Wednesday, August 1, 2018

UPANDE WA MASHITAKA WAIOMBA MAHAKAMA KUSIMAMISHA USHAHIDI ULIOTOLEWA NA KATIBU MKUU TFF

Na Karama Kenyunko,Globu ya jamii

UPANDE wa mashtaka katika kesi ya kugushi na utakatishaji wa fedha inayomkabili aliyekuwa Rais wa TFF Jamal Malinzi na wenzake wameiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusimamisha ushahidi uliotolewa na Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau ili waweze kumuita mtaalam wa Sayansi ya Tehama kutoa nyaraka za email alizozitoa katika kompyuta na kuchapisha(print).

Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru), Leornad Swai ameeleza hayo leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa Kidao.Swai amedai kesi hiyo ilipangwa kuendelea kusikilizwa, lakini imewapasa kumtumia Mtaalam wa Sayansi ya Tehama kwa kuwa yeye ndiyo aliyeta email katika kompyuta, kuichambua na kuichapisha (Print).

Na kuongeza kuwa wamefanya tafiti katika ushahidi wa vielelezo vya kielektloniki na kwamba ili kujenga msingi wa ushahidi wanaoutoa kutokana na maelekezo ya sheria ni vema wakasimamisha kwanza ushahidi uliopo ili mtu huyo aweze kutoa hizo nyaraka.Amedai kuwa, mtu huyo anauwezo wa kuitoa mahakamani kama sehemu ya kielelezo cha ushahidi na mashahidi wengine kuielezea.

Kwa mantiki hiyo Swai ameiomba Mahakama kusimamisha ushahidi wa Kidau aliyekuwa anaendelea kutoa ushahidi ambapo leo alitakiwa kuhojiwa na mawakili wa upande wa utetezi.Wakili wa Utetezi Richard Rweyongeza hakuwa na pingamizi na hayo na aliomba wapewe muda wa Katibu wa kusikilizwa.Hakimu Mashauri ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 14 na 15, mwaka huu ambapo itaendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.

Kidau wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo alidai katika kikao cha kamati ya utendaji ya TFF cha Juni 5 mwaka 2016 suala la kubadilisha mtia saini halikuwa moja ya agenda.Pia Kidau aliorodhesha mahakamani hapo tofauti zilizoko katika muhtasari wa kikao cha kamati hiyo ya utendaji ya TFF na hati ya kubadilisha watia saini iliyopelekwa katika benki ya Stanbic iliyotiwa saini na aliokuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi na Katibu Mkuu, Celestine Mwesigwa.

Hata hivyo baada ya ushahidi wake mrefu, upande wa utetezi walitaka kuwasilisha pingamizi kupinga shahidi huyo kutoa nakala ya email ya majadiliano ya kumkataa Nsiande.Mbali na Malinzi washitakiwa wengine kwenye kesi hiyo ni Mwesigwa, aliyekuwa mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, Karani Flora Rauya na Miriam Zayumba ambapo wanakabiliwa na mashitaka 30 yakiwemo ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na utakatishaji fedha.

Kesi hiyo sasa itaendelea kusikilizwa siku mbili mfululizo, Agosti 14 na 15 mwaka huu.

No comments: