Monday, June 11, 2018

SERIKALI YAPOKEA GAWIO LA SH. BILIONI 10.1 KUTOKA NMB

Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma

Benki ya NMB imetoa gawio la Sh. bilioni 10.1 kwa Serikali ambayo inamiliki asilimia 32 ya hisa za Benki hiyo baada ya kupata faida ya Sh. bilioni 94.8 baada ya kodi kwa mwaka 2017/2018.

Tukio hilo la kukabidhi hundi kifani ya gawio hilo limefanyika Makao Makuu ya Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma, kati ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango, kwa niaba ya Serikali, na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Ineke Bussemaker. 

Dkt. Mpango amezipongeza juhudi za watendaji wa Benki hiyo waliofanikisha kupatikana kwa faida iliyowezesha Serikali kupata gawio licha ya changamoto zilizoikumba Sekta ya Benki likiwemo suala la mikopo chechefu.

“Mikopo chechefu imekua tatizo kwa Benki nyingi nchini hivyo ninatoa rai kwa Benki ya NMB kuhakikisha inafuata taratibu za kukopesha na kuendelea kusimamia vizuri wakopaji ili kuondoa tatizo la mikopo chechefu” alieleza Dkt. Mpango. 

Aidha ameipongeza Benki hiyo kwa kutoa huduma katika Sekta ya kilimo na kuitaka ipanue wigo zaidi na kuziwezesha sekta za uvuvi na ufugaji kutokana na umuhimu wake katika ukuaji wa uchumi wa taifa. 

Alisema kuwa anatarajia Benki hiyo itatoa gawio zaidi mwaka ujao wa fedha na amemwagiza Msajili wa Hazina, kuzihakiki taasisi zote ambazo Serikali imewekeza hisa zake ili zitoe gawio lasivyo ametishia Serikali kuondoa hisa zake kwakuwa uwekezaji huo hautakuwa na tija. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Ineke Bussemaker alieleza kuwa licha ya Benki yake kutoa gawio hilo la shilingi bilioni 10.1 kwa Serikali, pia inalipa kodi za Serikali vizuri ambapo katika kipindi cha mwaka 2017/18 imetoa kodi ya shilingi bilioni 127.

Aliongeza kuwa tangu mwaka 2014 hadi 2017 benki hiyo imetoa kodi zinazofikia zaidi ya shilingi bilioni 460 na kwamba itaendelea kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za kibenki ili iweze kupata faida na kulipa gawio kubwa zaidi kwa wana hisa wake ikiwemo Serikali inayomiliki silimia 31.8 ya hisa 500.

Aidha, amesema kuwa Benki yake imeendelea kufanya kazi kwa karibu na Sekta ya Kilimo kwa kutoa huduma za kifedha kwa wakulima wakiwemo wakulima wa Tumbaku na Korosho katika mikoa ya Kusini ya Lindi na Mtwara, ambapo imefungua zaidi ya akaunti 300,000 na kuweza kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 250 mwezi Novemba mwaka jana.

Bi. Bussemaker alisema kuwa Benki yake inajitahidi kuhakikisha kunakua na huduma jumuishi za kifedha kwa wananchi kote nchini kwa kuweka Mawakala na kuongeza Matawi ya Benki hiyo na pia kuhamasisha wananchi wafungue Akaunti ya Benki hiyo.

Alisema kuwa ili kufanikisha utoaji wa huduma hiyo ya kifedha kwa watanzania, Benki hiyo imejipanga kutumia teknolojia ya kisasa ya masuala ya fedha ambayo itarahisisha kuwafikia watu wengi ikiwemo huduma za fedha kwa njia ya simu za mkononi. 

Katika Mwaka wa Fedha 2016/2017, Benki hiyo ilitoa gawio la shilingi bilioni 16.5 kwa Serikali, huku kukiwa na pungufu ya shilingi bilioni 6 mwaka huu hatua iliyomlazimu Dkt. Mpango kuiagiza Benki hiyi ihakikishe inaboresha huduma zake ili Serikali ipate gawio kubwa zaidi kwa ajili ya kutumia fedha hizo kuwaletea wananchi maendeleo katika sekta za maji, afya, elimu, na miundombinu mingine muhimu.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Bi. Ineke Bussemaker (kulia), akieleza kuhusu mkakati wa Benki yake wa kuhakikisha inaongeza ufanisi na kufungua akaunti za wateja wengi zaidi, wakati wa hafla ya kutoa gawio la Sh. bilioni 10.1 kwa Serikali ambayo ni mwanahisa, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
 Msajili wa Hazina Bw. Athuman Mbuttuka (Kushoto), Kaimu Kamisha wa Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Benedict Mgonya (katikati) na Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara hiyo Bw. John Rubuga, wakisikiliza kwa makini maelezo ya Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor. Mpango (Mb), kuhusu taasisi za fedha kutakiwa kuwafikia wafugaji na wavuvi wakati wa kupokea gawio la Sh. bilioni 10.1 kutoka Benki ya NMB, Jijini Dodoma.
 Kaimu Kamishna wa Sera Bw. William Mhoja (kushoto) na Kamishna Msaidizi wa Bajeti Bw. Pius Mponzi, wakifuatilia tukio la Benki ya NMB kuipatia Serikali inayomiliki asilimia 32 ya hisa za Benki hiyo, mgao wa Shilingi bilioni 10.1, baada ya kupata faida katika biashara mwaka 2017.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor. Mpango (Mb) (mbele),  akitoa maelekezo kwa taasisi za fedha kuzingatia kanuni za kukopesha ili kuondoa mikopo chechefu,  wakati wa hafla ya Benki ya NMB kutoa gawio la Sh. bilioni 10.1 kwa Serikali ambayo ni mwanahisa, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor. Mpango (Mb),  akitoa maelekezo kwa Msajili wa Hazina, Bw. Athuman Mbuttuka, kuzihakiki taasisi zote ambazo Serikali imewekeza hisa zake ili zitoe gawio kwa Serikali, wakati wa hafla ya Benki ya NMB kutoa gawio la Sh. bilioni 10.1 kwa Serikali ambayo ni mwanahisa, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor. Mpango (Mb) (wa sita kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Bi. Ineke Bussemaker (wa saba kushoto) na Maafisa waandamizi kutoka Benki ya NMB na Wizara hiyo wakiwa katika picha ya pamoja baada ya Serikali kupokea gawio la Sh. bilioni 10.1 kutoka NMB, Jijini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor. Mpango (Mb) (kushoto) akipeana mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Bi. Ineke Bussemaker, baada ya kupokea gawio la Sh. bilioni 10.1 kutoka NMB, katika ukumbi wa Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dodoma.
 Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor. Mpango (Mb) (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Bi. Ineke Bussemaker, wakiangalia hundi kifani yenye thamani ya shilingi bilioni 10.1, ambayo ni gawio lililotolewa na Benki ya NMB kwa Serikali, Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor. Mpango (Mb) (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB Bi. Ineke Bussemaker, wakipeana mkono wakati wa makabidhiano ya hundi kifani yenye thamani ya shilingi bilioni 10.1, ambayo ni gawio lililotolewa na Benki ya NMB kwa Serikali, Jijini Dodoma.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Fedha na Mipango)

No comments: