Thursday, June 14, 2018

MRADI UBORESHAJI RELI YA KATI DAR ES SALAAM - ISAKA (TRC) KUANZA,

Muonekano wa mradi wa uboreshaji wa reli ya kati Dares Salaam- Isaka ukiendelea.

 
Wanakijiji wa Halmashauri ya kibaha vijijini, wakifuatilia kwa makini maelelezo yanayotolewa katika mkutano unaoendeshwa na wataalamu kutoka shirika la reli Tanzania - TRC Kuhusu uboreshaji wa Reli ya kati Dar es salaam- Isaka
 Afisa maendeleo ya jamii TRC Bi Catherine Mroso, , akitoa maelezo katika kampeni ya uhamasishaji wa uelewa wa uboreshaji wa reli ya kati Dar es Salaam – Isaka katika mkutano na viongozi wa Halimashauri ya kibaha vijijini, Magindu, Mkoani Pwani.

 
Mratibu wa mradi wa uboreshaji wa reli ya kati Dares Salaam- Isaka, kutoka TRC Mhandisi Mlemba Allen Singo ni  akitoa maelezo katika mkutano wa wananchi wa Halmashauri ya Kibaha vijijini, Magindu, Mkoani Pwani





SHIRIKA LA RELI TANZANIA – TRC 

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 

YAH: MRADI WA UBORESHAJI WA RELI YA KATI 

Uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Uongozi wa TRC wamedhamiria kukarabati reli ya kati kipande cha kuanzia Dar es Salaam – Isaka (km970). Mradi huu umefadhiliwa na Benki ya dunia na kutekelezwa na Shirika la Reli Tanzania katika kipindi cha muda wa miaka miwili kuanzia juni 2018 hadi juni 2020. 

Lengo la uboreshaji wa reli ya kati ni kutoa usafiri wa kuaminika na kukuza upatikanaji wa huduma bora Nchini. Na maboresho hayo yatasaidia kuinua uwezo wa kubeba mzigo toka chini ya tani 13.5 za uzito wa eskeli hadi tani 18.5 kwa kufanya yafuatayo: 

I. Kutandika upya njia za reli zenye uzani wa paundi 80 kwa urefu wa kilometa 312 

II. Kufanya ukarabati wa njia ya reli iliyosalia kwa urefu wa kilometa 658 

III. Kufanyia ukarabati makaravati na madaraja 442 

IV. Kuboresha mfumo wa mawasiliano 

V. Kuboresha vituo vya kupakia na kupakua mizigo vya bandari ya Dar es Salaam, ilala na Bandari kavu ya Isaka. 

VI. Ununuzi wa vichwa vitatu vya treni (vipya) na mabehewa mapya 44 ya mizigo 

Katika kufikia malengo haya TRC itaingia mikataba 64 kati ya hiyo 32 ni ya kuajiri Washauri mbalimbali, 6 ni ya ujenzi na 24 ununuzi wa vifaa mballimbali na mikataba miwili ni ya huduma. Mpaka sasa zaidi ya 50% ya mikataba hii imeshasainiwa. 

Kupitia Mradi huu TRC pia imetengeneza mpango endelevu wa matengenezo ya miundombinu ili kufanya njia ya usafiri huu kuwa wa uhakika na kuaminika. Kuimarika kwa usafiri wa reli kutapunguza gharama za matengenezo ya barabara na hivyo serikali kuelekeza bajeti iliyookolewa kwenda kwenye huduma nyingine za kijamii. 

Maendeleo ya utekelezaji wa Mradi 

Kabla ya kuanza rasmi ukarabati wa njia za reli mwezi juni, TRC inaendelea kufanya kampeni ya uhamasishaji katika Mkoa wa Pwani na Dar es Salaam, katika Manispaa ya Ilala na Halmashauri ya Kibaha vijijini, ili kujenga uelewa kwa wananchi kuhusiana Mradi huu kupitia mikutano mbalimbali ya hadhara katika kata na vijiji vinavyopitiwa na mradi huu. 

Kampeni hiyo ya uhamasishaji inaambatana na kuelezea faida za mradi wakati wa ujenzi ambazo ni kuwepo kwa fursa za ajira, kukua kwa kipato cha wananchi maeneo ya mradi na kujengewa ujuzi kwa wote watakaoshiriki kwenye shughuli za ujenzi. 

Pia wananchi wamepata fursa ya uelewa faida za mradi baada ya uboreshaji wa reli ya kati ambazo ni kuboresha na kuongeza kiwango cha ubebaji mizigo kwa miuondo mbinu ya reli na madaraja. Kuongezeka kwa mwendokasi wa treni kutoka kilometa 35 kwa saa hadi kufikia kilometa 70 kwa saa na hivyo kupunguza gharama na muda wa usafirishaji mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam hadi bandari kavu ya Isaka hadi kufikia saa 24 kutoka zaidi ya masaa 36 ya sasa. 

Kampeni ya uhamasisha kwa wananchi imepelekea wapate kutambua hatua za uboreshaji ambapo Mradi huu umegawanyika katika vipande viwili, kipande cha kwanza kitaanzia Dar es Salaam hadi kilosa (kilometa 283), kipande cha pili ni kilosa hadi Isaka (kilometa 687) na vipande hivi vimeshapata wakandarasi na ujenzi unataraji kuanza mapema juni 2018. 

Kampeni ya uhamasishaji ni enedelevu mpaka pale mradi utakapokamilika, Uongozi wa TRC umesisitiza mambo ya kuzingatia kwa wananchi ambao reli ya kati inapita katika maeneo wanayoishi, ambayo ni: Hairuhusiwi shughuli zozote za kibinadamu katika maeneo ya reli ikiwa ni pamoja na biashara,kilimo na ufugaji. 

Wafanyabiashara wote watapaswa kupata kibali maalum cha biashara kutoka katika stesheni.Wakulima na wafugaji hawaruhusiwi kabisa kufanya shughuli za kilimo na ufugaji katika eneo la reli,vilevele wafugaji wanapaswa kutumia vivuko vya mifugo vinavyotambulika na kuepuka kuvusha mifugo yao maeneo yasiyo na vivuko. 

Tahadhari, Jamii inapaswa kuchukua tahadhari za kiafya na tabia zozote hatarishi ili kuepuka maambukizi ya magonjwa ya zinaa kama vile kaswende,kisonono na hata maambukizi ya virusi vya UKIMWI. 

Imetolewa na idara ya uhusiano kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa TRC

No comments: