Wednesday, May 30, 2018

SERIKALI YAAGIZA WAMACHINGA WATENGEWE MAENEO YA KUFANYIA BIASHARA

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo akiongea na wamachinga wakati  wa kufungua  Mkutano Mkuu wa Shirika la umoja wa wamachinga Tanzania- SHIUMA leo uliofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Dodoma, Jijini Dodoma.
 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo akiongea na wamachinga wakati  wa kufungua  Mkutano Mkuu wa Shirika la umoja wa wamachinga Tanzania- SHIUMA leo uliofanyika katika ukumbi wa shule ya Sekondari Dodoma, Jijini Dodoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Seleman Jafo  akiongea na baadhi ya viongozi wa shirika la umoja wa wamachinga Tanzania – SHIUMA leo alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu uliofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari ya Dodoma, Jijini Dodoma.

Na Angela Msimbira,

Wakuu wa Wilaya wameagizwa kuzisimamia halmashauri nchini kuhakikisha kuwa zinatenga maeneo maalum ya kufanyia biashara ndogondogo (machinga) ili  waweze kuendesha shughuli zao bila kuvunja sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa na serikali. 


Agizo hilo limetolewa na Waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Selemeni Jafo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Shirika la umoja wa wamachinga Tanzania – SHIUMA uliofanyika leo katika ukumbi wa shule ya Sekondari ya Dodoma, Jijini Dodoma.



Alisema Wakuu wa Wilaya wana wajibu wa kuratibu na kuhakikisha kuwa maeneo ya kufanyia bishara kwa wamachinga yanatengwa na Halmashauri ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa utaratibu bila kuvunja sheria za nchi. 



Aliongeza kuwa wamachinga ni watu muhimu katika kukuza uchumi wa Tanzania kwa kuwa wafanyabiashara wadogo ndio wanaoleta muunganiko wa watu katika kada mbalimbali wakiwemo wasomi wenye shahada, astashaada, kidato cha sita, kidato cha nne, darasa la saba na wasiosoma kabisa wote huunganika na kufanyabiashara kama wamachinga.



Alisema kati ya watanzania milioni 50, walioajiriwa serikalini na sekta ya umma ni 520,000, hivyo kundi kubwa ni la watu ambao ama wamejiajiri au wameajiriwa katika sekta binafsi. 



“Lakini kundi kubwa ni wale watu wanaojishughulisha kwa kutafuta riziki zao wenyewe ambao watu hao ndio unapata asilimia kubwa wako katika kundi la wamachinga,” alisema Mhe.Jafo na kuongeza:



“Utakuta mtu anafanyabishara katika mazingira magumu ambayo yanamfanya kila wakati kutokuwa na uhakika wa kupata kipato cha siku jambo ambalo linaathiri familia yake na kuongeza umaskini nchini, hivyo ifike mahali wakuu wa Wilaya waweke mikakati ya kuhakikisha wamachinga wote wanapatiwa maeneo bora ya kufanyia biashara ili wajikwamue kiuchumi,  “alisisitiza Waziri 



Aliongeza kuwa Serikali imejiwekea mkakati wa kutengeneza masoko mazuri na ya kisasa kwa kuweza kuweka mazingira bora kwa wamachinga kufanya biashara zao katika maeneo stahiki.



Aidha Waziri Jafo alisema kuwa Viongozi wanatakiwa kutafakari na kutatua kero ya maeneo kwa ajili ya kufanyia biashara wamachinga, hivyo serikali imeanza mpango mkakati  wa ujenzi wa masoko mazuri ya kisasa ili wafanyabishara waweze kufanya kazi katika mazingira bora na tayari imetenga shilingi bilioni 149 kwa ajili ya ujenzi wa masoko, stendi za kisasa na viwanda vidogo.



 “Nimetoa maagizo soko lolote litakalojengwa lazima mustakabali wa wafanyabiashara wadogo wadogo waliokuwepo awali umejulikana na kuwa kipaumbele kwa kupatiwa maeneo ya kufanyia biashara pindi majengo hayo yanapokamilika hivyo viongozi wa halmashauri wahakikishe wanatoa kipaumbele kwa wafanyabiashara waliokuwepo awali,” alisema Jafo.



Alisema kuwa Serikali imekuwa ikiwekeza katika miradi mikubwa ikidhani inawagusa maskini lakini kwa bahati mbaya masoko mengi yanayojengwa wanaonufaika ni watu wenye fedha na kuwaacha wafanyabiashara waliokuwepo awali kabla soko kujengwa. 



Hivyo nawaagiza Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wananchi masikini wanapatiwa nafasi katika masoko hayo ili waweze kujiongezea kipato.Amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri wote nchini kuhakikisha kuwa kabla soko halijaanza kujengwa kufanyike tathmini ya wafanyabishara waliokuwepo awali ili wawe kipaumbele pale soko linapokamilika.






Wakati huohuo Mhe. Jafo amewataka wamachinga nchini kuhakikisha wanajiunga na bima iliyoboreshwa ili iwawezeshe kuwasaidia pale wanapokuwa wagonjwa wao na familia zao kwa kuwa afya ni uhai.

No comments: