Wednesday, June 20, 2018

WAZIRI WA MIFUGO AOMBA RADHI BUNGENI...SPIKA ATOA MSIMAMO

*Ni kwa kitendo cha Wizara kuingia mgahawa wa Bunge kupima samaki
*Amwambia Waziri Mkuu kilichofanyika si uungwana, akubali kusamehe yaishe

Na Said Mwishehe,Globu ya jamii

PAMOJA na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Luhaga Mpina kuliomba radhi Bunge kwa kitendo cha Wizara yake kuingia kwenye mgahawa wa Bunge bila kibali na kupima samaki waliopikwa kwa rula, Spika wa Bunge Job Ndugai amasema kitendo hicho ni udhalilishaji.

Juzi Waziri Mpina alitoa maagizo kwa watendaji wa Wizara yake kuingia kwenye Mgahawa wa Bunge na kisha kuingia jikoni kupima samaki ambao tayari walikuwa wamepikwa.Kitendo hicho kilisababisha wabunge kuchachama na kutoa hoja ili kujadili kitendo hicho.Mbunge Peter Serukamba ndio aliyeomba muongozo.

Hivyo leo Mpina akiwa bungeni mjini Dodoma ameomba radhi Bunge pamoja na Spika wa Bunge kwa kitendo hicho.Hata hivyo Spika Ndugai amemueleza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa kitendo hicho ni udhalilishaji na si sahihi."Tunamshukuru Waziri kutokana na maelezo ambayo ameyatoa lakini niseme tu kwa Waziri Mkuu tumesikitishwa na kilichotokea.

"Sisi si Bunge pekee duniani bali ni sehemu ya mabunge mengine ya jumuiya ya madola.Ikisikika kuna Waziri amefanya kitendo hiki bungeni ni kosa. "Hata kama kuna kosa la jinai ambalo limefanyika ndani ya Bunge ni vema Spika akajulishwa badala ya watu kuingia tu,"amesema Spika Ndugai.

Amefafanua kwa akili ya kawaida tu mtu anapokwenda kununua samaki zaidi ya kilo 100 , ananunua samaki kwa kilo na si kupima kwa futi."Halafu samaki mwenyewe kapikwa na ameshakuwa kitoweo...sasa hii sheria ya kupima vitoweoo inabidi kuiangalia vizuri. "Hivi kweli jamani mtu anatakiwa kufunga mlango ndio ale samaki?Kibaya zaidi wapimaji wenyewe hao wa wizarani wakati wanapima hakuwa hata na glovu ...

"Wanashika shika samaki.Tena hawakuwa peke yao wamealika na waandishi wa habari, wamejaa zaidi ya 20 jioni.Na baada ya hapo wakaanza kurusha kwenye mitandao ya kijamii."Ni kama mpango fulani hivi ulioandaliwa ili kulidhalilisha Bunge na ndicho kiachoonekana,"amesema Spika Ndugai huku akionesha kusikitishwa na kitendo hicho.

Hata hivyo baada ya kumaliza kuzungumza baadhi ya wabunge walitaka kusimama kwa ajili ya kuzungumzia suala hilo lakini Spika akwaaambia kuwa ni vema wakasamehe."Kwa kawaida ndugu zangu ukikasirishwa sana na jambo fulani unatakiwa kusamehe.Hivyo niwaombe wabunge tusamehe,"amesema Spika Ndugai.


WAZIRI ALIOMBA RADHI BUNGE

Awali Waziri Mpina alisimama bungeni kuzungumzia suala hilo ambapo amefafanua Juni 19 mwaka huu akiwa katika mgahawa wa Bunge aliona samaki aina ya Sato na akawatilia shaka.

Kutokana na shaka hiyo aliatoa maagizo kwa Katibu wa Wizara kuagiza watendaji wake kupima samaki hao ambao walionekana ni wachanga. "Baada ya kuona wale samaki nikaomba kujiridhisha na hivyo watendaji wetu walifika pale na kupima samaki hao na tukajiridhisha walikuwa wachanga.

"Walipomhoji mmiliki wa mgahawa huo Daniel Ramba alikiri samaki hao walikuwa ni wachanga.Hivyo alitozwa faini ya Sh.300,000 na wakalipa kupitia Benki ya NMB,"amesema Waziri Mpina.Ameongeza mmiliki huyo alinunua samaki kilo 100 katika duka ambalo lilikuwa eneo la Uhindini mjini Dodoma.Mmiliki wa duka hilo ni Samuel Kamon ambaye naye alitozwa faini ya Sh.200,000.

Waziri Mpina amekiri watumishi hao waliingia kwenye mgahawa wa Bunge na kisha kupima samaki hao ambao walikuwa wamepikwa."Kutokana na hali hiyo niombe radhi kwa Bunge kutokana na wizara yake kutofuata tararibu,"amesema Waziri Mpina.

No comments: