Tuesday, July 10, 2018

TUMEANZA UTEKELEZAJI WA AGIZO LA WAZIRI MKUU KWA VITENDO-RC MASENZA

Na Francis Godwin Michuzi Blog, Iringa 

MKUU wa mkoa (RC) wa Iringa Amina Masenza amesema kuwa mkoa wake umeanza utekelezaji wa agizo la waziri mkuu Kasimu Majaliwa la kutaka wanaume kupimwa virusi vya UKIMWI ili kupunguza kasi ya maambukizi ya  VVU nchini.

Akizungumza leo katika ukumbi wa siasa ni kilimo mara baada ya kuwaongoza wadau wa maendeleo mkoani Iringa walioshiriki kikao cha mikakati ya utekelezaji wa agizo la waziri mkuu kupima VVU ,Masenza alisema kuwa zoezi la upimaji wa VVU kwa wanaume mkoani Iringa litasaidia kuwatambua wale ambao wameambukizwa na kuanzishiwa dawa za ARVs huku wale ambao hawajaathirika kujikinga na VVU.

Alisema kuwa michango ya wajumbe wa kikao hicho iliyotolewa ya kutaka wanaume kuhamasishwa kupima VVU kwa hiari majumbani kwao ni michango ambayo itasaidia kufikia malengo ya mapambano dhidi ya UKIMWI iwapo wanaume wote mkoani hapa wataonyesha ushirikiano katika zoezi hilo pindi litakapo anza .

Alisema kuwa taarifa za mganga mkuu wa mkoa wa Iringa zinaonyesha tatizo la UKIMWI bado kubwa ndani ya mkoa na kuwa pamoja na ukubwa wa tatizo ila bado kuna wadau wengi wa mapambano ya UKIMWI .

Kuwa kampeni ya kitaifa ya upimaji wa VVU na utoaji wa dawa za kupumbaza VVU iliyozinduliwa na Juni 19 mjini Dodoma na waziri mkuu imekwenda sanjari inajumuisha na usemi usemao Furaha yangu pima jitambue hivyo kampeni hiyo itanaza kwa wanaume na baadae makundi mengine katika jamii .

Kuwa makundi hayo ni pamoja na mabinti wa miaka kuanzia 15 hadi 21 ,wanawake wajawazito na wengine wote na kuwa njia pekee ya kufanikisha kampeni hiyo ni wananchi wote kujitokeza kupima VVU .

Alisema kuwa hali ya VVU ni mbaya nchini kwani kitaifa asilimia 52.2 ya watu wanaoishi na VVU hawajui kama wanaishi na VVU na kuwa hali hiyo inachangiwa na wanaume ambao kiwango chao cha upimaji ipo chini sana kwa kuwa na asiimia 45.3 ukilinganisha na asilimia 55.9 ya wanawake .

Hivyo alisema umefika wakati kwa kampeni za upimaji kuelekezwa kwa wanaume na vijana wote na kuwa hakuna sababu ya wanaume kuendekeza mfumo dume hata katika upimaji wa VVU .

Mkuu huyo wa mkoa aliwataka wanawake kuwahamasisha waume zao kujitokeza kwa wingi katika kampeni ya upimaji wa VVU kwani wanaume ni kichwa cha familia lazima kuonyesha ushiriki mkubwa wa kwenda kupima VVU .

" Kwa heshima kubwa na unyenyekevu usio na kiwango nawaombeni sana wanaume wote vijana wote na akina mama nendeni mkapime VVU ili kuanzishiwa dawa kwa wale ambao watakutwa wameathirika furaha yako ipo kwenye kupima ukijitambua utaishi kwa raha lakini mtambue ninyi wakina baba ndio ambao mnatuchanganya hamuachi kuwa na nyumba ndogo "

Wanawake tunaomba mseme nao wanaume kwa upore na kuwashauri kuitikia wito wa kupima VVU kwa siri majumbani kwao ama kujitokeza katika vituo vya afya na katika hospitali zetu .

Alisema kuwa mkoa wa Iringa ni wa pili kwa maambukizi ya VVU ukiongozwa na mkoa wa Njombe ambao unaongoza kitaifa na kuwa si sifa nzuri kwa mkoa kuongoza kwa maambukizi ya VVU na hivyo kusudio la mkoa ni kuona wanashuka katika kasi hiyo na kufikia asilimia 0.03.

Hata hivyo alisema kuwa uzinduzi wa kitaifa wa kampeni ya Furaha yangu umemethibitisha kuwa serikali yetu ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt John Magufuli imelenga kuona wananchi wake wanakuwa na afya njema na kufanikisha azima yake ya kuelekea Tanzania ya uchumi wa viwanda na yenye watu wenye afya njema.

Kwa upande wake washiriki wa kikao hicho waliunga mkono kampeni hizo na kuwa wapo tayari kushiriki kuelimisha jamii na kuwa mfano kwa kujitokeza kupima.Mbunge mstaafu wa viti maalum mkoa wa Iringa (CCM) Lediana Mng'ong'o alisema kuwa suala la maambukizi ya VVU mkoani Iringa ni kubwa na imekuwa ikichangiwa na madereva wa malori na wanawake wanaofanya kazi ya kujiuza mitaani .

Pia alisema wapo baadhi ya wanaume wamekuwa wakikwepa kwenda kupima VVU na wakiishia kuwatuma wake zao kupima wakijua kuwa akipima mwanamke na kuonekana salama na yeye atakuwa salama .

Huku mkuu wa wilaya ya Mufindi Jamhuri Wiliam alisema kuwa zipo dhana potofu kuwa wilaya ya Mufindi imekuwa na maambukizi makubwa ya VVU kutokana na kuwa na uchumi mkubwa jambo ambalo si kweli na kuwa ulaya ina uchumi mkubwa mbona kasi ya maambukizi ya VVU ipo chini.
Mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza akiongoza kupima VVU katika kikao cha mikakatiya kuanzakampeni za kupima UKIMWI kwa wanaume 
Viongozi wa mkoa wa Iringa wakiwemo wakuu wa wilaya ya Mufindi na kilolo wakionyesha karatasi baada ya kupima VVU 
Washiriki wa kikao cha kuweka mikakati ya zoezi la upimaji UKIMWI wanaume wakiwa katika kikao hicho.

No comments: