Thursday, June 14, 2018

KUBENEA AWATAKA VIONGOZI WA KISIASA KUWA KIPAUMBELE KATIKA KUCHOCHEA MAENDELEO

 Na Humphrey Shao, Globu ya Jamii
MBUNGE wa Ubungo, Saed Kubenea ametoa wito kwa viongozi mbalimbali nchini kuacha siasa na badala yake kufanyakazi kwa kwaajili ya maendeleo.Kubenea ametoa kauli hiyo leo  jijini Dar es Salaam alipotembelea miradi ya Maendeleo katika jimbo lake la Ubungo na kuikabidhi.

Miradi aliyoitembelea Kubenea ni wa ujenzi wa kibanda cha kupumzikia katika Zahanati ya Mavurunza iliyopo Kimara ambao umegharimu sh. Milioni 7.7, miradi wa ujenzi wa madarasa katika shule ya Msingi Mabibo ambao umegharimu Sh. milioni 17, mradi wa kisima katika soko la Mabibo uliogharimu sh. Milioni 12 pamoja na ujenzi wa ofisi za walimu katika Shule ya Msingi Kawawa.
Akizungumza baada ya kutembelea na kuikabidhi miradi hiyo, Kubenea alisema ni vyema kufanya kazi kwa kushirikiana na sio kuangalia chama.

"Mimi sifanyi mambo haya kwaajili ya siasa, ninafanya kwaajili ya maendeleo ya wananchi....ninajua hata siku nikiondoka itabaki historia kwamba Kubenea alifanya kitu fulani.
"Kwahiyo niwaombe viongozi wote, tusiangalie siasa eti huyu chama tawala, huyu Chadema...tufanye kazi pamoja katika kuleta maendeleo ya Taifa letu," alisema Kubenea.
Kubenea aliongeza kuwa maendeleo yana safari ndefu hivyo maeneo ya Hospitali, shule yanahitaji kuboreshwa.
Akizungumzia miradi hiyo Kubenea alisema fedha zake zimetoka katika mfuko wa jimbo ambapo ni sehemu ya fedha za bajeti ya mwaka 2017/18.

Akitoa shukrani kwa ujenzi wa Kibanda cha Mapumziko, Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Mavurunza alisema walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya msongamano wa wagonjwa ambao ulisababishwa na kutokuwa na sehemu ya kupumzika.
"Kwasasa tunafanya kazi kwa uhuru na usiri kati ya mgonjwa na daktari....tunakushukuru Mbunge wetu ambaye uliamua kujitolea fedha hizi kutoka katika mfuko wako," alisema Dorothy.
Aidha Dorothy alisema Zahanati hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo  jengo la wazazi kuhitaji ukarabati, kutokuwa na uzio pamoja eneo hilo kuhitaji kusawazishwa ambapo Kubenea aliahidi atalisawazisha kwa kipindi kifupi.
Naye Mkuu wa Shule ya Mabibo, Hussein Mabibo alisema fedha zilizotolewa ambazo ni sh. milioni 17 zimesaidia kujenga madarasa matano, kubadilisha vigae vilivyochakaa na kuweka mabati, kupanga rangi shule, kukarabati ofisi ya walimu pamoja na ofisi ya mwalimu Mkuu.
"Tunakuamini wewe Mbunge wetu ukisema hua unatekeleza, hivyo tunaomba utusaidie pia kukamilisha maktaba, ujenzi wa uzio wa shule kwaajili ya usalama wa wanafunzi pamoja na ukarabati wa madarasa tisa ambayo yako katika hali mbaya," alisema Dady.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa na Soko la Mabibo, Yusuph Kilema alisema kisima kilichojengwa katika soko hilo kimekamilika kwa asilimia 90 ambapo bado vitu vichache ili kianze kutumika rasmi.



 Mbunge wa jimbo la  Ubungo, Saed Kubenea akizungumza na wakazi wa kata ya Mavurunza Kimara mara baada ya kukabidhi jengo la kupumzikia wagonjwa katika zahanati ya Mavulunza lililojengwa na fedha za mfuko wa jimbo
 Mbunge wa jimbo la  Ubungo, Saed Kubenea  akiwa amembeba mmoja wa watoto waliofika kupata huduma katika Zahanati ya Mavurunza .
 Mbunge wa jimbo la  Ubungo, Saed Kubenea akisoma gharama za ujenzi wa Mnara wa kupandisha maji juu katika kisima kilichojengwa katika soko la Mabibo Garment kwa fedha za mfuko wa jimbo
 Mhandisi wa maji wa Manispa ya Ubungo akitoa maelezo kwa Mbunge wa jimbo la  Ubungo, Saeed Kubenea wakatia  alipotembelea miradi iijengwa kwa fedha za mfuko wa jimbo.
 Mwalimu wa shule ya Msingi Mkwawa Mabibo akimueleza Mbunge wa jimbo la  Ubungo, Saed Kubenea kiasi cha fedha zinazohitajika katika umaliziaji wa ofisi za walimu.
 Mbunge wa jimbo la  Ubungo, Saed Kubenea akiwa ameongozana na baadhi ya watendaji wa halmashauri na wafanyabishara wa soko la Mabibo
  Mbunge wa jimbo la  Ubungo, Saed Kubenea akisalimiana na wananchi na Makada Mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi.
  Mmoja ya wakazi wa Mavurunza akitoa pongezi kwa Mbunge wa jimbo la  Ubungo, Saed Kubenea mara bada ya kutekeleza ahadi zake kwa wakazi wa eneo hilo 

 wakazi wa Ubungo kata ya Mavurunza wakiwa wanasikiliza hotuba ya mbunge wa jimbo la  Ubungo, Saeed Kubenea 

 Mbunge wa jimbo la  Ubungo, Saed Kubenea akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mkwawa Mabibo

No comments: