Wednesday, July 25, 2018

WADAU WA ELIMU WAKIRI KAMBI ZA KITAALUMA ZACHANGIA KUIFIKISHA SIMIYU KUMI BORA MATOKEO KIDATO CHA SITA 2018

Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ( wa pili kulia) akifungua kikao cha Tathmini ya Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2016 na pongezi kwa walimu waliofanikisha wanafunzi kupata alama A na B, ambacho kimefanyika Mjini Bariadi Julai 24, 2018.

Na Stella Kalinga, Simiyu

Wadau wa Elimu mkoani Simiyu wamekiri kuwa kambi za kitaaluma zimekuwa na mchango mkubwa katika kuuwezesha mkoani huo kushika nafasi ya kumi Kitaifa katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita  mwaka 2018, kutoka nafasi ya 26 mwaka 2017.

Hayo yamebainishwa katika kikao cha tathmini ya Matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mwaka 2018 kilichofanyika Julai 24, Mjini Bariadi, ambapo pia walimu wa Kidato cha Sita waliowezesha wanafunzi kufaulu kwa alama A na B katika masomo yao wamepongezwa na kupewa zawadi ya fedha taslimu na vyeti.

Afisa Taaluma Mkoa wa Simiyu, Mwl. Onesmo Simime akitoa taarifa ya matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mwaka 2018, katika kikao cha tathmini ya Matokeo hayo kilichofanyika Julai 24, Mjini Bariadi.

Kikao hiki  kimewashirikisha  viongozi na Watendaji wa Serikali ngazi ya Mkoa na Wilaya, Wakuu wa Shule na walimu wa shule za Sekondari za kidato cha tano na sita, wadhibiti ubora, Maafisa Elimu Wilaya na Kata, Wenyeviti wa Bodi za Shule, Viongozi wa Dini, Viongozi wa Chama cha Walimu na wadau wengine.

Baadhi ya wadau waliochangia katika tathimini hiyo wamempongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka kwa kuanzisha wazo la kuwa kambi za kitaaluma ambazo zimeleta mafanikio makubwa na kutoa maoni ya namna ya kuboresha na kuzifanya kambi hizi kuwa mkakati endelevu katika kuinua ubora wa elimu mkoani Simiyu.

“Nampongeza sana mkuu wetu wa Mkoa kuja na wazo hili la kuwa na kambi za Kitaaluma na Mkuu wa Mkoa amesema ni agenda ya kudumu katika mkoa , kama walimu, wazazi, wanafunzi, sisi viongozi na wadau wengine wa elimu katika Mkoa wetu tukiendelea kushirikiana, kambi hizi zitabadilisha mfumo wa elimu na kuufanya mkoa ung’are katika sekta ya elimu” Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dkt. Seif Shekalaghe.
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Mhe. Festo Kiswaga akichangia hoja katika kikao cha Tathmini ya Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2016 na pongezi kwa walimu waliofanikisha wanafunzi kupata alama A na B mkoani Simiyu, ambacho kimefanyika Mjini Bariadi Julai 24, 2018.

“Kambi za Kitaaluma zimechangia kuufikisha mkoa kwenye nafasi ya 10 Kitaifa lakini nashauri iundwe kamati ya ndogo ya Maafisa Taaluma kutathmini mazuri na changamoto za kambi za kitaaluma ili tuweze kuboresha zaidi na kuufanya mkoa kufanya vizuri zaidi” Mwl.Baraka Owawa Katibu Chama cha Walimu Wilaya ya Bariadi.

Nao viongozi wa madhehebu ya dini walioshiriki katika kikao  hicho cha tathmini wamesema wanaunga mkono juhudi za Serikali katika maendeleo ya elimu na wakaahidi kushirikiana na Serikali kwa kuwa hata vitabu vya dini navyo vinahimiza kupenda na kuthamini Elimu.

Afisa Taaluma wa Mkoa wa Simiyu, Mwl. Onesmo Simime akitoa tathmini ya matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mwaka 2018 amesema idadi ya wanafunzi waliopata daraja la I imeongezeka kutoka wanafunzi 43 mwaka 2017 na kufikia 119, daraja la II imeongezeka kutoka 304 mwaka 2017 hadi 451, daraja III toka 325  mwaka 2017 hadi 381.
Katibu wa Chama cha Walimu( CWT) Mkoa wa Simiyu, Mwl. Said Mselem akichangia hoja katika kikao cha Tathmini ya Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2016 na pongezi kwa walimu waliofanikisha wanafunzi kupata alama A na B mkoani humo, ambacho kimefanyika Mjini Bariadi Julai 24, 2018.

Aidha, amesema idadi ya wanafunzi waliopata daraja sifuri imepungua kutoka kutoka wanafunzi 29 mwaka 2017 hadi wanafunzi 14 mwaka 2018 ambapo amebainisha kuwa shule sita kati ya 11 mkoani humo zimefanikiwa kuondoa daraja sifuri mwaka 2018.

Amesema pamoja na kambi za Kitaaluma mkoa uliweka mikakati ambayo pia imechangia kuongeza ufaulu kuutoa kwenye nafasi ya 26 mwaka 2017  hadi 10 Kitaifa mwaka 2018, ambayo ni kuhakikisha walimu wanafundisha vipindi vyote na kufidia vilivyopotea na kufanya mtihani wa utimilifu (Mock) wa Mkoa na kanda uliowasaidia walimu kubaini mada zenye changamoto na kufanya mapitiao ya mada hizo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Anthony Mtaka  amewapongeza walimu,wazazi wanafunzi  na wadau wote wa elimu waliofanikisha mkoa kufanya vizuri katika Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mwaka 2018, huku akisisitiza kuendelea kuweka mikakati ya kuboresha uendeshaji wa kambi za kitaaluma ili waweze kufikia lengo walilojiwekea la kufikia ‘single digit’ nafasi ya 1-9.
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani akimkabidhi cheti cha pongezi (Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka) Mwl. Makame S. Makame kutoka Shule ya Sekondari ya Bariadi kwa kuwezesha wanafunzi wa kidato cha Sita mwaka 2018 kufanya vizuri katika somo la Kiswahili, baada ya kikao cha tathmini ya Matokeo hayo kilichofanyika Julai 24, Mjini Bariadi.

Katika kikao hicho pia Mtaka ameagiza kuwa muda wa  wanafunzi wa madarasa ya mtihani katika Shule za Sekondari za Serikali(Kidato cha nne na cha sita)kuzimiwa taa utakuwa saa sita usiku siyo saa nne usiku, hivyo akiwataka walimu kuweka utaratibu wa viongozi wa wanafunzi kuendelea na ratiba kwa niaba yao baada ya ratiba ya walimu inayoishia saa nne usiku.

Wanafunzi wa kidato cha sita mwaka 2018 walikaa katika kambi za Kitaaluma kwa muda wa siku 10 mwezi Aprili, aidha wanafunzi wa Kidato cha nne na Darsa la saba wa mwaka 2018 waliwekwa katika kambi za kitaaluma mwezi Juni kwa siku 21 kwa ajili ya kujiandaa na mitihani yao ya Taifa.
Mchungaji wa Kanisa la AICT Bariadi, Amosi Ndaki akichangia hoja katika kikao cha Tathmini ya Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2016 na pongezi kwa walimu waliofanikisha wanafunzi kupata alama A na B mkoani Simiyu, ambacho kimefanyika Mjini Bariadi Julai 24, 2018.
Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Dkt. Joseph Chilongani akimkabidhi cheti cha pongezi (Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka) Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwandoya wilayani Meatu Mwl. Donald Maduhu kwa shule hiyo kushika nafasi ya kwanza Kimkoa katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita mwaka 2018 , baada ya kikao cha tathmini ya Matokeo hayo kilichofanyika Julai 24, Mjini Bariadi.
Baadhi ya wadau wa elimu mkoa wa Simiyu, wakimsikiliza Mkuu wa mkoa huo, Mhe. Anthony Mtaka (hayupo pichani) wakati wa kikao cha Tathmini ya Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2016 na pongezi kwa walimu waliofanikisha wanafunzi kupata alama A na B mkoani humo, ambacho kimefanyika Mjini Bariadi Julai 24, 2018.
Baadhi ya Wenyeviti wa Kamati za Elimu, Afya na Maji za Halmashauri za Mkoa wa Simiyu wakifuatilia kikao cha Tathmini ya Matokeo ya Mtihani wa Kidato cha Sita mwaka 2016 na pongezi kwa walimu waliofanikisha wanafunzi kupata alama A na B mkoani humo, ambacho kimefanyika Mjini Bariadi Julai 24, 2018.

No comments: