*Kamishna wa Bima nchini atoa ufafanuzi , aipongeza kampuni ya Sanlam kwa kutimiza miaka 100
Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
KAMISHNA wa Bima nchini Dk.Baghayo Saqware amesema kuanzia Agosti mwaka huu kampuni za bima nchini yataanza kusajili mawakala wa bima wao wenyewe kadri wanavyoweza huku mchakato wa ununuzi wa bima kwa njia ya kibenki ukiendelea.
Ametoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam wakati wa sherehe ya kutimiza miaka ya 100 ya kampuni ya bima ya Sanlam tangu kuanzishwa kwake.
Hivyo mbali ya kuipongeza Sanlam kwa kutimiza miaka 100 akatumia nafasi hiyo kutoa majibu ya changamoto ambazo ziliwasilishwa kwake na Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Sanlam Ibrahim Kduma.
Kaduma pamoja na kuzungumzia mafanikio ya kampuni hiyo kwenye masuala ya bima ametaja changamoto tatu ambazo zinakwamisha sekta ya bima nchini.Changamoto hizo ni masharti magumu ya kusajili wakala wa bima, kuchelewa kwa mchakato wa benki kutumika kununua bima pamoja na kodi kubwa.
Hivyo Dk.Saqware amewahakikisha watoa huduma za bima nchini kuwa tayari yameandaliwa mabadiliko ya sheria na hivyo kampuni ya bima itakuwa na uwezo wa kusajili mawakala wengi kadri ya uwezo wao.
Kuhusu benki kufanya shughuli za bima Dk.Saqware amefafanua changamoto hiyo nayo itapata ufumbuzi hivi karibuni kwani hivi sasa wanaandaa kanuni na Agosti mwaka huu watazipeleka kwa wadau ili wazipitie na kisha kuanza kutumika bada ya kupata baraza za Waziri.
"Kuhusu benki kufanya shughuli za bima hili lilichekelewa kwasababu Benki Kuu Tanzania(BoT) ilikuwa inataka kujiridhisha na sas imekubali , hivyo ni changamoto ambayo kimsingi imepata ufumbuzi wake na kilichobaki ni kuandaliwa kwa kanuni ili benki nazo zitumike kwenye masuala haya ya bima"amesema.
Akijibu kuhusu chagamoto ya kodi katika bima ya maisha, amejibu ni vema wadau wa bima wakafanya utafiti na kisha kuuwasilisha kwa Kamishna wa Bima.Amesema kuwa baada ya utafiti huo na maombi ya wadau wataangalia kama kuna uwezekano wa kutoa unafuu wa kodi au laa lakini akawahakikishia ni jambo ambalo linazungumzika kwani lengo la Serikali ni kuona suala la bima linapewa kipaumbele ili wananchi wengi wawe a bima mbalimbali.
Kuhusu kampunni ya Sanlam kutimiza miaka 100 tangu kuanzishwa kwake Juni 8 1918, Dk.Saqware amesema wanastahili pongezi kwani ni wazi wapo imara na wameweza kukabiliana na kila aina ya changomoto na kuzivuka wakiwa salama na bora katika kutoa huduma ya bima na hasa bima ya maisha.
Amesema bila kuwa na menejementi imara na yenye kupanga mipango ya uhakika ni ngumu kampuni kufika miaka 100 na kutoa mifano ya kampuni nyingi ambazo zimenzishwa na hazikufika miaka kama hiyo.Hivyo amewataka kuendelea kujiimarisha na kuendelea kutoa huduma bora za bima nchini.
Awali Mwenyekiti wa Bodi wa Kampuni ya Sanlam mbali ya kutaja changamoto hizo amesema sekta ya bima nchini bado haijapewa kipaumbele na hivyo kati ya watanzania milion 54 waliopo katika soko la bima ni asilimia 1.3.
"Ni vema kukawa na mikakati ya kuhakikisha idadi ya wanaonufaika na bima inaongezeka na moja ya kuhakikisha changamoto zilizopo zinaondelewa ili kupanua wigo wa masuala ya bima nchini.Kenya wamepiga hatua kwenye soko la bima ukingalinganisha na sisi,"amesema Kaduma.
Wakati huohuo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bima ya Sanlam Khamis Suleiman amesema pamoja na kujikita kwenye bima ya maisha bado wamekuwa wakijihusisha na shughuli za kijamii katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema kupitia Sanlam Foundation wametengea Sh.milioni 413 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa miundombinu kwenye sekta elimu nchini kwa kufanya mambo mbalimbali yakiwamo ya ujenzi wa madarasa.
Amefafanua kila mwaka kwenye mfuko huo watatumia Sh.milioni 136 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu na mradi huo ni wa kipindi cha miaka mitatu na kwamba watatekeleza ujenzi huo kwenye mikoa ambayo katika sekta ya elimu bado changamoto ziko nyingi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Bima ya Sanlam Life Insurance, Khamis Suleiman (wapili kushoto), akizungumza na baadhi ya wateja wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 100 ya kampuni hiyo.Hafla hiyo iliyofanyika jana usiku jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Bodi wa Kampuni ya Bima ya Sanlam Life Insurance Ibrahim Kaduma (kulia) pamoja na viongozi wengine akigonganisha glasi pamoja na wateja wa kampuni hiyo wakati wa hafla ya maadhimisho ya miaka 100 ya Sanlam tangu kuanzishwa kwake. Wa tatu kushoto ni Kamishna wa Bima Dk Baghoyo Sakwale ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wateja waliohudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 100 ya Kampuni ya Bima ya Sanlam Life Insurance ambayo imefanyika jijini Dar es Salaam ambapo pia wadau mbalimbali wa masuala ya bima walihudhuria.
No comments:
Post a Comment