Sunday, July 8, 2018

CUF WATANGAZA KUTOSHIRIKI UCHAGUZI MDOGO WA MARUDIO KATIKA KATA 79,MAJIMBO MAWILI

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii

CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema hakitashiriki Uchaguzi mdogo wa marudio katika Kata 79 na majimbo mawili ambao umetengazwa kufanyika Agosti 12 mwaka huu. 

Taarifa ya Naibu Mkurugenzi wa habari, Uenezi na Uhusiano na Umma Mbarala Maharagande ametoa taarifa ya kutoshiriki kwenye uchaguzi kwa vyombo vya habari na kufafanua uamuzi huo umetokana na Kamati ya Utendaji baada ya kufanya uchambuzi na tathimini ya kina kuhusu tangazo la kufanyika uchaguzi huo. 

Maragande ambaye yeye anatoka CUF ya upande wa Katibu Mkuu wa chama hicho Maalim Seif Ahmad amesema sababu za msingi za kutoshiriki katika uchaguzi huo ni nyingi moja wapo ikiwa ni mgawanyiko wa uongozi Katika uchaguzi huo uliojitokeza kutokana na mgogoro aliodai umepandakizwa na Profesa Ibrahim Lipumba na Washiriki wake

Hivyo amesema CUF unaona ni ishara kwa sasa kuelekeza nguvu na rasilimali zake chache zilizopo katika kushughulika na kupata ufumbuzi wa mgogoro uliopo. Ameongeza kuwa CUF inatoa mwito kwa vyama rafiki vyote katika UKAWA kukaa pamoja kufikia muafaka na maridhiano na kusimamisha wagombea bora, imara, na madhubuti kugombea nafasi hizo zote.

"CUF inatoa mwito kwa viongozi na wanachama wake wote katika maeneo yote ya marejeo ya uchaguzi kwa Tanzania Bara kushirikiana bega kwa bega na kuunganisha nguvu za pamoja na vyama rafiki vya UKAWA katika uchaguzi huu ili kuishinda CCM,"amesema. 

Maharagande amesema katikankata 79 zilizotangazwa, CUF imepoteza Kata 4 ilizokuwa inaziongoza kwa madiwani wake ambao waliamua kwenda CCM. Kata mbili zipo manispaa ya Jiji la Tanga Mjini na Kata moja Mtwara Vijijini na Diwani mmoja Kufariki (Wilaya ya Kwimba). 

Kutokana na vigezo vya kitaalamu na kitakwimu na ramani ya maeneo utakapofanyika uchaguzi huo wa marudio CUF ingeweza kushiriki kikamilifu katika Kata za mkakati 11 pekee.

Na kwamba Kata zingine CUF ingelazimika kuunganisha nguvu na vyama vingine katika UKAWA."Huu ndio msimamo wa CUF unaozingatia maslahi mapema ya chama unaopaswa kuheshimiwa na kila mwanaCUF wa ukweli,"amesema. 

Kuhusu uchaguzi Jimbo la Jang'ombe visiwani zanzibar unatarajia kufanyika Oktoba 17 Maharagande amesema CUF ilishaweka msimamo wake hakitashiriki uchaguzi huo ambapo ametoa sababu mbalimbali ambazo wanaamini ndio msimamo wao. 

Time ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)imetangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo katika Jimbo la Buyungu, mkoani Kigoma ambalo lilikuwa linaongozwa na Mbunge wa Chadema aliyefariki dunia hivi karibuni na kwenye Kata 79 za Tanzania Bara.

Hivyo uchaguzi huo mdogo utafanyika ndani ya halmashauri 43 zilizopo kwenye mikoa 24 ya Tanzania Bara.Mikoa hiyo ni pamoja na, Kigoma, Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kagera, Katavi, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mara, Mbeya, Mtwara, Morogoro, Mwanza, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida, Songwe, Tabora na Tanga.

Kwa upande wa Halmashauri zitakazokuwa na Uchaguzi ni Moshi, Ruangwa, Mbulu, Hanang, Babati, Serengeti, Tarime, Kyela, Mtwara, Newala, Kilombero, Kilosa, Kwimba, Makete, Wanging’ombe na Kalambo.

Pia Songea, Msalala, Meatu, Singida, Songwe, Tunduma, Tabora, Nzega, Urambo, Tanga, Karatu, Longido, Arusha, Ngorongoro, Monduli, Meru, Ubungo, Kondoa, Mpwapwa, Chamwino, Iringa, Kyerwa, Misenyi, Muleba, Nsimbo, Kasulu na Same.

No comments: