Na. Hassan Mabuye, Wizara ya Ardhi.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ameokoa takriban shilingi bilioni 16 za upimaji wa mpaka kati ya Tanzania na Kenya mara baada kuanza kazi ya upimaji wa mpaka huo wenye urefu wa jumla za kilomita 760 za nchi kavu.
Akiongea jana wakati akikagua kazi ya uwekaji wa alama mpya za mipaka iliyowekwa katika wilaya ya Tarime mkoani Mara Waziri Lukuvi amesema hapo awali wataalamu wa upimaji wa mpaka huo waliandaa makisio ya bajeti ya kiasi cha shilingi bilioni 22 ambapo mara baada kuanza kwa zoezi hilo amegundua kwamba zoezi hilo litagharimu shilingi bilioni 6 hadi kumalizika kwake.
“tulipanga kutumia shilingi bilioni 22 zilizokuwa katika makaratasi ambapo katika uhalisia tangu kuanza kwa kazi hii ya uwekaji alama mpya za mipaka tumegundua ya kwamba serikali inaweza kutumia shilingi bilioni 6 tu ambazo zitamaliza kazi hii ya uwekaji wa alama za mipaka kati ya Tanzania na Kenya” amesema Lukuvi.
Aidha, Waziri Lukuvi amewapongeza watendaji wa Idara ya Upimaji na Ramani iliyopo Wizara ya Ardhi inayoongozwa na Dkt. James Mtamakaya kwa kazi nzuri ya kizalendo iliyopelekea kuokoa fedha za serikali kwa kushirikiana na wataalam wa Mkoa na Halmashauri.
Ameongeza kwamba, kuna tofauti kubwa kati ya mipango ya fedha katika makaratasi na uhalisia wa kazi katika eneo husika, mara baada ya kuanza kazi katika maeneo husika ya uwekaji wa alama mpya za mpaka kati ya Tanzania na Kenya imebainika kiuhalisia kazi hiyo haitatumia kiasi kikubwa cha fedha kama ilivyokisiwa hapo awali.
Waziri Lukuvi amefanya ziara hiyo ya ukaguzi wa mpaka wa Tanzania na Kenya ambapo juzi amekagua mpaka wa Tanzania na Kenya katika eneo la mpaka lililopo wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro na jana amekagua mpaka wa Tanzania na Kenya katika eneo la mpaka lililopo wilaya ya Tarime Mkoani Mara.
Tanzania imeamua kuimarisha mipaka yake yote ya kimataifa kufuatia changamoto nyingi zinazojitokeza tangu kuasisiwa na wakoloni katika miaka ya 1886 hadi 1890 ambapo alama za mipaka hiyo ziliwekwa kwa umbali wa takribani kilomita 2 hadi 10 kutoka alama moja na nyingine hivyo kusababisha wananchi kutoielewa mipaka ya nchi zao kwa urahisi na hatimaye kuleta migongano.
Kazi hii ya kuimarisha mipaka ni Azimio la Umoja wa Afrika kwamba nchi zote ziwe zimekamilisha zoezi la uimarishaji wa mipaka ya kimataifa ifikapo mwaka 2022. Na baada ya zoezi hili la uwekaji wa alama mpya za mipaka yatatayarishwa Makubaliano (Protocol) ambayo yatasainiwa rasmi na viongozi wakuu wa nchi hizi mbili.
Kwa sasa serikali ya Tanzania na Kenya zimeamua kuweka alama mpya za mpaka kwa umbali wa mita 100 kutoka alama moja na nyingine ili iwe rahisi kwa wananchi kuziona alama hizi, sambamba na kutoa elimu kwa wananchi wanaoshi katika mpaka huo. Kazi hiyo inatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Marais wote wawili wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Kenya, Mhe. Uhuru Kenyata.
Uwekaji wa alama hizo unataraji kutatua changamoto zinazokabili mipaka ya nchi yetu ambazo, ni baadhi ya wananchi kufanya maendelezo ya ujenzi wa nyumba na kulima mashamba katika maeneo ya mipaka, hali inayopelekea migongano.
Aidha, changamoto hizi zinasababisha ugumu wa utengenezaji wa barabara ya kuhudumia mipaka ya nchi hizi mbili kwa kuwa watu wamevamia mipaka na kufanya maendelezo, pia inaleta ugumu wa uwekaji wa miundombinu ya maji na inaleta ugumu wa udhibiti wa magonjwa ya kuambukizwa ya wanaadamu na mifugo.
Changamoto nyingine inayosababishwa na kutokuwepo kwa alama za mipaka inayoonekana kwa wazi ni ugumu wa kudhibiti njia haramu za kupitisha bidhaa na hivyo kukosesha serikali mapato na hata katika masuala ya ulinzi na usalama wa nchi.
Mara baada ya kumaliza uimarishaji wa mipaka ya nchi hizi mbili Tanzania na Kenya wenye urefu wa kilometa 760 zikiwa za nchi kavu na kilomita 59.71 zikiwa ni mpaka wa majini. Kwa mwaka ujao wa fedha Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi itaimarisha mpaka wa Tanzania na Uganda na baadae kuendelea na mipaka mingine
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akikagua alama za mpaka wa Tanzania na Kenya.
No comments:
Post a Comment