SERIKALI imewaasa viongozi wa dini waeuepuke migogoro ya mara kwa mara katika Makanisa yao na badala yake waendelee kuwajenga waumini wao wakue kiroho na kujenga dhana ya umoja na upendo katika Taifa.
Pia imesema inawashukuru viongozi wa dini na madhehebu yote ya dini kwa kuendelea kuiombea nchi amani, mshikamano na utulivu, jambo ambalo linaongeza chachu kubwa kufikia mafanikio ya maendeleo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi.
Hayo yamesemwa leo (Jumapili, Mei 20, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika ibada ya kutawazwa Askofu Dkt. Maimbo Mndolwa wa Dayosisi ya Tanga kuwa Askofu Mkuu wa saba wa Kanisa la Anglikana Tanzania. Ibada hiyo imefanyika katika Kanisa Kuu la Roho Mtakatifu Dayosisi ya Central Tanganyika Jijini Dodoma.
“Nawaombeni wote kwa ujumla wetu, tuendelee kutumia Makanisa yetu kuombea Taifa hili ili tuendelee kuishi kwa amani, upendo na mshikamano”. Watu wa Mungu ni watu wa Upendo, watu wa Mungu ni watu wa amani, watu wa Mungu ni watu wa kiroho”.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa “haitarajiwi kuona watu wa Mungu wakiwa katika mstari wa mbele kuchochea migogoro, kuvunja amani ya Kanisa na kuongoza makundi yanayopingana katika kazi ya Bwana”.Amesema jukumu la makanisa ni kuwajenga waumini kukua kiroho, na kazi ya kuwaongoza watu wamjue Mwenyezi Mungu, ambapo amewaomba imani yao iwe moja na matendo yao yafanane na yale ya Kristo Yesu wanayemuamini.
Waziri Mkuu amesema kuwa nchi haiwezi kupata mafanikio ya kiuchumi na kijamii bila kuilinda amani iliyopo, hivyo amewaomba warejee kumbusho la maandiko Matakatifu katika Waebrania 12:14 “Tatufeni kwa bidii kuwa na Amani na watu wote”.
Pia Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi hao na wananchi kwa ujumla waendelee kuwaombea viongozi wa Tanzania hususani Rais Dkt. John Magufuli, kuendelea kuwa na afya njema, busara, upendo, hekima katika kuiongoza nchi yetu.
Waziri Mkuu ambaye amemuwakilisha Rais Dkt. Magufuli katika ibada hiyo amesema Serikali inatambua ushirikiano uliopo kati ya madhehebu mbalimbali ya dini nchini kwa ujumla wake na kwamba ushirikiano huo ni wa kihistoria.
Amesema mara zote madhehebu ya dini yamekuwa yakisaidiana na Serikali katika kutoa huduma za elimu, afya, maji na makundi maalum kama vile yatima, wazee, walemavu, wajane na huduma hizo zimekuwa zikitolewa kwa Watanzania wote bila ubaguzi wa aina yoyote. “Mambo haya hayawezi kupatikana nchini bila ya kuwa na amani”.
Kwa upande wake Askofu Dkt. Mndolwa baada ya kutawazwa aliahidi kulitumikia kanisa la Anglikana katika kweli, haki na upendo.
“Naahidi kwa makini kwamba nitaistahi na kudumisha na kuilinda Imani, haki na uhuru wa Kanisa la Anglikana Tanzania na kulitumikia katika kweli, haki na upendo, nisijifanye kuwa bwana juu ya urithi wa Mwenyezi Mungu, bali katika mambo yote nioneshe kielelezo kwa kundi la Kristo. Mungu nisaidie,”.
Askofu Dkt. Mndolwa anashika wadhifa huo baada ya aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Askofu Jacob Chimeledya kumaliza muda wake. Askofu Chimeledya alitawazwa mwaka 2013.
Maaskofu wengine waliowahi kuongoza kanisa hilo tangu kuasisiwa kwake nchini ni John Thomas Mhina Sepetu (1970-1978), Askofu Musa Kalemo Kahurananga (1979-1983), Askofu John Auckland Ramadhani (1984-1997), Askofu Donald Leo Mtetemela (1998-2008), Askofu Valentino Leonard Mokiwa (2009-2013).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMAPILI, Mei 20, 2018.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Askofu Mkuu wa saba wa kania la Anglikana Tanzania, Maimbo Fabian Mndolwa baada ya ya Askofu huyo kutawazwa kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, jijini Dodoma, Mei 20, 2018. Waziri Mkuu alimwakilisha Rais John Pombe Magufuli.
Askofu Mkuu wa saba wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Maimbo Fabian Mndolwa akila kiapo wakati alipotawazwa kuw Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, jijini Dodoma, Mei 20, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kasim Majliwa akisalimiana na Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikan Tanzania, Jaco Chimeldya katika sherehe ya kumtawaza Askofu Mkuu wa Saba wa kanisa hilo, Maimbo Fabian Mdolwa jijini Dodoma, Mei 20,2018. Mheshimiwa Majaliwa alimwakilisha Rais John Pombe Magufuli katika sherehe hiyo.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Askofu Mkuu wa saba wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Maimbo Fabian Mndolwa akizungumza na waumini wa kanisa hilo na wageni waalikwa baada ya kutawazwa kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, jijini Dodoma, Mei 20, 2018. Waziri Mkuu alimwakilisha Rais John Pombe Magufuli katika sherehe hiyo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza katika Rais John Pombe Magufuli kwenye sherehe ya kumtawaza Askofu Mkuu wa saba, Maimbo Fabian Mndolwa, jijini Dodoma, Mei 20, 2018.2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Askofu Mkuu wa saba wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Maimbo Fabian Mndolwa baada ya Askofu huyo kutawazwa kuwa Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, jijini Dodoma, Mei 20, 2018, kulia ni mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa. Waziri Mkuu alimwakilisha Rais John Pombe Magufuli.
Spika wa Bunge Job Ndugai akisalimiana na Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania , Oscar Mnunga katika sherehe ya kumtawaza Askofu Mkuu wa Saba wa kanisa hilo, Maimbo Fabian Mndolwa jijini Dodoma, Mei 20, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge akizungumza na Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Jacob Chimeledya katika sherehe ya kumtawaza Askofu Mkuu wa Saba wa Kanisa hilo, Maimbo Fabian Mndolwa jijini Dodoma, Mei 20, 2018.
No comments:
Post a Comment