Wednesday, June 27, 2018

MKUU WA MKOA WA IRINGA AWAFUNDA MAKANDARASI WANAWAKE


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza, amewataka makandarasi wanawake wote nchini kufanya kazi kwa kujiamini na kutooneana wivu katika maeneo yao ya kazi.

Amesema kuwa lengo la Serikali ni kuwawezesha makandarasi wanawake kufikia madaraja ya juu ya ukandarasi ili kuwawezesha kuchukua kandarasi kubwa, na hivyo kuinua kipato chao kitakachopelekea kuondokana na umaskini katika familia na jamii zinazowazunguka.

Ametoa wito huo mkoani Iringa, wakati akifungua mafunzo elekezi kwa makandarasi wanawake wa mikoa ya nyanda za juu kusini katika ushiriki wa kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara hapa nchini na kusema kuwa mashindano yao yawe ni ya kutimiza wajibu na siyo kushindana katika kuvaa wala kusuka.

"Nataka mwanamke wa kitanzania ujiamini na kusimama vyema na kusonga mbele kwani sifa yetu kubwa ni kuhakikisha tunatunza familia kwa hali yoyote, wajibikeni ipasavyo katika kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara bila woga wowote", amesema Mhe. Masanze.

Aidha Mhe. Masenza, amesisitiza umuhimu wa makandarasi hao kujaza nyaraka za zabuni na mikataba wenyewe ili kuepukana na utapeli na baadhi ya watu wanaojidai wanawasaidia shughuli hizo. Amewataka makandarasi wanawake hao kufanya kazi kwa ushirika na sio mmoja mmoja ili kuweza kumiliki kampuni au vikundi vya ujenzi ambavyo vitawasaidia kupata zabuni za miradi mikubwa inayoendelea kutekelezwa hapa nchini.

Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wanawake kutoka Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Rehema Myeya, amesema mafunzo hayo yatawasaidia makandarasi wanawake hao kuwajengea uwezo wa namna bora ya kujaza makabrasha ya zabuni pamoja na kusimamia mikataba kwa ufanisi zaidi. Ameongeza kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo katika nyanja za uongozi na namna bora zaidi za kutunza mahesabu na fedha ili waweze kuona faida ya kazi zao.

Naye Bi. Gisela Gongo kutoka mkoa wa Iringa amezitaja changamoto mbalimbali zinazowakabili makandarasi hao ikiwemo uelewa mdogo wa namna ya kujaza mikataba na kulalamikia kuwa lugha zinazotumika kwenye mikataba hiyo kuwa sio rafiki na hivyo kuwasababishia kukosa kazi nyingi za ujenzi na matengenezo ya barabara.

Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Iringa Mhandisi Daniel Kindole, amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa kufungua mafunzo hayo ambayo yanalengo la kuwaongezea uwezo na idadi ya makandarasi wanawake hapa nchini. Jumla ya makandarasi wanawake 35 kutoka katika mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Ruvuma, Rukwa na Katavi wameshiriki mafunzo hayo yakiwa na lengo kuu la kuwajengea uwezo zaidi ili waweze kushiriki na kushindana katika kazi za ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara hapa nchini.


Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano .

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza, akihutubia makandarasi wanawake kutoka mikoa ya nyanda za juu kusini (hawapo pichani), wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo katika ushiriki wa kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara, yaliyofanyika mkoani humo. 
Mratibu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wanawake kutoka Sekta ya Ujenzi, Mhandisi Rehema Myeya, akizungumza wakati akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza (kulia), kufungua mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo makandarasi wanawake katika ushiriki wa kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara, yaliyofanyika mkoani humo.
Baadhi ya makandarasi wanawake kutoka mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Ruvuma, Rukwa na Katavi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza (hayupo pichani), wakati wa ufunguzi wa mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo katika ushiriki wa kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara, yaliyofanyika mkoani Iringa.
Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Iringa Mhandisi Daniel Kindole, akimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza, mara baada ya kufungua rasmi mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo kwa makandarasi wanawake katika ushiriki wa kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara, yaliyofanyika mkoani Iringa. 
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza akiwa katika picha ya pamoja na makandarasi wanawake kutoka mkoa wa Iringa baada ya kufungua mafunzo elekezi ya kuwajengea uwezo katika ushiriki wa kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara, yaliyofanyika mkoani humo.Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano

No comments: