Na Said Mwishehe,Globu ya jamii
TAASISI ya Teknolojia ya Dar es Salaam(DIT), imeamua kubuni na kuzindua mashine maalumu ya kutengenezea mkaa mbadala.
Lengo la kubuni mashine hiyo ni jitihada za DIT katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kupitia mikakati yake ya kukabiliana na uharibufu wa misitu na utunzaji wa mazingira.
Akizungumzia kuhusu umuhim wa mashine hiyo leo kwenye Maonyesho ya Wiki ya Mazingira yanayoyendelea Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Mkufunzi wa Idara ya Uhandisi wa Mitambo wa taasisi hiyo Asaph Kagina, amefafanua mashine hiyo yenye uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani tatu za mkaa kwa siku ni suluhisho tosha katika kulinda misitu hapa nchini.
Amesema kuwa mashine hiyo inayotumia mabaki ya mazao mashambani, zikiwemo pumba za mpunga, mahindi, vifuu vya nazi, pumba pamoja na makaa ya mawe, imeundwa kutokana na wazo lilitokana na ripoti maalumu ya Banki ya Dunia kuhusu hali ya mazingira, pamoja na ripoti nyingine ya aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Misitu na nyuki Dk. Felician Kilahama.
Amefafanua ripoti ya Dk.Kilahama imeeleza wazi kuwa iwapo kasi ya ukataji miti itaendelea kwa kipndi cha miaka 10 Tanzania hakutakuwa na misitu ya miti na hivyo DIT kupitia watalaamu wake wameona haja ya kutafuta njia mbadala ya kupata mkaa ambayo itakuwa sahihi katika kulinda mazingira
"Ni mashine ambayo tuaamini kama ikitumika ipasavyo itatoa mchango mkubwa kwa Taifa katika kukabiliana na tatizo la uharibifu wa mazingira ambalo kwa kipindi kirefu limekuwa na athari kubwa huku likihatarisha hatari ya kutokea jangwa katika miaka kadhaa ijayo" amesisitiza Kagina.
Amesema mashine hiyo maalumu imetengenezwa na wanafunzi watatu wanaosoma katika taasisi hiyo waliokaa chini na kuja na wazo la kutengeneza mashine hiyo ili kutimiza ndoto zao za ulinzi wa mazingira na misitu kwa ujumla, kitu ambacho wamefanikiwa.
Aidha alisema mashine hiyo inayotumia nishati ya umeme pamoja na dizeli, imeundwa kwa kuzingatia mazingira ya mijini na vijijini huku ikivilenga zaidi vikundi mbalimbali vya ujasiramali ili kuviwezesha kuja na mradi huo utakaovisaidia kujitengenezea faida.
Alisema gharama za ununuzi wa mashine hiyo inatokana na uhitaji wa mteja kwa kuzingatia ukubwa, huku gharama ya juu kabisa ikiwa ni cha Sh Milioni 5, na ikiwa na uwezo wa kutengeneza faida kuanzia kiasi cha Sh 900,000 kwa siku moja.
Ameziomba taasisi za kifedha kuwasadia wajasiriamali kwa kuwapa mikopo ili waweze kununua mashine hiyo na hivyo kujikwamua kiuchumi sambamba na kuunga mkono juhudi za kukabiliana na uharibifu wa mazingira nchini.
Michuzi Blog imeshuhudia idadi kubwa ya wananchi ambao wanafika kwenye viwanja hivyo kufika banda la DIT ambapo pamoja na kuelezwa mambo mbalimbali yanayofanywa na taasisi hiyo wengi wao wamekuwa na shauku ya kutaka kujua zaidi kuhusu mashine hiyo ambapo baadhi yao wameelezea matumaini yao kuwa ikitumika vizuri itakuwa mkombozi katika kulinda mazingira nchini.
Mkufunzi wa Idara ya Uhandisi wa Mitambo kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam(DIT)akifafanua jambo kwa baadhi waandishi waliotaka kufahamu kwa kina machine ya kuzalisha mkaa mbadala ambayo imebuniwa na taasisi hiyo
Mkufunzi wa Idara ya Uhandisi Mitambo Katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam(DIT) Akita maelezo ya machine maalum ambayo imebuniwa na taasisi hiyo ambayo inazalisha mkaa mbadala
Mashine ya kutengeneza mkaa mbadala ambayo imebuniwa na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT).
No comments:
Post a Comment