Monday, June 25, 2018

KAMPUNI YA KANTON INVESTMENT, HALMASHAURI YA HANDENI WASAINI MAKUBALIANO KUENDELEZA ZAO LA MUHOGO

Na Grace Semfuko, Maelezo

HALMASHAURI ya Wilaya ya Handeni mkoani Tanga imewekeana saini na Kampuni ya Kanton Investment kutoka Jamhuri ya Watu wa China kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha kuchakata zao la mihogo, ikiwa ni juhudi za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kuvutia wawekezaji nchini.

Ujenzi wa kiwanda hicho utakaogharimu Dola milioni 10 unatarajia kuchakata tani 200 za mihogo pamoja na kusafirisha tani 400,000 za wanga kutoka katika tani milioni 1.6 za mihogo mibichi itayosafirishwa nchini China.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki Wilayani Handeni na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Kanton Investment, John Rwehumbiza wakati wa hafla ya utiaji saini wa maktaba wa makubaliano hayo iliyohudhuriwa na viongozi wa Serikali.

Rwehumbiza amesema kampuni hiyo imeanza majaribio ya kununua na kusafirisha nje ya nchi zao la Muhogo na kuonesha kupendwa raia wa China, na hivyo kuahidi kufanya uwekezaji kwa kujenga kiwanda cha wanga na kununua mihogo ya wakulima na kuisafirisha nchini humo.

Aidha ameongeza kampuni yake pia imepanga kutoa elimu kwa wakulima wa zao la muhogo kuhusu mbinu bora za uzalishaji wa zao hilo ambalo litawawezesha kutoa faida kubwa na hasa ukizingatia walaji wengi wa zao hilo wanatoka nje ya nchi ikiwepo China na Japan.

Wakati huohuo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, William Mafukwe amesema Ofisi yake itahakikisha inaweka mazingira mazuri kwa wawekezaji hao ili wafanye kazi katika mazingira wezeshi kama ilivyokusudiwa ili kuweza kuwanufaisha wakulima wa Wilaya hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe amesema Wilaya yake inayo ardhi ya kutosha ya uwekezaji katika maeneo ya kilimo na viwanda na hivyo makubaliano hayo ya awali yatasaidia kupanua wigo wa biashara ya zao la muhogo.

“Tunayo ardhi ya kutosha, tunawakaribisha wawekezaji wote na milango ipo wazi na tutatoa ushirikiano wa kutosha na malengo yetu ni kuhakikisha tunakuza uchumi wa wananchi wetu” alisema Gondwe.Ofisa Habari wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) Latifa Kigoda amesema lengo la kituo hicho ni kuhakikisha uwekezaji nchini unaleta tija kwa kuzingatia kuwa nia ya Serikali ya Awamu ya Tano ni kuifanya Tanzania kufikia nchi ya kipato cha uchumi wa kati kupitia viwanda..

“TIC nia yetu tkuona uwekezaji ukiongezeka siku hadi siku, nia ni kukuza uchumi wa Taifa pamoja na kuunga mkono Dhamira ya Mhe. Rais na Serikali ya Awamu ya Tano viwanda, hivyo ,tunaomba wawekezaji waje kuwekeza nchini,"amesema Latifa. 

Wilaya ya Handeni mkoani Tanga ina Kata 21 yenye jumla ya ekari 184,000 za kilimo cha Mihogo, ambapo uwekezaji huo unaelezwa utawezesha wawekezaji wapya kuwekeza katika zao la mihogo, hatua inayolenga kuongeza tija ya kiuchumi kwa Wilaya hiyo ambao asilimia 90 ya wakazi wake ni wakulima.

No comments: