Tuesday, May 8, 2018

Wananchi MBEYA watakiwa kufanya mazoezi


-->
Taasisi ya Mo Dewji imekuwa miongoni mwa wadhamini ambao kwa kushirikiana na Taasisi ya Tulia Trust wamewezesha kufanyika Tulia Marathon 2018, ikiwa ni mara ya pili kufanya hivyo baada ya mbio za mwaka jana ambazo zilikuwa na mafanikio makubwa.

Akizungumza katika mbio hizo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla alisema watu wengi hawana utaratibu wa kufanya mazoezi jambo ambalo sio zuri kiafya na hivyo kuwataka wananchi kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao.

Aidha Makalla alimpongeza Naibu Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Mwanzilishi wa Taasisi ya Tulia Trust, Dkt. Tulia Ackson kwa kuanzisha mbio hizo ambazo zinasaidia sana mkoa huo kuboresha sekta ya afya na elimu. 

“Michezo ni muhimu sana kwa afya zetu … tujifunze na sisi tuanze kufanya mazoezi sababu ni muhimu sana kwa afya zetu. Mimi hapa nilipo sijawahi kuumwa maralia tangu nikiwa kidato cha kwanza lakini sababu nafanya mazoezi. Ukiwa unafanya mazoezi magonjwa haya ya pressure unaachana nayo,” alisema na kuongeza.

“Niseme tunafaidika sana kupitia Trulia Trust kwa mambo ambayo anayafanya, anaupenda mkoa wetu ameboresha miundombinu katika elimu na afya. Alianza kwenye ngoma na sasa anafanya Tulia Marathon na kutokana na marathon hii anakwenda kusaidia afya na elimu.”

Naye Meneja Miradi wa Taasisi ya Mo Dewji, Rachel Chengula alisema wameamua kushirikiana na Tulia Trust ili kusaidia kuokoa maisha ya Watanzania ambao wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosa huduma bora za afya.

“Tunatambua kwamba maisha ya mwanadamu yanaanza mimba inapotungwa hivyo ni muhimu sisi kama sehemu Watanzania tuliojengwa katika misingi ya upendo kuona ni muhimu kushirikiana na serikali na wadau wengine kama Tulia Trust kuweka mazingira bora ya wodi za uzazi ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi nchini,

“Tunapongeza hatua ambazo zinachukuliwa na serikali za kukarabati vituo vya afya katika Halmashauri mbalimbali nchini kwa kujenga na kukarabati majengo ya upasuaji, wodi za wazazi na watoto pamoja na maabara. Tunaamini jitihada hizi zitasaidia kupunguza vifo vya kina mama na watoto nchini,” alisema Chengula.

Awali akizungumza kuhusu Tulia Marathon 2018, Dkt. Tulia alisema fedha ambazo zimepatikana katika mbio za mwaka huu zitatumika kusaidia kuboresha sekta ya elimu na afya kama ilivyokuwa mwaka jana na lengo lao ni kushirikiana na serikali ili kuwezesha wananchi wapate huduma bora za kiafya na elimu bora.
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Mwanzilishi wa Taasisi ya Tulia Trust, Dkt. Tulia Ackson akiongoza wanariadha waliojitokeza kukimbia katika Tulia Marathon 2018 zilizofanyika Jijini Mbeya.


Naibu Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Mwanzilishi wa Taasisi ya Tulia Trust, Dkt. Tulia Ackson akielezea mafanikio ambayo Tulia Marathon iliyapata kwa mwaka uliopita na mipango ya mwaka huu.
Meneja Miradi wa Taasisi ya Mo Dewji, Rachel Chengula akizungumza kuhusu Tulia Marathon 2018 na shughuli ambazo taasisi yao inafanya kwa jamii. Kulia kwake ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Mwanzilishi wa Taasisi ya Tulia Trust, Dkt. Tulia Ackson.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla akizungumza namna Tulia Marathon inawasaidia kuboresha sekta ya afya na elimu na kutoa pongezi kwa Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson.

Meneja Miradi wa Taasisi wa Mo Dewji, Rachel Chengula akikabidhi medali na fedha taslimu kwa washindi wa mbio za 5 KM zilizohusisha wanafunzi katika Tulia Marathon 2018 zilizofanyika Jijini Mbeya.



No comments: