutathmini upatikanaji wa Huduma za Uzazi wa Mpango.
Baadhi ya wadadisi wa utafiti wa kutathmini upatikanaji wa Huduma za Uzazi wa Mpango ambao ni wauguzi na madaktari kutoka katika Hospitali na Zahanati mbalimbali nchini wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayoendelea mkoani Morogoro.
Baadhi ya wadadisi wa utafiti wa kutathmini upatikanaji wa Huduma za Uzazi wa Mpango ambao ni wauguzi na madaktari kutoka katika Hospitali na Zahanati mbalimbali nchini wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo yanayoendelea mkoani Morogoro. 


UTAFITI wa kutathmini upatikanaji wa Huduma za Uzazi wa Mpango pamoja na dawa zinazohusiana na huduma za uzazi nchini utanarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi Oktoba waka huu.

Akifungua mafunzo ya siku kumi na moja kwa wadadisi wa utafiti huo, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Dk. Albina Chuwa amesema taarifa zitakazokusanywa kwenye utafiti huo ni pamoja na upatikanaji wa njia za uzazi wa mpango katika ngazi mbalimbali za vituo vya kutolea huduma za afya.

Aidha, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu huyo, utafiti huo utakusanya taarifa zinazohusu mfumo wa ugavi wa dawa au vifaa vinavyohusiana na njia za uzazi wa mpango pamoja na huduma za uzazi na uwepo wa watumishi waliosomea utoaji wa huduma hizo.

Utafiti huo ambao ni mara ya tatu kufanyika nchini kuanzia mwaka 2015 utaangalia pia uwepo wa miongozo mbalimbali kutoka wizara za afya inayoongoza huduma hizo na pia utakusanya maoni ya wateja waliofika kwenye kituo husika kwa ajili ya huduma za uzazi wa mpango.

Dk. Chuwa aliwaeleza washiriki wa mafunzo hayo kuwa, katika utafiti huo ambao utaangalia uwepo na upatikanaji wa huduma hizo katika kipindi cha miezi mitatu kabla ya siku ya utafiti na uwepo wake siku ya utafiti, unatekelezwa kwa mara ya kwanza na ofisi za takwimu za Tanzania Bara na Zanzibar.

Aliwapongeza washiriki kwa kuchaguliwa kuhudhuria Mafunzo hayo baada ya kushinda usaili ambao ulikuwa wenye ushidani mkubwa na kueleza matumaini yake kuwa watajifunza kwa bidii ili waweze kufanya kazi ya kukusanya taarifa kwa usahihi na ufanisi mkubwa na kuwezesha kupata takwimu bora.

Mkurugenzi Mkuu huyo aliwaeleza washiriki kuwa lengo la mafunzo haya ni kuwawezesha kufahamu taratibu zote zinazohusu kazi ya ukusanyaji wa taarifa na mbinu zinazotakiwa ili kupata taarifa sahihi kutoka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vilivyochaguliwa.

“Katika muda wa siku kumi na moja mtafundishwa madhumuni ya kila swali litakaloulizwa kwenye utafiti huu, mbinu za kuhoji na namna ya kujaza taarifa kwa kutumia Kishikwambi (tablet) pamoja na kushiriki kwenye mazoezi ya vitendo katika baadhi ya vituo vya kutolea huduma za afya hapa mkoani Morogoro” Dr. Chuwa alibainisha.

Katika hotuba yake hiyo iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Huduma za Kitakwimu wa NBS Irenius Ruyobya, Mkurugenzi Mkuu aliwakumbusha washiriki kuwa taarifa zitakazokusanywa katika utafiti huo zitatuzwa kwa usiri mkubwa kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015.

Katika mnasaba huo, aliwaeleza washiriki ambao wengi wao ni watumishi wa afya kuwa watapaswa kula kiapo cha kutunza siri kwa mujibu wa sheria hiyo.“Napenda niwakumbushe kuwa kazi ya kukusanya taarifa mtaifanya baada ya kusaini mkataba maalum ambao unaweza ukatenguliwa wakati wowote iwapo mtakiuka taratibu, hivyo nawasihi muwe makini katika utendaji wenu wa kazi” Dk. Chuwa alisisitiza.

1 comment:

Unknown said...

Unafanyaje ili ushiriki kwenye semina!?