Wednesday, May 30, 2018

MNYETI AAGIZA MANYARA IKAMILISHE VIWANDA 100

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Pastory Mnyeti akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, wakiwemo maofisa tarafa, madiwani, watendaji wa kata, vijiji, walimu na wenyeviti wa vijiji, juu ya kufanya kazi kwa uadilifu na kutumikia jamii, kulia ni Mkuu wa Wilaya hiyo mhandisi Raymond Mushi.
Mkuu wa Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, Mhandisi Raymond Mushi akizungumza na wananchi wa Kata ya Madunga juu ya kufanya kazi na kuwahusia kuwa siku mbili ambazo mtu hawezi kufanya chochote ni jana na kesho hivyo waitumie siku ya leo kwa kutimiza wajibu wao, kulia ni Mkuu wa Mkoa huo Alexander Mnyeti na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Nicodemus Tarmo.
Mkuu wa Wilaya ya Babati Vijijini Mkoani Manyara, Vrajilal Jituson, akizungumza na wananchi wa Kata ya Madunga ambao wanachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo yao ikiwemo suala la elimu.
Mbunge wa viti maalum wa mkoa wa Manyara, Esta Mahawe akizungumza na wananchi wa Kata ya Madunga ambapo alijitoa mashuka 10 kwa ajili ya wagonjwa watakaotumia kwenye zahanati ya kijiji hicho iliyozinduliwa na Mkuu wa mkoa huo Alexander Mnyeti.


Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti ameziagiza Halmashauri za Wilaya za Mkoa huo kuhakikisha zinatekeleza agizo la uanzishwaji wa viwanda 100 na hadi mwezi Septemba mwaka huu viwe vimekamilika. 

Mnyeti akizungumza na watumishi na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, alisema kila halmashauri ya mkoa huo wenye halmashauri saba, inapaswa iwe na viwanda 15. Mnyeti alisema serikali ilitoa agizo la kila mkoa uanzishe viwanda 100 hivyo na mkoa wa Manyara nao unapaswa kuhakikisha unatekeleza agizo hilo kwa kila halmashauri kuwa na viwanda 15. 

Alisema agizo hilo linatakiwa kutekelezwa kwa kila sekta ikiwemo kilimo na mifugo ambazo ndizo shughuli kuu za kiuchumi kwa wananchi wengi wa mkoa huo. “Watumishi wa umma wanapaswa kutambua kila taaluma waliyoisomea wanapaswa kuwekeza kwenye fikra ya viwanda kwa kuelimisha jamii juu ya umuhimu wa sekta hiyo,” alisema Mnyeti. 

Aliwapongeza mkuu wa wilaya hiyo mhandisi Raymond Mushi na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Hamis Malinga kwa kutekeleza agizo hilo la uanzishwaji wa viwanda vipya. “Kwenye miezi mitatu iliyopita Halmashauri ya Babati mlikuwa mmeshafanikisha uanzishwaji wa viwanda nane na hadi kufikia mwezi Septemba mtakuwa mmekamilisha viwanda 15 hongereni sana,” alisema Mnyeti. Mkuu wa wilaya ya Babati, mhandisi Raymond Mushi alisema wananchi wa eneo hilo ni wachapakazi wazuri na hujishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi, ujasiriamali na nyinginezo.

Mushi alisema kwa kiasi kikubwa wananchi wa wilaya yake ni wachapakazi huku wakishirikiana na serikali katika kufanikisha maendeleo mbalimbali.Mbunge wa Jimbo la Babati Vijijini, Vrajilal Jitu Son alisema wameshajipanga kutekeleza hilo kupitia viwanda mbalimbali vilivyopo jimboni humo. Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Babati, Hamis Malinga alisema kwa kiasi kikubwa wamefanikisha utekelezaji wa vipaumbele mbalimbali ikiwemo elimu, afya na maji.“Kwenye suala la migogoro ya ardhi, kamati ya ulinzi na usalama chini ya Mwenyekiti wake mheshimiwa mkuu wa wilaya kwa kiasi kikubwa imefanikisha kusuluhisha japo kuwa maeneo machache yaliyobaki na yanaendelea kufanyiwa kazi,” alisema.

Jituson alisema kwenye eneo hilo kuna viwanda mbalimbali vipya vilivyojengwa vikiwemo vya mafuta, sukari, kukoboa mpunga, unga, na kiwanda cha vyakula vya mifugo. Alisema kupitia nafasi ya vijiji vingine 30 kupatiwa umeme wa Rea awamu ya tatu, itasaidia kuanzisha viwanda vidogo na vya kati kwa wajasiriamali mbalimbali waliopo kwenye jimbo hilo. 

Mkazi wa Kijiji cha Endanachang’ John Lorry alisema serikali na sekta binafsi zinapaswa kujipanga na kuanzisha kiwanda cha biskuti ili zao la mbaazi lipate soko. Lorry alisema changamoto ya soko la mbaazi imekuwa kero kwa jamii ila kupitia viwanda wakulima wengi wa eneo hilo wataweza kunufaika kwa kupata sehemu ya uhakika ya kuuza zao hilo.

No comments: