Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko, akitoa hotuba ya ufunguzi wa warsha ya madini, iliyotolewa na wataalam kutoka Australia; Juni 4 na 5 mwaka huu, jijini Dodoma.
Na Veronica Simba – Dodoma
Wataalam mbalimbali kutoka sekta ya madini nchini wameshiriki warsha
maalum iliyotolewa na wataalamu kutoka Australia, kwa lengo la kujifunza
uzoefu kutoka nchi hiyo ambayo imepiga hatua kubwa katika sekta husika.
Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko alifungua rasmi warsha hiyo ya siku
mbili, Juni 4 jijini Dodoma na kusema kuwa Tanzania inahitaji kujifunza
zaidi kutoka nchi zilizofanikiwa katika sekta ya madini kama Australia, ili
iweze kukuza zaidi mchango wake katika katika Pato la Taifa.
“Wenzetu Australia, sekta yao ya madini ina mchango mkubwa sana; zaidi
ya asilimia 40 kwenye Pato lao la Taifa. Kwa hiyo, tunakutana nao
kubadilishana uzoefu, ni namna gani wao wamefanya kuwezesha sekta
husika kuchangia kwa kiasi hicho kwenye Pato la Taifa.”
Aidha, Naibu Waziri alisema kuwa, suala muhimu ambalo Wizara ya Madini
inalisimamia ni kuhusu usimamizi wa rasilimali za madini.
Alisema kuwa, lengo jingine la warsha hiyo ni kujifunza Australia imefanya
nini katika kusimamia na kutatua migogoro kwenye sekta ya madini, ili
Tanzania itumie mbinu hizo kutatua migogoro iliyopo kwenye sekta husika.
Mtaalamu wa Madini kutoka Australia, Rick Rogerson, akiwasilisha mada katika warsha ya wataalam wa madini nchini (hawapo pichani), iliyofanyika Juni 4 na 5 mwaka huu, jijini Dodoma.
Biteko alitumia fursa hiyo kuiomba serikali ya Australia kuangalia
uwezekano wa kuendesha warsha husika kwa wachimbaji wadogo nchini ili
wapate maarifa ya namna bora ya usimamizi wa rasilimali za madini.
Akizungumzia mchango wa sekta ya madini kwenye uchumi wa viwanda,
Biteko alieleza kuwa, rasilimali za madini ni tegemeo kubwa katika kukuza
uchumi huo.
“Ndiyo maana mtaona kwamba tunayo miradi mikubwa ya makaa ya
mawe, ambayo inazalisha nishati ya umeme utakaotumika kwenye
viwanda vyetu. Kwa hiyo lazima tuisimamie vizuri,” alifafanua.
Aidha, aliongeza kwamba, Tanzania ina madini mengi ya teknolojia
yakiwemo ya Neobium yanayohitajika sana duniani kwa ajili ya viwanda.
Alitaja madini mengine muhimu kwa viwanda kuwa ni Graphite pamoja na
Marble, ambayo yote yanapatikana kwa wingi Tanzania.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi David
Mulabwa, alisema kuwa, warsha hiyo ni muhimu sana katika kuwaongezea
watumishi ujuzi na maarifa kwa ajili ya kukabiliana na changamoto za
kisekta.
Kutoka kushoto ni Kamishna wa Madini Tanzania, Mhandisi David Mulabwa; Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Tanzania, Prof Shukrani Manya wakijadiliana jambo, wakati wa ufunguzi rasmi wa warsha ya wataalam wa madini nchini, iliyotolewa na wataalam kutoka Australia; Juni 4 na 5 mwaka huu, jijini Dodoma.
“Kuna mambo ya mazingira, tozo na kodi mbalimbali katika sekta. Kwa
hiyo, jinsi watumishi wanavyokuwa na ujuzi na maarifa, tunaamini
watakuwa katika nafasi nzuri ya kufanya ya kufanya maamuzi ambayo
yatasaidia kuhakikisha kwamba rasilimali za nchi hii zinalinufaisha Taifa
ipasavyo.”
Awali, mmoja wa waratibu wa warsha hiyo, ambaye ni Afisa kutoka Ubalozi
wa Australia kutoka Ofisi ya Nairobi, Deanna Simpson, alieleza kuwa;
Serikali ya nchi yake imekuwa ikitoa warsha za aina hiyo katika nchi
mbalimbali za Afrika, zikiwemo Kenya, Madagascar, Ethiopia na Sudan.
Aidha, aliongeza kuwa, Australia Magharibi ina kampuni zaidi ya 100
zinazoendesha miradi mbalimbali ya madini zaidi ya 350 katika nchi za
Afrika takribani 30 ikiwemo Tanzania.
Warsha hiyo ya madini imehitimishwa Juni 5, mwaka huu.
Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (kushoto), akijadiliana jambo na
Mtaalamu wa Madini kutoka Australia, Rick Rogerson, muda mfupi baada
ya Naibu Waziri kufungua rasmi warsha ya wataalam wa madini nchini,
iliyotolewa na wataalam kutoka Australia; Juni 4 na 5 mwaka huu, jijini
Dodoma.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Tanzania, Prof Shukrani Manya (kulia),
akisalimiana na wataalamu wa madini kutoka Australia, Danielle Risbey na
Rick Rogerson, muda mfupi kabla ya kuanza kwa warsha ya wataalam wa
madini nchini, iliyotolewa na wataalam kutoka Australia; Juni 4 na 5 mwaka
huu, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Madini Doto Biteko (waliokaa-katikati), akiwa katika picha
ya pamoja na wataalamu mbalimbali wa madini nchini, walioshiriki warsha
maalum iliyotolewa na wataalamu kutoka Australia. Naibu Waziri alifungua
rasmi warsha hiyo ya siku mbili, Juni 4 mwaka huu jijini Dodoma.
Afisa Ubalozi wa Australia kutoka Ofisi ya Nairobi, Deanna Simpson
(kushoto), akizungumza, wakati wa ufunguzi wa warsha ya wataalam wa
madini nchini (kulia), iliyotolewa na wataalam kutoka Australia; Juni 4 na 5
mwaka huu, jijini Dodoma.
Wataalamu mbalimbali wa sekta ya madini nchini, wakifuatilia mada
mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa na wataalamu wa madini kutoka
Australia, katika warsha iliyofanyika Juni 4 na 5 mwaka huu jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment