Friday, June 29, 2018

Wanawake Milioni 2.6 Kunufaika na Mradi wa ‘50 Million Women Speak Project’

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.

Takribani wanawake milioni 2.6 wanategemea kunufaika na mradi ujulikanao kama 50 Million Women Speak Project’ unaolenga kuwawezesha wanawake kupata taarifa za kiuchumi kupitia mtandao wa mawasiliano.

Takwimu hizo zimetolewa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bw. Julius Mbilinyi alipokuwa akifungua kikao cha wadau wa Kitaifa wa masuala ya maendeleo ya wanawake nchini.

Bw. Mbilinyi amesema kuwa takwimu za Hali ya Afya na Demografia za mwaka 2015 zinaonesha asilimia 51 ya Watanzania ni wanawake ambao kati ya wanawake hao, asilimia 70 wanajihusisha na shughuli za kilimo na ujasiriamali hivyo mradi huo utatumika kusaidia kuimarisha shughuli zao.

“Mradi huu wa miaka mitatu unategemea kunufaisha wanawake kutoka nchi 30 za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi pamoja na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika ambazo kwa ujumla zinakadiriwa kuwa na wanawake milioni 500, kwa Tanzania mradi huu unategemea kunufaisha takriban wanawake milioni 2.6.” alisema Bw. Mbilinyi.

Bw. Mbilinyi ameongeza kuwa mradi huo una umuhimu kwa kuwa utawafikia wanawake hasa wa vijijini ili kuwawezesha kujiletea maendeleo jumuishi yanayoenda sawa na utekelezaji wa malengo endelevu ya Kimataifa, mpango wa miaka mitano ya maendeleo, Agenda ya Afrika Tuitakayo pamoja na Dira ya Taifa ya Maendeleo.

Vile vile mradi huo utawezesha wanawake kunufaika kwa kupata taarifa mbalimbali za kibiashara zikiwemo za upatikanaji wa mitaji, masoko na stadi za biashara kwa kutumia mitandao ya mawasiliano, vituo vya taarifa za wanawake, majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi pamoja na vikundi mlezi.

Akizungumzia mkutano huo, Bw. Mbilinyi amesema kuwa wamemua kufanya kikao cha wadau wa maendeleo ya wanawake takribani 50 ili kuwafahamisha kuhusu mradi huo, jinsi utakavyofanya kazi pamoja na kukusanya mawazo yao yatakayosaidia kuboresha utekelezaji wake nchini.

Kwa upande wake Msimamizi wa Mradi huo kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Wilson Muyenzi amesema kuwa mradi huo unategemewa kuongeza fursa za ajira kwa wanawake, kufahamu gharama za ubadilishaji fedha pamoja na kupanua masoko kwenye nchi mbalimbali zinazoshiriki katika mradi huo.

“Wanawake watakaotumia huduma za mradi huu wataweza kuongeza mapato yao kwa kiasi cha dola 50,000 hadi 100,000 kwa kipindi cha miaka mitatu ya utekelezaji wa mradi pamoja na kuongeza ajira kwa vijana wanawake kwa asilimia 10.” Alisema Bw. Muyenzi.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Bw. Julius Mbilinyi akifungua kikao cha wadau wa Kitaifa wa masuala ya maendeleo ya wanawake nchini kilichofanyika jijini Dodoma.Kutoka kushoto ni Mkurugenzi wa Sekta ya Jamii kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mary Makoffu na Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Vijana na Uwezeshaji Kiuchumi, Esther Riwa.
Msimamizi wa Mradi huo kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bw. Wilson Muyenzi akitoa mada katika kikao cha wadau wa Kitaifa wa masuala ya maendeleo ya wanawake nchini kilichofanyika jijini Dodoma.
Wadau wa masuala ya maendeleo ya wanawake nchini wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumaliza kikao cha kujadili kuhusu mradi ujulikanao kama 50 Million Women Speak Project’ unaolenga kuwawezesha wanawake kupata taarifa za kiuchumi kupitia mtandao wa mawasiliano kilichofanyika jijini Dodoma.

No comments: