Thursday, October 25, 2018

MASHIRIKA YENYE SIFA KAMA ZA NGOs YATAKIWA KUWA NA CHETI CHA UKUBALIFU

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu akitoa taarifa kuhusu usimamizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii jijini Dodoma kushoto ni Niabu wake Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akitoa maelezo kuhusu usimamizi wa uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali katika kusaidia makundi maalum nchini wakati Wizara ilipokuwa ikiwasilisha taarifa kuhusu usimamizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo jijini Dodoma kushoto ni Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Peter Serukamba akitoa maoni yake kwa Viongozi na Watendaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto walipowasilisha taarifa ya usimamizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mbele ya Kamati yake jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. John Jingu akitoa maelezo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo jijini Dodoma kuhusu Marekebisho ya Kanuni za Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na itakavyosaidia kuweka uwazi na uwajibikaji kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kulia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile.
Kaimu Mkurugenzi Idara ya Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Bw. Leornad Baraka akifafanua kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu Usajili na Uratibu wa Mashirika hayo nchini mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii jijini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na watendaji kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakisikiliza hija mbalimbali wakati Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu ilipowasilisha taarifa kuhusu usimamizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mbele ya Kamati hiyo jijini Dodoma.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii na watendaji kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto wakisikiliza hija mbalimbali wakati Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu ilipowasilisha taarifa kuhusu usimamizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mbele ya Kamati hiyo jijini Dodoma. 

Picha na Kitengo cha Mawasiliano- WAMJW 

……………………………………………………………………………………. 

Na Mwandishi Wetu- Dodoma 

Serikali imesema Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ya mwaka 2002 kama ilivyorekebishwa mwaka 2005 imeweka masharti kwa mashirika yaliyokuwa yamesajiliwa katika Sheria nyingine na yanasifa za kusajiliwa kama Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, kuomba Cheti cha Ukubalifu chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali. 

Hayo yamesema mapema leo mjini Dodoma na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati akiwasilisha taarifa ya usimamizi wa Mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Maendeleo ya Jamii. 

Waziri Ummy Mwalimu amesema kimsingi Cheti cha Ukubalifu kinatolewa ili kuyaweka Mashirika yote Yasiyo ya Kiserikali chini ya usimamizi mmoja ili kuondokana na changamoto za awali ambapo mashirika hayo yalikuwa yakiratibiwa chini ya Sheria na Mamlaka zaidi ya moja. 

Waziri Ummy aliwaambia wajumbe wa Kamati hiyo kuwa kutokana na kutungwa kwa Sera na Sheria hii kwa mara ya kwanza Tafsiri ya “Shirika Lisilo la Kiserikali” ilipatikana rasmi akiongeza kuwa Tafsiri hii inayotofautisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Asasi nyingine za kiraia kama vile Jumuia za kijamii zinazosajili Wizara ya Mambo ya Ndani, Makampuni yanayosajiliwa BRELA na Bodi za wadhamini zinazosajiliwa na RITA. 

Aidha Waziri Ummy aliendelea kusema kuwa kufuatia marekebisho ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mwaka 2005, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yalipewa hadhi ya utu inayoyawezesha kumiliki na kuuza mali, kutengeneza faida, kushitaki na kushitakiwa katika vyombo vya Sheria. 

Waziri Ummy amesema hadi kufikia Machi, 2018, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 4,868 tayari yamefanyiwa uhakiki kati ya Mashirika 8,716 ambapo Taasisi 513 zenye sifa za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambazo zilikuwa zimesajiliwa katika Sheria nyingine zilielekezwa kuzingatia matakwa ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa kusajiliwa chini ya Sheria husika. 

Pamoja na uhakiki huo Waziri Ummy amesema bado yapo baadhi ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambayo yamesajiliwa chini ya Sheria nyingine lakini hawakuja kuhakikiwa na wala bado hawajasajili kwenye Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Na. 24 ya mwaka 2002. 

Ameiambia Kamati hiyo kuwa taratibu za kuyaondoa kwenye Regista Mashirika ambayo yamesajiliwa chini ya Sheria hii na hayakujitokeza kwenye zoezi la uhakiki zinaendelea ikiwa ni pamoja na kuyafutia usajili. 

Akiongea kuhusu changamoto za kijamii kwa Mashirika hayo Waziri Ummy alisema uzoefu katika nchi nyingine unaonyesha kuwa baadhi ya Mashirika yametumika kufanikisha vitendo mbalimbali vya kihalifu na hivyo kuhatarisha usalama wa nchi. 

Amevitaja baadhi ya vitendo vya kihalifu ambavyo vinaweza kutumika kupitia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuathiri usalama wa nchi kuwa ufadhili wa ugaidi, Utakasishaji wa fedha haramu, Ujasusi, Usafirishaji wa binadamu, Kuhamasisha chuki dhidi ya Serikali, Kuhamasisha vitendo vinavyokinzana na mila na desturi za Kitanzania ikiwa ni pamoja na matendo ya Ushoga na Usagaji. 

Kwa upande wake Naibu Waziri amesema kuwa wanaendelea na uandaaji wa kanzi data ambayo itasaidia kuhainisha Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kwa sehemu yanapofanyia kazi na kuwezesha Serikali kuratibu vyema shughuli za Mashirika hayo kwa maendeleo ya Taifa. 

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Peter Serukamba amesema kuwa Serikali inawajibu wa kuyaratibu vyema na kuyalea Mashirka hayo kwa mustakhabali wa taifa. 

Akichangia wasilisho hilo mmoja wa wajumbe wa Kamati Mhe. Salma Kikwete amesema kuwa Serikali inatakiwa kuwekewa utaratibu mzuri kwa Mashirika hayo kufanya kazi sehemu ambazo zinachangamoto nyingi. 

Pia Katibu Mkuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. John Jingu ameiambia Kamati kuwa lengo la kufuatilia fedha zinazoingia kupitia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali sio baya bali ni kuweze kujua mchango wa Mashirika hayo katika kuwaletea wananchi maendeleo. 

Wizara katika tamko lake la Mwezi wa tisa iliyataka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali nchini kuwasilisha ripoti ya mwaka 2016/17 yenye taarifa za mapato na matumizi na kutaja chanzo cha fedha kwa shirika husika.

No comments: