Sunday, October 14, 2018

NAIBU WAZIRI OLE NASHA AWATAKA WAHITIMU FEZA KUEPUKA VITENDO VIOVU

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha amewataka wahitimu wa darasa la saba katika shule ya Msingi Feza kuepuka vitendo viovu ambavyo vinaweza kukatisha ndoto zao katika maisha. 

Ole Nasha ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam katika mahafali ya 15 ya darasa la saba ya shule hiyo na kuwataka vijana hao kutambua kuwa kuhitimu katika hatua hiyo ndio mwanzo wa safari ndefu waliyonayo katika Elimu na kuwa nidhamu pekee ndio msingi wa mafanikio.

“Jamii yetu kwa sasa inakabiliwa na mmomonyoko wa maadili vitendo viovu kama vile vijana kujishirikisha katika masuala ya ngono, ulevi, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii jihadharini navyo sana katika maisha yenu, mkijiingiza tu mtaharibu ndoto zenu mlizojiwekea na matokeo yake mtashindwa kushiriki katika jitihada za kuijenga nchi yenu,” alisisitiza Naibu Waziri Ole Nasha

Alisema Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa Sekta binasfi katika maendeleo ya Elimu nchini kwa kuwaandaa vijana kimaadili na kitaaluma ili kufikia dira ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 inayolenga kuwa na mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa, stadi, umahiri, uwezo na mitizamo chanya ili kuweza kuchangia katika kuleta maendeleo ya Taifa.

“Mtaona Serikali sasa imefuta tozo na kodi ambazo zilikuwa ni kero kwa wamiliki wa Shule binafsi kama vile Tozo ya Uendelezaji Ujuzi (Skills Development Levy-SDL), Tozo ya Zimamoto, Kodi ya Mabango na Tozo ya Usalama Mahali pa Kazi (Occupational Safety and Health Administration-OSHA) hii yote ni kuthamini mchango mkubwa ambao mmekuwa mkiutoa katika kuelimisha vijana wa Taifa hili,” aliongeza Naibu Waziri Ole Nasha.

Hata hivyo amewataka wamiliki wote wa shule nchini kutambua kuwa pamoja na shule kuwa zao wanatakiwa kufuata taratibu, sheria na kanuni katika uendeshaji wa shule hizo kwa ni bado elimu itolewayo ni mali ya umma na watoto ni wa kitanzania. 

Naye Mkurugenzi wa Shule za Feza Ibrahimu Yunus anasema kwa sasa shule hiyo ya Msingi ina jumla ya wanafunzi 770 ambapo wanaohitimu darasa la saba mwaka huu ni jumla ya wanafunzi 75 huku shule hiyo ikijivunia kufanya vizuri kwenye masuala ya Elimu katika ngazi zote zinazotolewa shuleni hapo.

Imetolewa na 
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akihutubia wakati wa mahafali ya kumaliza Elimu ya Msingi Feza yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam. Amewataka wahitimu kuwa na nidhamu, bidii na kutanguliza uzalendo katika yale watakayokuwa wakifanya ili kuweza kufikia malengo yao.
Baadhi ya Wahitimu wa Darasa la Saba katika shule ya Msingi Feza wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Mh William Ole Nasha wakati wa mahafali yao yaliyofanyika jana Oktoba 13,108 jijini Dar es salaam. 1. 
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia William Ole Nasha akigawa cheti kwa mmoja wa wanafunzi aliyehitimu darasa la saba mwaka huu katika shule ya Msingi Feza wakati wa mahafali yao yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Oktoba 13, 2018.

No comments: