Wednesday, June 20, 2018

TAARIFA KUHUSU KUHAMISHA SOKO LA KATENGELE - WILAYANI ILEJE

JIOGRAFIA/MAHALI LILIPO SOKO

Soko la Katengele linapatikana katika vilele vya milima yenye msitu ujulikanao kama Iyondo - Mswima wenye miti ya asili na ile ya kupandwa ukizungukwa na Kata za Kalembo, Sange, Ibaba, Ngulugulu na Kufule.
Pia soko hili hupitiwa na  Barabara ya Mkoa ya Ibungu - Ileje hadi  KKK Wilayani Rungwe ikiligawa katikati na kuacha upande mmoja kuwa  Kata ya Sange na upande mwingine Kata za Kafule na Sange.

HISTORIA YA SOKO:

Soko hili limekuwepo kwa muda mrefu likianzia kabla ya wakoloni, wakati wa ukoloni na baada ya Uhuru wa wetu mnamo 1961 hadi sasa.
Katengele awali palijulikana kama Katengele Bhalindu (yaani mabinti) ikielezwa kuwa ndipo palikutanisha vijana waliotaka kuoa au kuolewa kwa kabila la Wandali ambalo ni kubwa kwa Wilaya hii na maarufu kwa Mkoa wa Songwe na Mbeya kutokana na uchapaji kazi hususani zile za kutumia nguvu.
Kuhusu “Katengele Bhalindu” (yaani mabinti) hapa ndipo palipokuwa soko la awali pakiwa na msitu mdogo ambapo inasemekana kuwa mabinti wawili walipotea bila kupatikana katika mazingira ya kutatanisha kwa muda mrefu na imebaki kuwa simulizi inayoendelea  kila linapotajwa neno katengele.
Awali lilikutanisha watu wa maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Ileje na Wilaya za Mbozi, Rungwe na Kyela wakiuza bidhaa kwa fedha tasilimu pamoja na biashara ya kubadilishana bidhaa kwa bidhaa.  
Kwa miaka ya hivi karibuni limekuwa maarufu sana kwa biashara ya ng’ombe, bidhaa za asili pamoja na zile za viwandani likiwavutia hata raia wa Nchi jirani ya Malawi.

KUANZISHWA KWA MRADI WA SHAMBA LA MITI

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Misitu (TFS) imeamua kuanzisha Shamba la Miti la Iyondo - Mswima ukiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya 2015/2020 ibara ya 31 vifungu vya b,c,d,e na f kuhusiana sekta ya Maliasili.
Kwa mujibu wa Meneja wa Mradi wa Iyondo – Mswima Ndg. Deograsian Kavishe upandaji miti utaanza rasmi katika mwaka wa Fedha 2018/2019 ikiwa baadhi ya kazi zilianza kutekelezwa na Mradi katika mwaka wa fedha 2017/2018.
Kuanzishwa kwa shamba hili la Katengele kunaifanya Tanzania kuwa na mashamba ya miti ya kupandwa 23 yakiwa yanapatikana katika Kanda mbalimbali kati ya hayo manne yapo katika hatua ya uanzishwaji likiwemo hilo la Iyondo – Mswima (Ileje).

KUHAMISHWA KWA MNADA WA SOKO LA KATENGELE

Kutokana na soko hili kuwa ndani ya msitu wa hifadhi na kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa kwa kufuata Kanuni, Sheria na taratibu za uanzishwaji na uendeshaji wa miradi ya upandaji miti hapa Nchini, soko hilo halistahili  kuendelea kuwepo mahali lilipo, hivyo linatakiwa kuhamishiwa sehemu nyingine nje ya hifadhi zikiwemo kaya 13 zinazoishi ndani ya eneo hilo.
Ujenzi wa miundombinu katika eneo lililochaguliwa utafanywa na serikali kupitia wakala wa Misitu (TFS).

MICHAKATO YA KUHAMISHA SOKO

Ili kuendeleza mahusiano mazuri na wadau mbalimbali wa maendeleo TFS imeshirikisha Baraza la Madiwani, wataalam wa Halmashauri pamoja na Serikali Kuu.
Michakato hiyo ilianzia kwenye vikao vya CMT, Kamati ya Uchumi Ujenzi na Mazingira, Kamati ya Fedha Uongozi na Mipango pamoja na Baraza la Madiwani ambalo liliridhia kuhama kwa Mnada wa Soko hilo kutoka mahali lilipo na kwenda sehemu nyingine.
KIKAO CHA BARAZA LA MADIWANI
Baraza la Madiwani baada ya kujadili na kupitia mapendekezo ya vikao vilivyotangulia kisheria liliridhia juu ya kuhama kwa soko la Katengele kutoka mahali lilipo na kwenda Njiapanda ya Shule ya Msingi Mbangala katika barabara ya Ibaba - Katengele ili kupisha uanzishwaji wa Mradi wa Shamba la Miti la Iyondo - Mswima.

Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya upigaji kura kufanyika ambapo Wah. Madiwani wane waliliridhia mnada wa Katengele uhamishiwe eneo la Ghala - Sange huku Madiwani 18 wakiridhia Mnada wa Katengele uhamishiwe Njiapanda ya Shule ya Msingi Mbangala.

MAONI YA BARAZA LA MADIWANI

Baraza lilishauri kuwa wakati wa kuhamisha Mnada wa Katengele ufanyike utaratibu wa kukutanisha wananchi waliokuwa katika eneo la mnada pamoja na wadau wa mnada huo wakiwemo viongozi wa maeneo yanayozunguka mnada, machifu na Wah. Madiwani ili kuwajengea uelewa na kuwajulisha mchakato wa kuhamisha mnada.
Aidha ilishauriwa kutoa mwaliko kwa wadau kutoka maeneo mbalimbali ili kuwajulisha juu ya mabadiliko ya eneo jipya la mnada

GHARAMA ZA UJENZI WA MIUNDO MBINU KWENYE ENEO JIPYA LA MNADA

Serikali kupitia Wakala wa Misitu (TFS) inatarajia kujenga miundombinu katika eneo jipya la mnada ili kutoathiri bajeti ya Halmashauri ambayo tayari ilishatekelezwa kwenye soko la awali ukiwemo ujenzi wa machinjio.

MANUFAA YA MRADI WA UPANDAJI MITI WA IYONDO MSWIMA-ILEJE

Meneja wa Mradi huu Ndg. Deograsian Kavishe alibainisha faida kadha zitakazotokana na kuwepo kwa Mradi huu kiwilaya, kitaifa na kimataifa ambazo ni pamoja na:
Ajira kwa jamii ambapo mpaka sasa wananchi wa maeneo hayo wameshaanza kufanya kazi za awali katika Mradi huo, ongezeko la viwanda ndani na nje ya Wilaya vinavyochakata mazao ya magogo, kukabiliana na ongezeko la uvunaji miti michanga (pre mature) na  jamii kupata elimu ya upandaji miti.
Faida zingine ni uanzishwaji na uboreshaji wa huduma za jamii, kuwezesha Mashamba Darasa ya miti kwa Taasisi za Serikali kama vile shule na magereza pamoja na kugawa miche ya miti kwa jamii ikiwa ni njia mojawapo ya uhamasishaji wa upandaji miti.
Kuanzishwa kwa Mradi huu kutaitangaza Ileje kitaifa na kimataifa kutokana na shughuli za kitalii zinazoweza kufanywa katika eneo hilo lenye jiografia ya kipekee katika Mkoa wa Songwe pamoja na uwepo wa nyani aina ya mbega ambao hupatikana sehemu zenye baridi kali.

CHANGAMOTO ZA UANZISHWAJI WA SHAMBA LA IYONDO MSWIMA NA UHAMISHAJI WA MNADA WA KATENGELE

Zipo chanagamoto kadha zinazokabili juu ya kuanzishwa kwa Mradi huu, moja ni mshituko na hofu kwa watumiaji wa soko hilo ambao wanaona giza mbele yao hili linatokana na mazoea ya uendeshaji wa mambo.
Pia hofu nyingine ni juu ya hatima ya miti ya watu binafsi ambayo imebainika kuwa ipo ndani ya hifadhi ya Msitu wa Iyondo – Mswima ambao walitumia gharama kubwa katka kuipanda ikiwa ni sehemu ya uwekezaji.

MAONI YA MWANDISHI WA TAARIFA HII

Kila jambo linapoanzishwa huwa na changomoto zake, hata ujenzi wa barabara ya Mpembe - Isongole ambayo kwa muda mrefu tumekuwa tukiihitaji imeshawathiri baadhi ya watu hata kuhamia kwa Serikali yetu huko Dodoma kumewaathiri baadhi ya watu.
Kinachotakiwa ni kutathmini faida na hasara juu ya jambo tunalolihitaji si lazima tulio hai sasa tukanufaika bali twaweza kuwa washiriki wa ujenzi wa misingi imara kwa vizazi vijavyo kama walivyofanya babu zetu ambao licha ya kutokuwa na “Elimu ya Kimagharibi” kuna mambo walifanya ambayo mpaka leo tunayafaidi ukiwemo ulinzi wa mazingira.
Kamwe tusikubali ujio wa miradi kama hii kutugawa  bali tukae pamoja kwa kujadiliana ili tuweze kuimba wimbo mmoja kwa kufuata midundo ya ngoma inayopigwa.
Imeandaliwa na:

Daniel J. Mwambene

KITENGO CHA HABARI
ILEJE




Eneo la Mnada wa Katengele Wilayani Ileje mkoani Songwe unaotakiwa kuhamishwa ili kupisha Mradi wa Upandaji Miti.
Askari Jeshi USU (ambalo ni jina geni kwa wengi ) Deograsian Kavishe Meneja Mradiwa Upandaji Miti wa Iyondo-Mswima akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Ileje.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Mhe.Ubatizo Songa akiongoza Wahe. Madiwani na Wataalam wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje walipotembelea eneo la Mradiwa Upandaji Miti la Iyondo-Mswima



Sehemu ya Msitu wa Iyondo-Mswima ikionesha msitu wa asili na kupandwa.
Kitalu cha miti kilichopo Katengele-Ileje kikitarajiwa kubadilisha sura ya msitu wa Iyondo-Mswima wiyani Ileje
Eneo la Njiapanda ya Shule ya Msingi Mbangala panapotarajiwa kuhamishiwa Mnada wa Katengele.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje Ndugu Haji Mnasi (aliyesimama) akizungumza kwenye Baraza Maalum kuhusu Mnada wa Katengele








No comments: