Sunday, May 27, 2018

WAKULIMA KAKONKO WAHIMIZWA KULIMA KILIMO CHA BIASHARA

Na Rhoda Ezekiel Kigoma, 

WAKULIMA wilayani Kakonko mkoani Kigoma, wametakiwa kulima kilimo cha biashara na kuachana na kilimo cha kujikimu wenyewe ili kuweza kuondokana na umasikini.

Mwito huo ulitolewa jana katika Kijiji cha Kiga wilayani hapo na Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Kigoma, Josephu Lubuye wakati wa ugawaji wa mashine ya kuchakata Muhogo kwa kikundi cha Mwendo wa saa, iliyo tolewa na Shirika la BTC kupitia mradi wa kilimo wa ENABEL unaotekelezwa na Serikali ya Ubelgiji na Tanzania.

Lengo ni kuendeleza kilimo cha muhogo na maharage kwa kuwakopesha wakulima mashine na kuwapatia mafunzo ya namna ya kulima kitaalamu.

Hivyo Lubuye amesema wakulima wanatakiwa kubadilika na kuanza kilimo cha biashara na mashine hiyo waliyoipata itumike kuchakata mazao mengi ya mihogo waliyolima kutokana na maombi na aandiko lao la kuomba mashine ya kuchakata mihogo.

Amesema hiyo itaongeza uzalishaji wa zao hilo kwa wingi ili wakulima wengine wajifunze kupitia kikundi hicho kutokana na uzalishaji watakaoufanya kupitia mafunzo ya kilimo cha biashara waliyo yapata kuongeza uzalishaji na ubora.

Akikabidhi mashine hiyo yenye thamani ya Sh.milioni mbili na yenye uwezo wa kuzalisha kilo 700 kwa saa moja na hufanya kazi kwa muda wa saa nane, Mkuu wa wilaya ya Kakonko kanali Hosea Ndagala amewataka wakulima kuacha kuuza mazao ambayo hayajaongezwa thamani.

Amefafanu kwa kutumia fursa hiyo ya mashine waliyopatiwa itawasaidia kuinua uchumi wao na kulima kitaalamu ilikuongeza uzalishaji.Aidha Mkuu huyo amesema Serikali ya Awamu ya tano ina lengo la kuongeza viwanda na kikundi cha mwendo wa saa wameonesha nia ya uwanzishwaji wa viwanda kwa kuonesha mfano.

Amewataka wananchi wengine kuja kujifunza kupitia vikundi vilivyo fanikiwa na waache maneno ya kuongea na sasa waanze kuanzisha viwanda kwa vitendo ."Niwapongeze wanakikundi wa Mwendo wa saa kwa juhudi mnazozifanya kuhakikisha mnaondokana na umasikini kwa kilimo cha Muhogo, niwaombe wakulima mjitahidi kulima kwa kufuata maelekezo ya wataalamu ilikilimo mtakacho lima kiwe chenye tija kitakacho wasaidia kutoka mahali fulani na kuinua uchumi wenu.

" Serikali imewapatia mashine hii muitumie kuzalisha zaidi masoko yapo na wafadhiri wa mradi huu wameahidi kuwatafutia masoko,hivyo niwaombe muitumie fursa hii na kuwafundisha wengine waige kwenu", amesema Kanali Ndagala. 

Amewahimiza kuwa ili kuwafikia ambao wamefika mbali ni lazima kuongeza kasi ya uzalishaji, na kwa hatua walioifikia kikundi hicho cha kutoka kwenye vikoba na kuingia kwenye Sacoss na kuwa na hekari 16 za muhogo aliwaomba wabadilike kulima kibiashara.

"Achaneni kulima kilimo cha kujikimu ili kuondokana na umasikini,kilimo cha kisasa na kuacha kulima kilimo kisicho na tija na kutumia mbegu bora, kusikiliza wanayo washauri wataalamu wa kilimo na matokeo wameanza kuyaona," amesisitiza.

Kwa upande wake Katibu wa Kikundi cha Mwendo wa saa Daudi Bukuku amesema kikundi kina wanachama 25 ambapo kati yao wanawake 12 na wanaume 13.Ameongeza kikundi kilianza kwa kununua na kukopeshana hisa huondeshwa kwa kuzingatia sheria na kufafanua wanayo mifuko mitatu ya kujiingizia kipato, mfuko wa hisa ambao una kiasi cha Sh. milioni 13, mfuko wa elimu na afya wenye Sh.milioni mbili na mfuko wa faini na zawadi Sh.300,000.

Amesema kikundi kinaendesha shughuli za kilimo kwaajili ya kukuza kipato ambapo kina hekari tano za migomba ya kisasa, hekari 16 za mihogo na hekari mbili za maharage katika vijiji vya kitangaza na mkombozi.Hata hivyo matarajio ya kikundi ni ifikapo mwaka 2021 kiwe na hekari 30 za mihogo na hekari moja moja kwa kila mwanamundi na kikundi kuhama kutoka vikoba na kuwa Sacoss.

Kuhusu changamoto amesema ni ukosefu wa mashamba ya kutosha na masoko pamoja na mafunzo ya mara kwa mara ya kuwaelimisha namna bora ya kilimo.
 Mkuu wa wilaya ya Kakonko kanali Hosea Ndagala akikabidhi  mashine  ya kuchakata muhogo,yenye thamani ya Sh.milioni mbili na yenye uwezo wa kuzalisha kilo 700 kwa saa moja.DC Ndagala amekabidhi hiyo mashine ya kuchakata Muhogo kwa kikundi cha Mwendo wa saa, iliyo tolewa na Shirika la BTC kupitia mradi wa kilimo wa ENABEL unaotekelezwa na Serikali ya Ubelgiji na Tanzania.
 Sehemu ya shamba ka Muhogo. 
 Mkuu wa wilaya ya Kakonko kanali Hosea Ndagala akitumbukiza muhogo kwenye mashine ya kuchakata muhogo,ili kujionea ufanyaji wake kazi,mashine hiyo ina uwezo wa kuzalisha kilo 700 kwa saa moja.
Mihogo ilioandaliwa tayari kwa kuchakatwa na mashine

No comments: