Friday, October 19, 2018

DK.MABODI AMUOMBEA KURA MGOMBEA WA CCM JANG’OMBE


NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdalla Juma Saadalla ‘Mabodi’ (kulia), akimnadi na kumuombea kura mgombea wa tiketi ya CCM katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Jang’ombe Ramadhan Hamza Chande(kushoto) katika kampeni za CCM Uchaguzi wa Jang’ombe zilizofanyika Uwanja wa Kwaalinatu.
BAADHI ya Wana –CCM walioudhuria katika Mkutano huo wa kampeni uliofanyika Kwaalinatu.
Mgombea uwakilishi wa CCM Jimbo la Jang’ombe Ramadhan Hamza Chande akiomba kura kupitia mkutano huo wa kampeni uliofanyika uwanja wa Kwaalinatu.
MKE wa Rais mstaafu wa awamu ya nne ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Salma Kikwete akimuombea kura Mgombea wa tiketi ya CCM Uchaguzi wa Jang’ombe Ramadhan Hamza Chande.

NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla ‘Mabodi’ amewatahadharisha wanachama wa chama hicho, kuwa makini kwa kuepuka propaganda na njama chafu zinazofanywa na viongozi wakuu wa CUF waliotengeneza migogoro bandia ili waweze kupata huruma ya wananchi kuingia madarakani.

Tahadhari hiyo aliitoa wakati akimnadi mgombea wa nafasi ya Uwakilishi kwa tiketi ya CCM Ramadhan Hamza Chande katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Jang’ombe huko katika Uwanja wa Kwaalinatu.

Alisema CUF wametengeneza mgogoro bandia wenye lengo la kuiyumbisha CCM mwaka 2020 mbinu dhaifu ambazo hazitoweza kufanikiwa mbele ya CCM ya sasa iliyokuwa imara na inayokwenda sambamba na ulimwengu wa siasa za Kisayansi.

Dk. Mabodi alisema ushahidi pekee wa kuonyesha kuwa viongozi wa CUF hawana uadui kwa upande wa Zanzibar na Tanzania bara ni pale waliposhirikiana kumnadi mgombea wa Chama hicho katika kampeni za Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Liwale ambao mgombea wa CCM ameibuka mshindi.

Akimnadi na kumuombea kura Mgombea wa CCM katika Uchaguzi wa mdogo wa Jimbo la Jang’ombe Ramadhan Hamza Chande, Dk. Mabodi aliwasihi Wana-CCM na wananchi wa Jimbo hilo kumchagua mgombe huyo ili aendeleze mambo mema yaliyoasisiwa na viongozi wa waliopita wa nafasi hiyo.

Alisema CCM imempitisha Ramadhan ikiamini kuwa ana uwezo na anafaa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015/2020 kwa kasi kubwa.

“Mgombea huyo ni mbunifu, mchapakazi na mwenye uzalendo wa kweli nakuombeni wananchi wa Jang’ombe mfanye maamuzi sahihi ya kumpa kura nyingi za ndio aweze kuwatumikia kwa uadilifu.

Pia Ramadhan Hamza nakusisitiza kuwa ukipewa nafasi ya Uongozi wewe utakuwa ni kiongozi na mwakilishi wa Wananchi wote na sio CCM hivyo utatakiwa kuwatumikia bila upendeleo wala ubaguzi”, alisisitiza Dk.Mabodi.

Akieleza namna Chama kilivyojipanga kuwaletea maendeleo Wananchi, Dk.Mabodi alisema CCM inafanya siasa za kuimarisha maendeleo katika sekta zote Mijini na Vijijini ili kumaliza ahadi zote zilizotolewa katika Uchaguzi mkuu uliopita kabla ya mwaka 2020.

Dk.Mabodi aliongeza kuwa Chama kimekuwa kikishuka kwa wananchi wa makundi yote kwa lengo la kuratibu changamoto na kuzitatua kwa wakati.

Naye Mgombe wa tiketi ya CCM katika Uchaguzi mdogo wa Jang’ombe Ramadhan Hamza Chande, aliwaomba wananchi na wanachama wa CCM wa jimbo hilo kukichagua Chama Cha Mapinduzi kupitia mgombe huyo aweze kuwatumikia na kuharakisha maendeleo ya Jang’ombe.

Katika maelezo yake Ramadhan alisema atakapopewa rdhaa na wananchi hao ya kuwa kiongozi atashirikiana nao kupanga mikakati ya kupanga mikakati yenye tija ndani ya Jimbo hilo.

Awali Mke wa Rais mstaafu wa awamu ya nne ya Jamhuri ya Tanzania Mama Salma Kikwete, alisema matunda yanayotokana na sera na mipango endelevu ya CCM yanaonekana wazi wazi kwani Zanzibar na Tanzania bara zote zinang’ara kwa miundombinu ya kisasa ya barabara na kuimarika kwa Sekta za Elimu, Afya pamoja na Maji safi na Salama.

Alisema CCM imekuwa ikiendeleza misingi ya maendeleo iliyoasisiwa na Vyama vya ukombozi vya ASP na TANU vilivyoungana na kuunda taasisi hiyo kwa nia ya kuongeza nguvu za kusimamia ufanisi sera na mipango ya maendeleo kwa wananchi wote.

Akizungumza katika Mkutano huo wa kampeni aliyekuwa kiongozi wa ngazi za juu wa CUF Julius Mtatiro aliyejiunga na CCM, aliwaomba wananchi wa Jang’ombe kumchagua mgombea wa CCM kwani vyama vya upinzani hasa CUF vina matatizo na migogoro isiyoweza kutatulika kutokana na ubinafsi na sera za ubaguzi za viongozi wa vyama hivyo.

Mtatiro alitumia mkutano huo kuwaomba radhi Watanzania hasa Vijana wa CCM kuwa kipindi yupo upinzani alitumiwa vibaya na CUF kukwamisha mipango ya maendeleo iliyokuwa ikitekelezwa na Serikali zote mbili za Chama Cha Mapinduzi.

Alisema kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 aliyohudumu katika CUF, hakuna hata siku moja Chama cha CUF ama UKAWA waliyoweza kushauri ama kupongeza mambo mema yanayofanywa na CCM badala yake waliponda na kupotosha umma kwa makusudi.

“Nakuombeni vijana wenzangu mnisamehe sana nilipoteza muda na nguvu nyingi kwa upinzani lakini baada ya kuona kasi ya maendeleo katika CCM ya sasa nikaona bora nitoke kule na kujiunga na CCM ili niwatumikie Watanzani ’’, alieleza Mtatiro.

Akizungumza Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Abdallah Hasnuu Makame, akimuombea kura mgombea wa CCM katika mkutano huo wa kampeni alisema mafanikio makubwa yaliyopatikana yametokana uwepo wa tunu za Taifa ambazo ni Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 pamoja na Muungano wa Serikali mbili.

Alisema wananchi wa Jimbo la Jang’ombe hawatojutia maamuzi yao endapo watamchagua mgombea wa CCM aweze kuwaongoza kwa kipindi cha miaka miwili kufika 2020, kwani historia ya siasa za Tanzania toka mwaka 1992 ulipoasisiwa mfumo wa vyama vingi CCM ndio Chama pekee kilichoweza kutimiza kwa vitendo matakwa ya wananchi katika mfumo wa vyama vingi.

Akizungumza Mwakilishi wa Viti Maalum CCM Mkoa wa Kusini Pemba Mhe. Faida Mohamed Bakari, aliwaomba wanawake na vijana wa Jang’ombe kumchagua Ramadhan awe mwakilishi kwani ana uwezo mkubwa wa kusimamia maslahi ya makundi hayo sambamba na kuanzisha miradi mbali mbali itakayoweza kuwanufaisha wananchi.

Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Jang’ombe unatarajiwa kufanyika Octoba 27, mwaka 2018, kufuatia aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo Abdallah Diwani kuvuliwa uanachama kwa makosa ya ukiukaji wa maadili ya Chama Cha Mapinduzi.

No comments: