Thursday, July 26, 2018

KUPATWA KAMILIFU NA KUREFU ZAIDI KWA MWEZI PAMOJA NA MPANGILIO WA SAYARI ANGANI

Dr. N. T. Jiwaji
ntjiwaji at yahoo dot com

Usiku wa Ijumaa ya tarehe 27 Julai 1016 siyo wa kukosa kuangangalia angani.  Usiku huo, Mwezi mpevu utafunikwa kabisa na kivuli cha Dunia na kusababisha kupatwa kamilifu na kuonekana wa rangi nyekundu.  Kupatwa kunatokea wakati Dunia na Mwezi zinakuwa katika mstari mnyoofu, Dunia ikiwa kati ya Jua na Mwezi.  Kupatwa huku kutukuwa wa kukolea sana na wa muda mrefu zaidi kwa karne hii.

Mwezi utafunikwa kwa muda mrefu zaidi kwa vile utakuwa na umbali mkubwa zaidi kutoka Duniani hivyo utapita ndani ya sehemu pana zaidi ya kivuli cha Dunia, na kuchukua muda mrefu zaidi kuvuka kivuli hicho. Safari hii Mwezi utabaki umepatwa kwa muda wa saa moja na dakika arobaini na tatu ambayo ni karibu masaa mawili hivi.  Kupatwa kurefu kiasi hiki ni nadra sana kwa vilie kawaida ni dakika mia tu, kwa wastani.  Kupatwa kurefu zaidi ya hii hakutatokea tena hadi baada ya miaka 105 ijayo siku ya tarehe 9 Juni, 2123.

Kupatwa kwa Mwezi kunaweza kuangaliwa kwa macho pekee bila madhara yoyote kwa vile tunafahamu kuwa mwanga wa Mwezi kawaida hautudhuru, na siku ya kupatwa mwanga unafifia hata zaidi baada ya kuzuiliwa na kivuli cha Dunia. Kupatwa kutaanza saa tatu na dakika ishirini na nne (3:24usiku) kwa kupatwa kiasi na kuanza kumegwa kingo ya mashariki ya Mwezi kwa kufunikwa na giza nyeusi ambayo itafunika Mwezi polepole hadi kufunika wote saa nne na nusu (4:30usiku), wakati ambapo Mwezi utakuwa umepatwa kamilifu na utageuka kuwa na rangi nyekundu. Hali hii ya Mwezi kuwa mwekundu wakati wa kupatwa kamilifu kutaendelea hadi saa sita na dakia kumi na tatu (6:13usiku) ambapo kupatwa kamilifu kutamalizika. Baada ya hapo kingo ya mshariku ya Mwezi itaanza kuchomoza kutoka katika kivuli na kuanza kuonesha uweupe utaongezeka polepole hadi saa saba na dakika kumi na tisa (7:19usiku) ambapo Mwezi utakuwa umeachwa na giza nyeusi, na ndio mwisho wa kukpatwa kiasi.
Pamoja na kuuona Mwezi ukiwa umepatwa kwa giza nyeusi, kuna sehemu ya kupatwa ambayo hatuwezi kutambua kwa urahisi.  Wakati huo Mwezi unakuwa umefunikwa na kivuli chepsi cha Dunia. Hali hii ya kupatwa kwepesi itaanza saa mbili na dakika kumi na nne (2:14usiku) hadi saa tatu na dakika ishirini na nne (3:24usiku) ambayo ni mwanzo wa kupatwa kiasi na kuanza kuonesha giza ukingoni mwa Mwezi.  Mwishoni tena kuna kupatwa kwepesi kuanzia mwisho wa kupatwa kisai saa saba na dakika kumi na tisa (07:19usiku) hadi saa nane na dakika ishirini na nane (08:28usiku) ambayo ndiyo mwisho kabisa wa tukio hili la kupatwa kwa Mwezi.
Ingawa Mwezi wote unamezwa ndani ya kivuli cha Dunia wakati wa  kupatwa kamilifu, Mwezi haupotei moja kwa moja kwa vile mwanga kidogo hupenya ndani ya kivuli cheusi baada ya kupindwa na angahewa ya Dunia.  Mwanga huu huwa ni wa rangi nyekundu na kusababisha Mwezi kuonekana kuwa wa rangi nyekundu muda wote ambao umepatwa kamilifu kuanzia saa 04:30usiku hadi saa 06:13usiku.  Mandhari hii ya uwekundu wa Mwezi si wa kukosa kuuona kwa sababu kukolea kiasi hiki cha kupatwa kamilifu hakutatokea kwa miaka saba ijayo hadi Septemba 7, 2025 

Kiasi cha uwekundu wa Mwezi uliopatwa kamilifu hutegemea kiasi cha uchafuzi wa angahewa ya Dunia yetu.  Angahewa ikiwa ni safi tutaona Mwezi ukin’gaa kwa mwanga mwekundu, lakini hali ya angahewa kama imechafuka, uwekundu utafifia kwa kiasi cha uchafuzi wa angahewa.  Kuna kipimo cha hali ya rangi ya Mwezi unaitwa Danjon unaoanza 0 kama Mwezi hautakuwa na mn’gao, hadi 4 kama unan’gaa sana kwa rangi nyekundu ikiwa angahewa ni safi kabisa. Siku ya Ijumaa tunategemea Mwezi un’gae vizuri kwa uwekundu, lakini ujionee mwenyewe hali halisi ya rangi yake na kupima kiasi cha uchfuzi wa angahewa yetu.  
Siku ya Ijumaa Julai 27 Mwezi mpevu utachomoza katika upeo wa mashariki Jua linazama upeo wa magharibi wakati wa machweo.  Hii ina maanisha Mwezi unaangaliana na Jua na kusababisha Mwezi mpevu wa mduara kamili.  Pamoja na Mwezi kuna sayari nne zinaoonekana katika anga la jioni.  Jirani kabisa na Mwezi utaona nyota nyekundu kali inachomoza wakati wa machweo.  Hiyo ni sayari ya Mirihi (Mars) ambayo ipo jirani zaidi na Dunia na inaangaliana moja kwa moja na Jua na kusababisha in’gae vikali sana. Juu zaidi katika anga ya mashariki utaona sayari ya Zohali (Saturn) ambayo ingawa hain’gai mno utaweza kuitambua kutokana na kun’gaa moja kwa moja badala ya kumeremeta kama nyota za jirani yake.  Utosini utaona nyota inayon’gaa sana.  Hiyo ni Mstarii (Jupiter) na upande wa magharibi ni nyota inyon’gaa mno kwa unjano, ambayo ni Zuhura (Venus).  

Utaona kuwa sayari zote pamoja na Mwezi unatengeneza mstari mmoja angani kutoka mashariki hadi magharibi.  Sayari huwa kila mara uktaziona katika eneo hili tu la mstari unaotoka mashariki ya anga hadi magharibi ya anga.  Hii inasababishwa na Mfumo wetu wa Jua umeundwa katika bapa nyembamba, na kutoka Duniani tunaziona sayari hizo angani tukiwa tumeelekeza macho yetu katika bapa ya Mfumo wetu wa Jua.

Kama unatumia darubini kuangalia sayari ya Mshtarii (Jupiter) utaona sayari kama mduara na pamoja na hiyo utaona nukta nne zikin’gaa kama nyota ambazo kwa kweli ni miezi ya Mshtarii.  Miezi hiyo imepangika katika mstari mmoja, sawa kama tunavyoona sayari katika anga yetu.  Hii ina maanisha miezi hiyo inaizunguka Mshtarii kama vile sayari zinavyozunguka Jua katika bapa moja.  Sayari ambayo siyo kukosa kuangalia kwa darubini ni Zohali (Saturn) kwa vile utaweza kuona ajabu ya pete inayozunguka Zohali.  Cha ajabu kingine ni kuangalia Zuhura (Venus) kwa darubini na utaona kuwa ni nusu duara wakati huu.  Katika siku zijazo hadi Septemba Zuhura itaonekana kama hilali kama vile hilali ya Mwezi wetu. Yote haya yanasababishwa na mzingo wa Zuhura upo ndani ya mzingo wa Dunia na husababisha Zuhura kuwa na awamu kama vile za Mwezi.  Sayari ya Mirihi huonekana kama duara kamili yenye rangi nyekundu.  

Chukua nafasi ya kuwa nje ukiwa unaangalia anga wakati wa kupatwa kwa Mwezi kutambua nyota nyingi zilizopangwa katika mkanda mwembamba. Hautaona nyota nyingi mbali na mkanda huu wa nyota nyingi ambayo inajulikana kama Njia Nyeupe. Mkusanyiko wa nyota nyingi sana katika mkanda mmoja unatokana na galaksi yetu kuwa na muundo wa bapa na sisi tukiwa tuanangalia nyota nyingi katika bapa ya galaksi yetu. Mkanda huu wa nyota hauoneshi nyota nyingi ukiwa katika miji mikubwa kutokana na uchfuzi wa anga na mwanga mkali unaotoka ardhini.  Kwa upande wa makundi ya nyota utaweza kutambua kundi la Msalaba wa Kusini na pia kundi la Nge ambayo ina umbo kama nge.
Mapendekezo kwa waalimu na wazazi

Walimu wanaweza kuchukua nafasi hii kuwaandaa wanafunzi kutazama kupatwa kwa Mwezi nyumbani kwao pamoja na wazazi na ndugu na jamaa, na baadaye kujadiliana nao kuhusu walichoona.

Hapa anaweza kutumia vitabu vya Maarifa ya Jamii darasa la sita ambako kuna habari za kupatwa kwa Mwezi katika somo kuhusu Mfumo wa Jua. Inafaa kuwahi kufundisha habari hizi  hata kama somo kwa jumla halikuanzishwa bado.

Hata kwa madarasa ya chini mwalimu anaweza kutumia matini husika.

Wanafunzi wa Sekondari wanaweza kutayarishwa kwa tukio hili kwa kukumbusha walichojifunza katika madarasa msingi na kuunganisha na matini ya somo la Jiografia ya Kidato cha Kwanza inayohusu Mfumo wa Juan pamoja na mada ya kupatwa kwa Mwezi na Jua.

Wanafunzi wa Kidato cha Nne wanaosoma Fizikia katika mada ya Astronomia pia watafaidi sana kufuatilia tukio hili kama elimu nyongeza kwa vile ni muhimu na ya kusisimua, ingawa halipo katika mtala au katika vitabu vyayo. Hii inawahusu pia wanafunzi wa sayansi wote katika Sekondari na Vidato vya Tano na Sita pamoja na wanafunzi wa sayansi vyuoni.

Kwa kila namna mwalimu atachora ubaoni nafasi za Jua, Dunia na Mwezi pamoja na aina za kivuli na kuwaeleza watakachoona wakati Mwezi umepatwa.

Wanafunzi wanaweza kuandika wanachoona wakati wa tukio, wakijibu maswali kama:

- Je waliweza kuona Mwezi?
- Mwezi ulikuwa na umbo gani?
- Je waliona mabadiliko gani katika uangavu wa Mwezi, tena saa ngapi?
- Je waliona sayari nyekundu jirani na Mwezi?
- Je waliona na kutambua sayari ya Zohali kwa kutambua kuwa haimeremeti?
- Je waliona Mshtarii utosini?
- Je waliona Zuhura ikin’gaa kwa unjano?
- Je waliona nyota nyingi zimejipanga kama mkanda?
- Je waliweza kutambua kundi la Msalaba wa Kusini?
- Je waliweza kutambua kundi lenye umbo la nge?
- Giza (au kupungua kwa uangavu) waliona kwenye sehemu gani za Mwezi?
- Wachore sehemu angavu na zenye giza kwenye uso wa Mwezi mpevu.
- Waandike kwa maneno yao jinsi wanavyoweza kueleza walichoona.

Baad ya hapo siku ya kwenda shule, watumie nafasi ya kusikia taarifa za wanafunzi, kujibu maswali na kutoa maelezo yanayohitajika.

No comments: