Thursday, September 27, 2018

WAZIRI LUGOLA AWAPA WIKI MBILI POLISI KIGOMA KUSAMBARATISHA UJAMBAZI WILAYANI KIBONDO

 Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kibondo, Mkoani Kigoma (hawapo pichani) wakati alipofanya ziara ya kikazi wilayani humo jana kwa ajili ya kusikiliza kero mbalimbali zinazowakabili wananchi pamoja na Taasisi zilizopo ndani Wizara yake. Lugola ametoa wiki mbili kwa Jeshi Polisi mkoani humo, kuhakikisha linakomesha matukio ya ujambazi yaliyokithiri katika Wilaya hiyo pamoja na sehemu zingine mkoani humo. Kulia ni Mwanasheria wa Sekretaireti ya Mkoa wa Kigoma, Said Kamugisha ambaye pia ni Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa huo. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Louis Bura. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibondo, Louis Bura, wakiingia katika ukumbi wa mikutano wa Community Centre mjini Kibondo, kwa ajili ya kuzungumza na watumishi waliopo chini ya Wizara yake. Lugola katika mkutano huo alitoa wiki mbili kwa Jeshi Polisi mkoani humo, kuhakikisha linakomesha matukio ya ujambazi yaliyokithiri katika Wilaya hiyo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Meja Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga akizungumza katika Kikao cha Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (wapili kushoto) kuhusu masuala mbalimbali ya mkoa wake, baada ya Waziri Lugola kufanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Kibondo mkoani humo, jana. Lugola katika mkutano wa hadhara na wanannchi mjini humo, alitoa wiki mbili kwa Jeshi Polisi mkoani humo, kuhakikisha linakomesha matukio ya ujambazi yaliyokithiri mkoani humo. Kulia ni Mwanasheria wa Sekretaireti ya Mkoa huo, Said Kamugisha. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Louis Bura. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (katikati) akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kibondo, katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa wilaya hiyo. Waziri Lugola akizungumza katika mkutano wa hadhara na wananchi wa Kibondo, alitoa wiki mbili kwa Jeshi la Polisi mkoani Kigoma, kuhakikisha linakomesha matukio ya ujambazi mkoani humo. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.


Na Felix Mwagara, MOHA-Kibondo

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola ametoa wiki mbili kwa Jeshi Polisi Mkoa wa Kigoma, kuhakikisha linakomesha matukio ya ujambazi yaliyokithiri katika Wilaya ya Kibondo pamoja na sehemu zingine mkoani humo.

Lugola aliongeza kua, katika kupambana na majambazi hao ambao wanasumbua wananchi wilaya hiyo ya Kibondo na kukosa amani katika maeneo yao, polisi ifanye operesheni maalumu kuwatia mbaroni watuhumiwa hao. Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Community Centre mjini Kibondo, leo, Lugola alisema katika operesheni hiyo pia itambatana na utoaji onyo kwa watu wasio waaminifu wanaowahifadhi raia wa kigeni ambao wengi wao ni wahalifu. 

‘’Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, natoa wiki mbili tu, kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya fanyeni operesheni ya kuwasaka majambazi hawa usiku na mchana mpaka jambazi wa mwisho awe amekamatwa,’’ alisema Lugola.

Lugola alisema haiwezekani tukasalimu amri kwa majambazi, haiwezekani kunyoosha mikono kwa jambazi waliopo katika maeneo mbalimbali wa wilaya hiyo pamoja na mkoa kwa ujumla.Waziri Lugola pia aliwataka wananchi wilayani humo kutoa taarifa polisi za wahalifu hao ili kuwezesha operesheni hiyo ifanikiwe zaidi na wananchi waweze kuishi kwa amani na kufanya shughuli zao za kuijenga nchi. 

Waziri huyo pia licha ya kusema anajua changamoto mbalimbali zinazowakibili polisi ikwemo ukosefu wa magari lakini aliwataka aliwataka wawahi katika matukio ya uhalifu yanapotokea, wanaweza kutumia pikipiki ili kuwahi kwa wakati katika matukio hayo. 

Waziri Lugola yupo katika ziara ya kikazi Mkoa wa Kigoma ambapo anatembelea Wilaya zote mkoani humo kwa kufanya kikao na watumishi walio chini ya wizara yake pamoja na kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwa ajili ya kusikiliza kero zao pamoja na kuzitatua.

No comments: